May 15, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mavunde:,Tutafuata ushauri wa Kamati ya Kudumu ya Bunge

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online. Arusha.

WAZIRI wa Madini, Anthony Mavunde, ameihakikishia Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuwa Wizara hiyo itaufanyia kazi ushauri uliotolewa wa kuhakikisha mradi wa jengo la ghorofa nane la kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC), linakidhi mahitaji ya watumiaji kwa kipindi kirefu.

Upanuzi wa miundombinu ya kituo hicho ni mojawapo ya hatua za utekelezaji wa Sera ya Madini ya Mwaka 2009 na mikakati ya muda mfupi na mrefu ya Wizara hiyo ya kuhamasisha shughuli za uongezaji thamani madini zinafanyika nchini ikiwemo kuongeza na kuzalisha wataalamu katika tasnia hiyo, ambao wataweza kufanya shughuli za uongezaji thamani madini kwa ubora wa kimataifa.

Mavunde, ameyabainisha hayo, Machi 13, 2024 wakati wa ziara ya kamati hiyo, ilipotembelea eneo linapotarajiwa kujengwa jengo hilo la TGC lililopo Kata ya Themi-Njiro jijini Arusha.

Lengo likiwa ni upanuzi wa miundombinu ya kituo hicho kilicho chini ya Wizara ya Madini kinachojihusisha na utoaji mafunzo ya uongezaji thamani madini yakihusisha ukataji,ungarishaji na utambuzi wa madini ya vito pamoja na utengenezaji wa bidhaa za usonara kama pete, hereni, mikufu na huduma mbalimbali kama maabara.

Waziri Mavunde amezitaja huduma zitakazokuwa ndani ya jengo hilo ni pamoja ofisi za TGC na za madini kwa Mkoa wa Arusha,viwanda vya uongezaji thamani madini vya wafanyabiashara, sehemu maalumu ya kuendesha minada ya madini, maktaba pamoja na mabweni ya wanafunzi watakaojiunga na kituo hicho.

Huku huduma nyingine ni maabara za madini ya vito na bidhaa za usonara, makumbusho ya madini ya vito na bidhaa za sonara pamoja na maduka ya bidhaa za madini.

Akizungumza katika ziara hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Dkt. David Mathayo ameitaka Wizara kuangalia uwezekano wa kuongeza ukubwa wa eneo ili kukidhi mahitaji ya muda mrefu ya jengo hilo kuweza kupokea na kuhudumia wageni wanaokuja kupata huduma mbalimbali zitakazotolewa ikiwemo maabara za .adini, uendeshaji wa minada ya madini ya vito, mafunzo ya uongezaji thamani madini.