Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Benki ya NBC Yajivunia Mafanikio Mapambano Dhidi ya Saratani.
Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imetanganza msimu wa nne wa mbio za NBC Dodoma International Marathon 2023 zinazotarajiwa kufanyika Julai 23 mwaka huu katika uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, huku ikijivunia mafanikio makubwa yaliyotokana na mbio hizo ikiwemo kuweza kukusanya fedha zaidi ya sh millioni 500 ili kusaidia mapambano dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi kwa wanawake nchini yaani “Cervical cancer”.
Hafla ya uzinduzi wa mbio hizo imefanyika mapema hii leo jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa mchezo wa riadha nchini pamoja na wadau wa mbio hizo akiwemo Mwenyekiti wa Chama cha Riadha Tanzania (RT), William Kallaghe, Mkurugenzi wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) Dkt. Crispin Kahesa, wafanyakazi wa benki ya NBC wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki Bw Theobald Sabi pamoja na wadau wa vyombo vya habari.
Akizungumza kwenye hafla hiyo Sabi alisema kupitia uratibu wa mbio hizo katika kipindi cha miaka mitatu sasa, Benki ya NBC imefanikiwa kukusanya zaidi ya Shilingi millioni 500 ambazo zimekabidhiwa kwa taasisi ya Saratani ya Ocean Road ili kufadhili upimaji na matibabu ya saratani hiyo kwa wanawake.
“Ninayo furaha kuwajulisha kuwa ripoti ambayo wenzetu wa Ocean Road wametupatia, inaonyesha kuwa fedha zilizokusanywa kupitia mbio hizi, zimewezesha upimaji wa zaidi ya wanawake 20,473 ambapo kati yao 1,330 waligundulika kuwa na vimelea vya saratani ya shingo ya kizazi na wanaendelea na matibabu na wauguzi 98 wamepata mafunzo ya kusaidia wagonjwa wa saratani. Hili ni jambo kubwa na la kujivunia sana.’’ Alisema Sabi huku akiwapongeza washiriki na wadau wa mbio hizo kwa mafanikio hayo.
Aidha Sabi aliongeza kuwa mbali na mafanikio hayo mbio hizo pia zimefanikiwa kuunga mkono juhudi za serikali katika kukuza utalii wa ndani na kufungua fursa za kiuchumi hususani katika jiji la Dodoma ambapo zimekuwa zikifanyika.
“Mwaka jana zaidi ya wageni elfu 7,000 walifika jijini Dodoma kwa ajili ya mbio hizi ambapo walihitaji chakula, malazi, mavazi, vinywaji na usafiri. Tunaamini wakazi wa Dodoma walinufaika na fursa hizo za kiuchumi na wataendelea kujivunia mbio hizi.’’ Alisema.
Sabi aliwasihi wapenzi na wadau wa mchezo wa Riadha nchini kuanza kujiandaa mapema kwa ajili ya mbio hizo za kimataifa huku lengo likiendelea kuwa ni kuchangia sekta ya afya hususan eneo la mapambano dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi kwa wanawake na maeneo mengine ambayo yatatajwa siku chache zijazo.
Kwa upande wake Dkt Kahesa alisema ‘NBC imekua mdau mkubwa katika kupambana na saratani haswa ya shingo ya kizazi. Takwimu zinaonyesha kati ya kesi elfu arobaini za saratani Tanzania elfu ishirini na sit ani saratani ya shingo ya kizazi.
Matibabu ya saratani nayo ni gharama, kwani mgonjwa hulazimika kutumia kati ya milioni 10 hadi 40 katika matibabu ya saratani.
‘Kwa takwimu hizi zilizotolewa leo ni Dhahiri kwamba NBC Dodoma marathon inasaidia sana katika kuboresha afya na Maisha ya watanzania na kuwaondoloea jukumu kubwa la matibabu kwasababu wanawake wanapopimwa mapema na kugundulika na vimelea hupatiwa matibabu ya awali kuzuia usambaaji wa saratani hii’.
Naye Mwenyeki wa RT, Kallaghe alisema “NBC Dodoma marathon ni kati yam bio zenye viwango vya hali ya juu na vyenye mchango mkubwa katika kukuza mchezo huu wa riadha Tanzania. Tumeshuhudia wenyewe kuwa NBC Dodoma marathon ni kati ya wadau wanaotoa Zawadi kubwa kwa washindi ili kuleta hamasa na mwamko wa mchezo huu ndani nan je ya nchi. Naambiwa mwaka jana peke yake NBC marathon ilivutia Zaidi ya wanariadha wa kulipwa 60 kutoka mataifa mbali mbali”.
Tangu kuanza kwa mbio hizo zinazoingia msimu wa nne mwaka huu zimekuwa zikibeba agenda ya kusaidia mapambano dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi kwa wanawake nchini yaani “Cervical cancer”. Aina hiyo ya saratani ndio inayoongoza kwa kuchangia vifo vingi zaidi vya wanawake nchini Tanzania na katika nchi zinazoendelea.
More Stories
Elon Musk : Bill Gates atafilisika endapo…
CRDB yazindua matawi Majimoto, Ilula kuwahudumia wananchi
Lina PG Tour yafufua gofu Moshi