December 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mashindano ya Safari Lager Cup yazinduliwa rasmi Dar

Na Hamisi Miraji, Timesmajira Online

Bia ya Safari Lager, imezindua rasmi mashindano makubwa ya mpira wa miguu yajulikanayo kama Safari Cup, yenye lengo la kuibua vipaji katika mikoa mbalimbali hapa nchini.

Mashindano hayo yalizinduliwa jana, katika Viwanja vya Leaders Club Jijini Dar es Salaam, ambapo wadau mbalimbali wa soka walihudhuria hafla hiyo ya Uzinduzi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Meneja wa Chapa ya Safari Lager, Pamela Kikuli alisema bia ya Safari, ambayo ni ya mabingwa imeamua kuja na kampeni hiyo iii kuibua vipaji vipya vya mpira wa miguu kwani wanaamini kuna vipaji vingi nchini ambavyo havijaibuliwa.

“Kama mnavyojua Tanzania ina vipaji vingi sana lakini vinahitaji sapoti ya hali ya juu, Bia ya Safari imeamua kuja na kampeni hii ambayo itakuwa mwarobaini kwa vijana wenye vipaji vya soka kuanza kutambulika,” alisema Kikuli.

Kikuli alisema mashindano hayo yatafanyika katika mikoa minne huku akitaja na tarehe ya kufanyika kwake.

.Meneja wa Chapa ya Safari Lager, Pamela Kikuli akipiga mpira kuashiria ufunguzi wa mashindano makubwa ya mpira wa miguu yajulikanayo kama Safari Lager Cup, mbele ya makocha Jamhuri Kihwelo (katikati) na Sekilojo Chambua (kulia), uzinduzi huo ulifanyika leo kwenye Viwanja vya Leaders Club Jijini Dar es Salaam.

Mashindano hayo yataanza mkoani Mbeya (FFU tarehe 7 Oktoba, Arusha (Uwanja wa Ngarenaro) tarehe 21 Oktob, Mwanza (Uwanja wa Nyamagana) tarehe 4 Novemba. Dar es Salaam yatafanyika kwenye Viwanja vya Kinesi tarehe 18 Novemba.

Hata hivyo alisema, walengwa wakuu ni vijana wenye umri wa Miaka 18 na zaidi ambao wataitwa kwenye usaili ili washiriki katika mashindano ya mtoano yatakayofanyika na kuchagua vijana ambao watawakilisha timu ya kila mkoa kati ya mikoa minne iliyochaguliwa.

“Baada ya hapo timu zile za mkoa zitatumika kuchagua vijana ambao wataunda timu moja kubwa ya wachezaji 22 ambao watacheza mechi ya kirafiki na timu mojawapo ya Ligi Kuu ambayo itatangazwa hapo baadaye,” alisema.

Katika hatua nyingine, Kikuli alisema timu hiyo ya Safari Champions itakayochaguliwa kucheza mechi kirafiki na timu mojawapo ya Ligi Kuu, itajinyakulia kitita cha Tsh,milioni 44 na itajulikana kama Timu ya Mabingwa ya Safari Cup yaani Safari Cup Champions.

Mbali na hivyo pia, Kocha Jamhuri Kihwelo na Sekilojo Chambua watashiriki katika kuibua vipaji kwa kuchagua vijana watakaounda timu hizi za mikoa na hatimaye timu ya Safari Lager Cup Champions.

“Tunaipongeza sana bia ya Safari kwa kuona umuhimu huu wa kuibua vipaji miongoni mwa vijana kwani kuna vipaji vingi mno mikoani lakini hakuna wa kuviibua na kuviendeleza,” alisema Kocha Kihwelu. Naye Kocha Chambua alisema,

“Ni heshima kubwa kwetu kupata fursa hii ya kutafuta vipaji mikoani na kuunda timu hii ya Safari Lager Cup Champions. Ni matumaini yetu kuwa vijana watajitokeza kwa wingi kwenye usaili ili washiriki katika mashindano haya.”

Bia ya Safari Lager iliwahi kudhamini mashindano ya Taifa Cup ambayo yalishirikisha mikoa yote ya Tanzania kwa lengo la kuibua vipaji.

Meneja wa Chapa ya Safari Lager, Pamela Kikuli (katikati), akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani), katika uzinduzi wa mashindano ya Safari Lager Cup, uliofanyika leo kwenye Viwanja vya Leaders Club Jijini Dar es Salaam. Wa kwanza kushoto kocha Jamhuri Kihwelo wa pili kutoka kulia kocha Sekilojo Chambua.