Na Allan Kitwe, TimesMajira Online, Morogoro
MASHINDANO ya kumsaka bingwa wa mchezo wa Riadha nchini yameanza
kutimua vumbi katika uwanja wa Jamhuri Mkoani Morogoro.
Mwenyekiti wa Mashindano hayo ambaye pia ni Mjumbe wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) Alfred Shahanga amesema jumla ya Mikoa 16 kutoka Bara na Visiwani imejitokeza kushiriki mashindano hayo.
Ametaja Mikoa hiyo kuwa ni Tabora, Morogoro, Dodoma, Dar, Shinyanga, Singida, Kilimanjaro, Tanga, Kagera, Kigoma, Mbeya na Njombe kutoka Tanzania Bara.
Mingine ni Kaskazini Unguja, Kusini Unguja, Kaskazini Pemba, Kusini Pemba na Mjini Magharibi kutoka Zanzibar.
Ametaja Mikoa ambayo haijashiriki mashindano hayo kuwa ni pamoja na Arusha, Manyara, Mwanza, Ruvuma, Lindi, Mtwara na mingineyo.
Rais wa Shirikisho hilo Silas Lucas amesema kuwa mashindano hayo ni muhimu sana kwa kuwa yatasaidia kuinua na kukuza vipaji vya wachezaji wa mchezo huo.
Akizungumzia Mikoa ambayo viongozi hawakuleta timu katika mashindano hayo alisikitishwa na kubainisha kuwa hawafai kuwa viongozi wa riadha katika mikoa hiyo kwa kuwa hawawatendei haki wachezaji.
“Hawa Viongozi hawafai na hawawatendei haki wachezaji, tutawashughulikia,” alibainisha.
Akifungua mashindano hayo kwa niaba ya Katibu wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT), Afisa Michezo wa Baraza hilo Charles Maguza amepongeza Mkoa wa Morogoro kwa kukubali kuandaa mashindano hayo na Mikoa yote iliyoleta timu.
Amesisitiza kuwa mashindano hayo ni muhimu sana kwa kuwa yanachochea kuinua na kukuza vipaji vya mchezo huo.
Aidha amesema kupitia mashindano hayo wachezaji wanafahamiana, kuvadilishana uzoefu na pia wanajipima viwango vyao ili kujua kama wanaweza kushiriki mashindano makubwa zaidi.
Kiongozi huyo ameagiza Shirikisho la Riadha kukutana na Viongozi wote ambao hawakuleta timu katika mashindano hayo ya Taifa ili kujua tatizo ni nini na kulitafutia ufumbuzi.
Katika kuendelea mchezo huo ametoa wito kwa Makocha kuandaa wachezaji vizuri ili wakimbie kwa muda mzuri zaidi.
Aidha amewataka kujiendeleza zaidi ili kujenga wachezaji katika kiwango bora zaidi..
Mashindano hayo yaliyoanza Jana yanatarajiwa kuhitimisha leo (jumamosi) ambapo watapatikana washindi wa michezo yote akiwemo bingwa wa jumla wa Riadha hapa nchini.
More Stories
15 wajinoa Juventus,akiwemo mtoto wa Mwenyekiti wa CCM Mbeya
Za Kwetu Fashion Show, yawapaisha wanamitindo nchini
TCAA yaadhimisha siku ya usafiri wa anga Duniani kwa kushiriki mbio za Marathon UDSM