Na Suleiman Abeid, TimesMajira Online, Kakonko, Kigoma
CHAMA Kikuu cha Ushirika katika wilaya za Mbogwe na Bukombe (MBCU) mkoani Geita kimefanikiwa kupata faida ya zaidi ya shilingi milioni 290 kwa msimu wa mwaka 2021/2022 na hivyo kuweza kuwalipa malipo ya pili wakulima wote waliouza pamba yao kwa chama hicho.Mwenyekiti wa MBCU, Benedictor Bulugu amesema mbali ya kuwalipa wakulima malipo hayo pia chama chake kimeweza kurejesha mkopo wote wa shilingi bilioni tisa walizokopeshwa na Benki ya Maendeleo ya kilimo Raslimali nchini (TIB) na riba yake na kubakiwa na faida ya kutosha.
Bulugu ameyasema hayo wakati wa zoezi la ulipaji malipo ya pili kwa wakulima wa zao la pamba katika Chama cha Msingi cha Ushirika cha Kanyonza Amcos wilayani Kakonko, mkoani Kigoma ambapo amesema malipo hayo yanatokana na asilimia 50 ya faida waliyozalisha katika msimu wa mwaka 2021/2022.
Amesema hatua hiyo ni utekelezaji wa maazimio ya mkutano mkuu wa wanachama wote wa MBCU uliofanyika mwaka jana ambao uliazimia iwapo patapatikana faida baada ya kutoa gharama zote za uzalishaji asilimia 50 ya faida hiyo irejeshwe kwa wanachama.
“Tumegawa malipo ya pili ikiwa ni kutekeleza maagizo ya wanachama ambao walisema baada ya kuanza uzalishaji wa kuchambua pamba kwenye kiwanda chetu na kuuza pamba nyuzi na mbegu faida itakayopatikana asilimia 50 itarudi kwa wakulima na 50 itaendesha shughuli za ofisi,”
“Sasa baada ya kuuza pamba nyuzi na mbegu, tumeitisha mkutano mkuu mwingine na kuwasomea wanachama wetu taarifa ya mapato na matumizi ambapo pia tumefanikiwa kulipa deni lote la mkopo na riba yake kwa asilimia 100 kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB), hivyo sasa tunalipa malipo ya pili kwa wakulima,” anaeleza Bulugu.
Kwa upande mwingine Mwenyekiti huyo ametoa wito kwa wakulima wote wa zao la pamba katika mikoa ya Geita, Shinyanga na Kigoma ambao awali hawakuamini kama MBCU inaweza kuwalipa malipo ya pili sasa wapeleke pamba yao kwa mwaka huu kwenye vyama vya ushirika vya msingi vinavyosimamiwa na ushirika huo.
Kwa upande wake Kaimu Meneja wa MBCU, David Magai amesema mafanikio ambayo yamepatikana na kuwezesha wakulima kulipwa malipo ya pili yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na chama hicho kushiriki moja kwa moja kwenye ununuzi na uchambuaji wa pamba kwa msimu wa mwaka 2021/2022.
“Kwa msimu uliopita tumepata faida ya zaidi ya shilingi milioni 290 ambapo asilimia 50 ndiyo imerejeshwa kwa mkulima ikiwa ni malipo yake pili kama walivyokuwa wameagiza, mtaji wa kuendeshea shughuli zetu tulipata kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo nchini, ambayo ilitupatia mkopo wa shilingi bilioni tisa,” anaeleza Magai.
Baadhi ya wakulima ambao wamepokea malipo ya pili kutokana na pamba waliyouza msimu uliopita wamekipongeza na kukishukuru chama cha MBCU ambapo wamesema suala hilo awali wengi wao waliona lisingewezekana na sasa ni kama ndoto kwao.
Wakulima hao wametoa wito kwa wakulima wengine ambao hawakutaka kukiuzia pamba chama hicho katika msimu uliopita kwamba hivi sasa wabadili mitizamo yao na wapeleke pamba yao kwenye chama hicho kwa vile kimeonesha mafanikio makubwa ndani ya kipindi cha msimu wa mwaka mmoja.
Zabibu Malecela, Scholastica Petro na Leonard Kagola wakazi wa kijiji na kata ya Kanyonza wilayani Kakonko mkoani Kigoma wanasema kwa sasa pamba yao yote wataielekeza kwenye Chama Kikuu cha MBCU kwa vile kimeonesha mwelekeo mzuri kwa wakulima.
“Kwa kweli hiki chama kimefanya jambo ambalo hapa kwetu halijawahi kutokea, leo tumefurahi sana kwa kulipwa malipo ya pili kwa pamba yetu tuliyouza mwaka jana, tunaomba waendelee hivi hivi kila mwaka, huko nyuma hakuna kampuni hata moja ambayo iliweza kufanya jambo hili,”
“Kwa Serikali tunaiomba sasa iendelee kutusaidia kuweza kupata viuatilifu na pembejeo zote muhimu kwa wakati ili tuweze kulipa kwa ufanisi na kupata mazao mengi, tunataka tulime kilimo chenye tija, hawa MBCU wameonesha wanaweza kutupeleka mbali kwenye mafanikio, tunawapongeza kwa hili,” anaeleza Kagola.
Naye diwani wa kata ya Kanyonza, Alfred Elias ameushukuru uongozi wa MBCU kwa kuwalipa wakulima malipo ya pili na kwamba kitendo kilichofanyika hakijawahi kutokea kwa wakulima wa kata yake ambapo amewaomba wakulima kukipa ushirikiano wa karibu chama hicho kwenye msimu wa mwaka huu.
“Ninashukuru sana kwa tukio hili la leo, maana naona wananchi wangu wa kata ya Kanyonza kila mmoja nyuso zao zimetabasamu, hii ni fursa nzuri kwao, niwapongeze viongozi wa Chama chetu cha msingi cha Kanyonza Amcos kwa usimamizi mzuri, maana hapa kila mkulima atapata haki yake,”
“Jambo hili ambalo limefanywa na MBCU halijawahi kutokea huko nyuma makampuni mengi yakiwemo ya watu binafsi hununua pamba na kuondoka zao, hayarejeshi kwa wakulima sehemu ya faida kama ambavyo wenzetu hawa walivyofanya leo, mungu awabariki sana,” anaeleza Alfred.
More Stories
Makalla:Kupanga fujo ni dalili za kushindwa uchaguzi
Tanzania yapanda viwango Utawala wa Sheria Duniani
Rais Samia apeleka neema Tabora