May 3, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mbunge Chikota ampongeza Rais Samia

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

MBUNGE wa Jimbo la Nanyamba
Abdallah Chikota amempongeza Rais Dk.
Samia Suluhu Hassan kwa kuanzisha kongani ya viwanda vya kubangua korosho mkoani Mtwara.

Alitoa pongezi hizo jana bungeni jijini hapa
wakati wa mjadala wa bajeti ya Ofisi ya Rais TAMISEMI 2024/25, alisema kongani hiyo itasaidia uzalishaji wa ajira kwa wakazi wa mkoa huo.

“Tunamshukuru Rais kwa mradi wa
umwagiliaji wa Arusha chini, ujenzi wa viyuo vya afya vitatu, mradi wa TACTIC, ujenzi wa stendi mpya ya mabasi na ujenzi wa barabara ya lami kilomita tano,” alisema Chikota.

Alimpongeza Waziri wa Ofisi ya Rais
TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa na
Manaibu Waziri wake kwa uchapakazi wao
na kushughulikia hoja za wabunge.

Hata hivyo, alisema jimboni kwake yapo
matatizo yanayohisiana na miundombinu
ambapo mbali na kuupungeza Wakala wa
Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) alisema wakala huo unakabiliwa na upungufu wa Wahandisi wa barabara.

Alisema meneja wa TARURA katika
jimbo lake anahudumia wilaya tau ambazo
ni Masnispaa ya Mtwara, Halmashauri ya
Mtwara na Halmashauri ya Mji wa Nanyamba.

Alipendekeza kuwa TAMISEMI ipewe kibali
maalum cha kuajiri Wahandisi wa barabara
kwaajili ya kupelekwa wilayani.

Alisema upungufu wa watumishi pia upo
katika sekta ya afya ambapo katika mkoa wa Mtwara kuna upungufu wa 6.088 waliopo ni 2,153 ambao ni upungufu wa asilimia 65.

Katika sekta ya elimu alisema kuna
upungufu wa walimu ambapo aliishauri
TAMISEMI kuhakikisha inatoa kibali cha
walimu 300 kuajiriwa katika Halmashauri ya Nanyamba.

Alisema mapato ya serikali za mitaani
madogo na vyanzo vingi si vya ukakika na
vichache vilivyopo havisimamiwi vizuri.

“Halmashauri nyingi zinategemea ushuru
wa mazao kama chanzo muhimu cha mapato yake. Vyanzo vingi vya uhakika vipo serikali kuu,” alisema Chikota.

Alisema kwa sababu wizara imetenga
zaidi ya Sh. Bilioni 190 kwa ajili ya ununuzi
wa magari ya viongozi basi Mkuu wa Wilaya ya Mtwara anunuliwe gari jipya kwa sababu lililopo halimwezeshi kutimiza majukumu yake vizuri.