Na Judith Ferdinand,Timesmajira online, Mwanza
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linamshikilia Mchungaji wa kanisa la Neno na mkazi wa Mwangika wilayani Sengerema kwa tuhuma za kufanya shughuli za kanisa bila kuwa na kibali cha usajili kinyume na sheria pamoja na kutoa mahubiri potofu kwa waumini wake.
Hayo yamebainishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Wilbroad Mutafungwa jijini hapa ambapo ameeleza kuwa Juni Mosi mwaka huu majira ya saa 8 mchana huko katika kijiji cha Chema, tarafa ya Kahunda, Wilaya ya Sengerema,mkoani hapa kulipatikana taarifa kuwa kuna mtu anatoa mahubiri ya kupotosha jamii.
Ambapo aliwataka waumini wake wasiende hospitali kupata huduma ya matibabu pindi wakiugua au kuuguliwa na badala yake wapelekwe kwenye kanisa lake liitwalo Neno kwaajili ya kuombewa na kupata uponyaji wa magonjwa yanayo wakabili.
Mutafungwa ameeleza kuwa mara baada ya taarifa hiyo Askari Polisi walifika katika kanisa hilo lililopo kijiji cha Chema na kufanikiwa kumkamata Herman Magigita(60) ambaye ni Mchungaji wa kanisa hilo kwa tuhuma hizo za kufanya shughuli za kanisa bila kuwa na kibali cha usajili kinyume cha sheria na kutoa mahubiri potofu kwa waumini wake.
Pia ametoa wito kwa wakazi wa Mkoa wa Mwanza kuendelea kuliamini jeshi hilo na kutoa taarifa zaidi za uhalifu na wahalifu wote ili hatua za kisheria ziendelee kuchukuliwa dhidi yao.
“Kamwe tusifiche uhalifu kwa namna yoyote ile, Jeshi la Polisi tumejipanga vizuri kuhakikisha kuwa taarifa hizo zinafanyiwa kazi kwa weledi na uaminifu mkubwa,”ameeleza Mutafungwa
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa