December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mavunde aridhishwa mafanikio ya STAMICO

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

WAZIRI wa Madini, Anthony Mavunde amelipongeza Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kwa hatua kubwa iliyopigwa katika kipindi kifupi kutoka kuwa Shirika tegemezi na kuwa Shirika linalojitegemea huku akilitaka kuendelea kufanya kazi kwa bidii zaidi ili kufikia azma ya kuwepo kwa Shirika hilo.

Ameyasema hayo Septemba jana jijini Dodoma katika kikao kifupi na Menejimenti ya Shirika hilo ambapo alieleza kuwa STAMICO imefanya kazi kubwa sana katika muda mfupi na kuleta ushindani dhidi ya kampuni kubwa zilizokuwa zimezoeleka katika Sekta ya Madini hapa nchini.

Waziri Mavunde amesema kuwa Shirika hilo limeonesha kuwa hakuna jambo linaloshindikana; kujitolea, uadilifu na maono ni chachu iliyopelekea mafanikio katika Shirika hilo.

“lakini nimpongeze Mkurugenzi Mtendaji, Dkt. Venance Mwasse tangu amefika hapa amefanya mapinduzi makubwa lakini bila ninyi asingeweza peke yake, nawapongeza sana na hiki kiwe kichocheo cha kufanya vizuri zaidi” amesema Mhe. Mavunde.

“Lakini kwa upekee sana nimpongeze Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko, Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara, Kheri Mahimbali kwa usimamizi wao thabiti bila wao yawezekana msingefika hapa na nyinyi wenyewe mmekiri kuwa Wizara imewasaidia sana kufanya mapinduzi haya makubwa,” ameongeza Mavunde.

Aidha, ameitaka Shirika hilo kufikiria kufanya kazi zaidi hadi nje ya mipaka ili kujiimarisha na kujitangaza zaidi kwa kuleta ushindani katika tasnia ikiwemo ya Uchorongaji.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya STAMICO, Meja Jenerali Mstaafu Michael Isamuhyo amempongeza Mhe.Mavunde kwa kuteuliwa kwake kuwa Waziri wa Madini na kumuahidi kuwa Shirika litafanyia kazi maelekezo yake ili kufikia lengo.

Akizungumzia Mipango ya Shirika hilo, Meneja Rasilimali Watu Deusdedith Magala ameeeleza kuwa Shirika limepanga kuondokana kabisa na utegemezi wa mishahara kutoka serikalini kuanzia mwaka wa fedha 2024/2025; kuongeza gawio lake serikalini mwaka 2024/2025; kuzalisha kwa wingi Mkaa mbadala Rafiki Briquettes uonaotokana na Makaa ya Mawe; kuimarisha uchimbaji wa Makaa ya Mawe.

Ametaja mipango mingine kuwa ni kuongeza uwekezaji kwenye tasnia ya Uchorongaji; kuendeleza leseni za Shirika hilo na kuzitangaza kwa lengo la kupata wawekezaji wa Madini ya Kimkakati ya Lithium, Graphite, REE na Cooper; mpango wa utafiti wa leseni za Shirika hilo; kuimarisha usimamizi wa kamputanzu ya STAMIGOLD na kampuni za ubia za kiwanda cha kusafisha Dhahabu Mwanza na miradi ya kuchimba Dhahabu wa Buckreef na Buhemba.