June 1, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Masaburi Naibu Meya Ilala

Na Heri shaban, TimesMajira Online

MADIWANI wa Halmashauri ya jiji la Dar es Salam wamemchagua Naibu Meya wa Halmashauri ya jiji hilo OJAMBI MASABURI, aliyeshinda kwa kishindo kwa kupata kura zote 45 za wapiga kura katika baraza hilo la jiji.

Naibu Meya Masaburi alichaguliwa katika baraza la Madiwani ukumbi wa mikutano Arnatoglou wilayani Ilala leo.

Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo Msimamizi wa uchaguzi huo Katibu Tawala wa wilaya ya Ilala Charangwa Selemani, alisema kwa mujibu wa Serikali za mitaa kila baada mwaka mmoja uchaguzi wa Naibu Meya katika halmashauri za Manispaa unafanyika.

“Chama cha Mapinduzi CCM wilaya ya Ilala kimeleta jina moja la mgombea wa nafasi ya Naibu Meya Ojambi Masaburi anagombea nafasi hiyo awamu ya pili mfululizo hivyo wapiga kura wapige kura mpige kura ya ndio au hapana “alisema Charangwa.

Katibu Charangwa Selemani alisema katika baraza hilo la jiji la Dar es Salaam idadi ya Wajumbe wanatakiwa wawe 54 lakini katika baraza hilo la kumchagua Naibu Meya wa Halmashauri ya jiji na kamati zake wapo madiwani 45 ambapo wote walipiga kura ya ndiyo kumchagua Ojambi Masaburi.

Akizungumza katika mkutano huo wa Baraza la Madiwani Naibu Meya Ojambi Masaburi aliwapongeza Wenyeviti Kamati zote waliopita kwakishindo katika kinyanganyiro hicho ambapo Kamati ya Uchumi na Huduma za Jamii alichaguliwa Saady Kimji Diwani wa kata ya Ilala, aliyepita kwa kura 10 na Kamati ya Mipango Miji na Mazingira alichaguliwa Nyasika Getama, aliyeshinda kwa kishindo kwa kupata kura zote 16 za wajumbe ambapo anakuwa Mwenyekiti wa Kamati za huduma ya Mipango Miji na mazingira kwa kipindi cha awamu ya pili mfululizo.

MASABURI alisema anawashukuru sana madiwani kwa kura nyingi ambapo aliwaaidi madiwani wa Halmashauri hiyo kuwapa ushirikiano na kutetea maslahi ya madiwani wote.

Naibu Ojambi Masaburi alisema atafanya nao kazi madiwani wote kwa ushirikiano bila kuweka matabaka katika kufanya kazi za chama na Serikali na kuakikisha Halmashauri ya jiji inasonga mbele katika makusanyo ya Mapato na miradi ya Serikali.

Alipowapongeza viongozi wa chama cha Mapinduzi CCM wilaya ya Ilala Katibu na Mwenyekiti wake pamoja na mkuu wa Wilaya ya Ilala ambapo Masaburi alisema yeye ni Mtumishi wa Madiwani wote hivyo atawapa ushirikiano mkubwa.

Mwenyekiti wa Kamati ya Uchumi na Huduma za Jamii Halmashauri hiyo Saady Kimji Diwani wa kata ya Ilala, alisema anawashukuru kwa umoja wao anashirikiana nao bega kwa bega ili kuakikisha wanamsaidia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan, Halmashauri hiyo iweze kusonga mbele katika kusimamia miradi mbali mbali ya maendeleo ikiwemo sekta ya afya.

Mwenyekiti wa Kamati ya Mipango Miji na mazingira Nyasika Getama Diwani wa kata ya Kivule ambaye ameshinda nafasi hiyo kwa awamu ya pili aliibuka kidedea kwa kupata kura zote 16 alisema anashirikiana na madiwani wenzake pamoja katika idara hiyo kuakikisha wanafanya kazi kwa weledi mkubwa .

Nyasika Getama aliwataka madiwani wa Ilala waendelee kumuamini
katika utekelezaji wa majukumu yao katika halmashauri hiyo.

Katika baraza hilo la Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam Mwenyekiti wa kikao hicho Meya Omary Kumbilamoto aliwapongeza Wenyeviti Kamati zote waliochaguliwa na kuwataka kufanya kazi pamoja kuakikisha Halmashauri hiyo inafikia malengo yake katika sekta zote .

Meya Kumbilamoto aliwataka madiwani wake kuakikisha wanatoa ushirikiano kwa Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Jomary Mrisho Satury katika ukunyaji Mapato ya Serikali na kusimamia miradi ya maendeleo ndani ya Halmashauri hiyo.