CHADEMA yaikubali hotuba yake asema imegusa mioyo yao, Adai hawakusudii kumzengua,
Na Penina Malundo, TimesMajira Online, Dar es Salaam
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimemuandikia barua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, wakiomba kukutana kwa maelezo kuwa hotuba yake ya kwanza aliyoitoa Machi 19, mwaka huu mara baada ya kuapishwa imegusa mioyo ya watu wengi wenye hofu ya Mungu wakiwemo wana-CHADEMA.
Kauli hiyo ilitolewa jijini Dar es Salaam leo na Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe kupitia hotuba yake iliyorushwa moja kwa moja kupitia mitandao ya kijamii.
Mbowe amesema pindi watakapokubaliwa kukutana na Rais Samia, hawakusudii kumzengua wala na wao hawatarajii kuzenguliwa, hasa kwa kuzingatia kwamba hotuba yake hiyo ya Machi 19, mwaka huu imegusa mioyo ya watu wengi wenye hofu ya Mungu, wakiwemo wana-CHADEMA.
Mbowe alitumia fursa hiyo kunukuu baadhi ya maneno aliyoyasema Rais Samia kwenye hotuba yake, amesema;
“Katika kipindi hiki cha maombolezo huu ni wakati wa kuzika tofauti zetu kama Taifa, kufarijiana, kuonesha undugu, sio wakati wa kuangalia mbele kwa mashaka, bali ni wakati wa kutazama mbele kwa kujiamini. Ni wakati wa kufutana machozi na kufajiriana “
Kwa mujibu wa Mbowe kutokana na kuguswa na maneno yake hayo, yeye kwa niaba ya CHADEMA tayari amemwandikia Rais Samia barua ya kuomba kukutana naye.
“Tumeomba rasmi kukutana naye ili tuweze kumueleza kilio chetu, hatutegemei kumzengua, wala hatutegemea kuzenguliwa. Tunataka kumueleza tuliyonayo kwenye mioyo yetu na kumkabidhi mapendekezo ya kina kuhusiana na namna ya kujenga mtengamano wa taifa letu,” amesema Mbowe.
Mbowe amesema kwa sasa wanatambua majukumu ya Kitaifa aliyonayo Rais Samia, lakini wanatambua kuwa atawapa nafasi ya kuwasikiliza.
Ushindani wa kujenga
Aidha, Mbowe amesema wao kama CHADEMA wanamshauri Rais Samia kujiandaa kupata ushindani wenye kujenga sio wenye lengo la kubomoa.
“CHADEMA hatutaki visasi , bali tunataka kushindana kwenye ushindani huru na wa haki,” amesema Rais Magufuli.
Asema TRA wamefungua kaunti zake
Katika hatua nyingine, Mbowe amesema Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imemwandikia barua ya kufunguliwa akaunti zake zote zilizokuwa zimefungwa kwa madai ya kudaiwa kodi ya sh. bilioni mbili.
Amesema wakati wa akikabiliwa na kesi ya uchaguzi, Novemba 23, mwaka jana yeye pamoja na aliyekuwa Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko walifutiwa dhamana baada ya kukiuka masharti ya dhamana..
Amesema akiwa gerezani Novemba 30, mwaka jana TRA walimwandikia barua kumjulisha kuwa mojawapo ya kampuni yake ilikuwa inadaiwa kodi ya sh. Bilioni 2 , jambo alilodai halikuwa la kweli.
Amesema wakati TRA inamwandikia barua hiyo, alikuwa gerezani hivyo, hakuwa na namna ya kujibu TRA, japo alipewa siku 60 kama ana pingamizi.
Mbowe amesema baada ya siku 60, aliandikiwa barua ya pili na TRA, akijulishwa kwamba asipojibu ndani ya siku 30 itaonekana kwamba deni la kodi hiyo ni halali, lakini hakuna namna ya kufanya hivyo kwa sababu alikuwa gerezani..
Kwa mujibu wa Mbowe, alivyotoka gerezani alizungumza na mamlaka zote husika, lakini akaunti zote zilifungwa.
“Juzi nadhani baada ya hotuba ya Rais Samia katika mazingira ya kushangaza TRA wameniandikia barua kwamba wamefungua akaunti zangu, hawakunieleza kuhusu fedha zangu walizozichukua,” amesema Mbowe na kuongeza;
“Hiyo ni moja ya sababu iliyonifanya niondoke nchini nikaamua kwenda nje kufanya biashara ya kimataifa,” amesema Mbowe.
Apata chanjo ya CORONA
Katika hatua nyingine, Mbowe aliweka wazi kuwa tayari amepata chanjo ya Corona katika nchi aliyokuwepo, lakini hakutaja ni nchi gani.
Aliunga mkono uamuzi uliotangazwa hivi karibuni na Rais Samia wa kuunda Kamati itakayomshauri kwenye masuala ya Corona.
“Binafsi naunga mkono mwelekeo uliooneshwa na Rais Samia katika suala zima la ugonjwa wa CORONA. Namuomba Mama Samia aunde haraka Kamati ya CORONA na hata pale ambapo hatuna wataalam wa kutosha, tuweze kupata wataalam kutoka nchi tofauti ili waweze kutushauri namna ya kuweza kukabiliana na jambo hilo,” amesema Mbowe.
Katiba Mpya
Akizungumzia madai ya Katiba mpya, Mbowe amesema hilo; “Hitaji la Katiba mpya halitakiwi kuwa hitaji la Rais au chama chake. Uhitaji wa Katiba mpya hauhitaji kuwa utashi binafsi wa Rais na chama chake kwani mjadala ulishafungwa, hilo ndilo hitaji la Watanzania.”
“Hatupashwi kuwa na mjadala wa kama tunahitaji au hatuhitaji Katiba, mjadala unatakiwa kuwa tunahitaji utaratibu gani kuweza kufikia huko,” amesema na kuongoza kwamba lazima tuwe na Katiba ambayo itaunda taasisi.
More Stories
Kamishna Hifadhi ya Ngorongoro atakiwa kupanua wigo wa Utalii nchini
Wakuu wa Wilaya,Wakurugenzi watakiwa kusimamia programu za chakula shuleni
Mbowe akuna wengi kuhusu maridhiano