Na Mwandishi Wetu,TimesMajira Online, Makambako
KATIKA kuunga mkono juhudi za Serikali na kupanua wigo wa huduma za afya ya uzazi na afya kwa ujumla Marie Stopes Tanzania imefungua Kituo cha Afya (Polyclinic) Makambako ambacho kitatoa huduma mbalimbali ikiwemo huduma za afya ya uzazi,kliniki kwa wajawazito.
Pia huduma za uzazi wa mpango,uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi,huduma za kibingwa kwa wanawake na watoto,huduma za afya kwa ujumla na vipimo mbalimbali kama ultrasound,vipimo vya homa ya ini,chanjo kwa watoto na chanjo ya homa ya ini.
Kituo hiki cha afya ambacho kimejengwa kwa ufadhili wa Shirika la Misaada la Canada kupitia Ubalozi wa Canada nchini,kimelenga kuhudumia wakazi wa Mji wa Makambako na maeneo ya jirani ambao kwa sasa una idadi ya wakazi wanaokadiriwa kufikia 116,398 ambapo asilimia 52 ni wanawake.
Akizungumza katika uzinduzi wa kituo hiki,Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Marie Stopes Tanzania,Bw.Vadacanthara Chandrashekara amesema; “Ujenzi wa kituo hiki ni mwendelezo wa jitihada za Shirika la Marie Stopes kusogeza huduma kwa wananchi hasa wale wenye mahitaji ya huduma za afya ya uzazi katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania ambapo tumekuwepo kwa miaka 32 sasa.
“Kituo cha Makambako kitajikita katika msingi wa biashara ya kijamii inayolenga kutatua changamoto zinazoikumba jamii kwa kuhakikisha huduma bora na zinazofikiwa kwa urahisi na viwango.” amesema mkurugenzi mkuu huyo.
Akitoa maelezo ya uwekezaji uliofanywa na Serikali ya Canada kupitia Ubalozi wa Canada nchini Tanzania,Mkuu wa Maendeleo kutoka Ubalozi wa Canada Bi.Helen Fytche amesema;“Serikali ya Canada inathamini sekta ya afya na uendelezaji wa jitihada za kukuza usawa wa kijinsia na hivyo tumewekeza Dola za Canada 300,903.89 sawa na shilingi za kitanzania 543,835,348.29.
“Tuna imani kwamba tutaweza kuwafikia wanawake,wasichana na wanaume wa Makambako kwa ajili ya elimu na huduma za afya ya uzazi na afya kwa ujumla,” amesema.
Katika kuhakikisha ubora na ufanisi wa huduma za kituo hiki,watoa huduma wamepatiwa mafunzo maalumu ili kuweka kipaumbele na kuzingatia mahitaji ya usawa wa kijinsia na pia kutoa huduma rafiki za afya ya uzazi kwa vijana hasa kwa kuzingatia mahitaji ya kipekee waliyonayo na miongozo iliyotolewa na serikali.
Kituo hiki kina chumba maalaumu kwa ajili ya kuwahudumia vijana na hivyo ni
fursa kwa vijana kupata huduma za afya ya uzazi ambazo ni rafiki,zenye usiri na staha kwa vijana balehe.
More Stories
Watakiwa kushirikiana kutikomeza matatizo ya lishe
CCBRT yazidi kuunga mkono juhudi za Rais Samia
Madaktari bingwa wa Samia watua Rukwa