Na David John, TimesMajira Online, Dar es Salaam
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema mchakato wa kupitia fomu za makada wa chama hicho waliojitokeza kugombea urais upo katika hatua za mwisho kukamilisha.
Chama hicho kimesema mara baada ya mchakato kukamilika, utaratibu wa kuchukuwa fomu hizo za urais ikiwamo na za ubunge,udiwani utatangazwa na kuwekwa hadharani.
Akizungumza na waandishi wa habari Makao Makuu wa CHADEMA Kinondoni Jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika, pamoja na mambo mengine amesema mchakato wa kupitia fomu za wagombea urais upo katika hatua za mwisho, lakini chama kitapanga siku nyingine za kuzungumzia suala hilo.
Hata hivyo, alielezea kusikitishwa kwake na kauli ya Mkuu wa Jeshi la Polisi ncjini, IGP Simon Sirro, ya kuwaonya wanasiasa wanaosema watalinda kura zao. Mnyika amesema wao kama chama watalinda Kura zao kwa nguvu ya umma.
Wakati huo huo CHADEMA imelitaka Jeshi la Polisi nchini kuonesha ushahidi wa CCTV Kamera ili kuthibitisha madai kuwa Mwenyekiti wa Chama hicho, Freeman Mbowe alilewa kama ambavyo ilielezwa na Jeshi hilo.
“Mwenyekiti Freeman Mbowe alishambuliwa na alipata madhara katika moja ya sehemu za mwili wake, lakini mbaya zaidi Jeshi la Polisi limeendelea kukaa kimya na badala yake wanatoa taarifa ambazo hawana ushahidi.
Tunalitaka Jeshi la Polisi kujitokeza hadharani na kutoa ushahidi wa CCTV Kamera, “amesisitiza Mnyika “Kwa nini Jeshi la Polisi wanashindwa kuja na majibu wakati madaktari ambao walimpokea Mwenyekiti Mbowe wangeweza kutoa ushahidi.”
Amesema suala hilo linahitaji ushahidi vinginevyo ni kuendelea kuwachafua viongozi wa chama hicho kwa wananchi katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.
More Stories
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa
NLD kipo tayari kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa