May 18, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwanasiasa mkongwe, Pereira Ame Silima (kulia) akipokea makabrasha ya fomu za kugombea Urais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar

Urais Z’bar: Silima kuinua uchumi wa Zanzibar

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Zanzibar

MAKADA wanaoomba kusimamishwa na Chama Cha Mapinduzi CCM kuwania kiti cha Urais Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba, mwaka huu wamezidi kuongezeka na kufikia 29.

Idadi ya wanaowania kusimamishwa na CCM kuwania kiti hicho ambapo Rais wa sasa Dkt. Ali Mohamed Shein anamaliza muda wake, imefikia 29 baada ya jana wanasiasa wengine wawili kujitokeza kuchukua fomu.

Mwanasiasa mkongwe, Pereira Ame Silima akisaini kitabu baada ya kufika katika ofisi za CCM Zanzibar

Kuongezeka kwa makada hao kunatafsiriwa kwamba kunachangiwa na kukua kwa demokrasia ndani ya Chama hicho, huku wapembuzi wa masuala ya kisiasa wakisema ni mapema mno kujua atakayesimamishwa na CCM kupeperusha bendera hiyo.

Hadi jana mawaziri sita tayari wamejitosa kwenye kinyang’anyiro hicho, ambapo kati ya waliochukua fomu wanaume ni 26 na wanawake watatu.

Jana ilikuwa zamu ya mwanasiasa mkongwe, Pereira Ame Silima (61) ambapo alichukua fomu za kuomba kusimamishwa na CCM kuwania kiti cha urais Zanzibar.

Silima alichukua fomu ya kuwania nafasi hiyo kwenye Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui. Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa fomu, Silima amesema kikubwa kilichomsukuma ni nia yake thabiti ya kukuza uchumi wa wananchi wa Zanzibar.

Mwanasiasa mkongwe, Pereira Silima akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) baada ya kuchukua fomu za kugombe kiti cha Urais wa Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu wa 2020

Alifafanua kuwa licha ya viongozi waliopo na waliotangulia kufanya kazi nzuri, lakini ameona kuna changamoto katika ukusanyaji mapato ya ndani na kwamba kasi yake haiendani na uwezo wa kuzalisha.

“Nchi inahitaji maendeleo ya kiuchumi yatakayochagiza ukuaji kipato cha taifa na mwananchi mmoja mmoja, lakini sasa kipato cha wananchi ni kidogo na hivyo wengi kuangukia kwenye umaskini.

Kama nikipata ridhaa ya kuongoza nitahakikisha taifa linapiga hatua kimaendeleo,” amesema Silima.

Kwa upande wa ukuaji kiuchumi, kuhusiana na kuongeza wigo wa ukusanyaji kodi, Silima ambaye pia ni Mtaalam wa masuala ya Usimamizi wa Fedha na Biashara za Kimataifa amesema Zanzibar kwa sasa inategemea sekta za Utalii na Bahari kukuza mapato jambo ambalo linahitaji kufanyiwa maboresho.

“Uchumi wa Zanzibar unategemea sekta chache ikiwemo utalii na uchumi wa bahari ambao haujawekezwa ipasavyo, hivyo kama nitachaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar jukumu langu la kwanza litakuwa ni kuhakikisha kunakuwa na miundombinu ya kutosha ya kukuza uchumi,” amesema.

Kuhusiana na umoja na mshikamano, Silima amesema kwa sasa Zanzibar inahitaji jamii yenye umoja kuliko iliyopo sasa katika upatikanaji wa huduma muhimu kama elimu bora, afya na maji, yaani asiwepo wa kumwogopa mwenzake kwa sababu yoyote ile.

“Baadhi ya wanasiasa walitugawa Wanzanzibar kutokana tu na itikadi za kisiasa hadi kufikia watu kuogopana, katika zama zangu kila mtu atakuwa huru kufanya vile atakavyo katika misingi ya kisiasa au kidini ili mradi tu havunji katiba ya nchi,” amesema Silima.

Kwa upande wa ustawi wa jamii, Silima ambaye ni mtaalam katika Utayarishaji na Uchambuzi wa Sera mbalimbali amesema atatumia uzoefu wake kuhakikisha Zanzibar inakuwa na mkakati maalum wa kukomesha vitendo vya unyanyasaji wa watoto na wanawake.

Kwa mujibu wa Silima licha ya viongozi waliotangulia kufanya juhudi mbalimbali za udhibiti vitendo hivyo, matokeo hayajawa mazuri kulingana na matarajio ya wananchi.

“Nimechoka kuchagua na kuwa mpiga makofi, sasa naomba ridhaa ya chama na baadaye wananchi ili niweze kusimamia hivi vitu mwenyewe, huku nikikuza sekta za kilimo na gesi ambayo haijawa tayari, hata mimi nina mchango mzuri kama nitapata fursa hiyo,” alimazia Silima.

Silima licha ya kushika nyadhifa mbalimbali ndani ya Serikali ya Zanzibar ikiwemo Katibu Mkuu wa Wizara za Biashara Masoko na Utalii, Kilimo, Mifugo na Maliasili tangu Machi 2017 hadi sasa amekuwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Dodoma.

Kielimu, Silima aliyewahi kutunukiwa tuzo ya mwanafunzi bora wa Shahada ya Kwanza ya Misitu kwa miaka mitatu mfululilizo, ni msomi mwenye Shahada ya Uzamili ya Mipango ya Usimamizi wa Misitu kutoka Chuo Kikuu cha Helsinki, Finland.