April 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa.

Maonesho ya Sabasaba 2020 kuanza Julai Mosi

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

SERIKALI imesema inaendelea na maandalizi ya Maonesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa yanayotarajiwa kuanza Julai Mosi hadi Julai 13, mwaka huu.

Hayo yamebainishwa kupitia taarifa iliyotolewa na Wizara ya Viwanda na Biashara mapema leo ambapo maonesho hayo ambayo yamekuwa yakifanyika nchini kwa miaka 43 tokea kuanzishwa yanatarajia kufanyika mwaka huu jijini Dar es Salaaam kwa mara nyingine ambapo yatakuwa ni maonesho ya 44.

Maonesho hayo ambayo hufanyika katika Uwanja wa Maonesho wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, katika barabara ya Kilwa, hutoa fursa ya kutafuta masoko ya mazao na bidhaa za kilimo, viwanda na huduma nchini.

Taarifa hiyo imebainisha kuwa, mwaka huu kauli mbiu ya Maonesho ya 44 ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF) ni “Uchumi wa Viwanda kwa Ajira na Biashara Endelevu” inayolenga kutambua mchango wa Sekta ya Kilimo na Viwanda katika kuzalisha ajira na kujenga biashara endelevu.

Aidha, taarifa hiyo imefafanua kuwa, kanuni za afya kwa lengo la kuhakikisha kuwa Uwanja wa Maonesho unakuwa salama kwa waoneshaji na watembeleaji zinazingatiwa kwa kuchukua hatua zote zinazostahili za kujikinga na maambukizi ya COVID-19.

“Ili kuendana na hali halisi na kufikia wigo mkubwa zaidi wa wazalishaji na wanunuzi. Mikutano yote ya ana kwa ana ya wafanyabiashara (B2B) itaandaliwa na kuratibiwa kwa njia ya mtandao,”imeeleza taarifa hiyo iliyo sainiwa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa.

Ameeleza, lengo la mikutano hiyo ni kuimarisha upatikanaji wa masoko endelevu ya bidhaa na huduma. Katika kurahisisha utembeleaji wa maonesho, watembeleaji watapata fursa ya kununua tiketi kupitia simu za mikononi.

“Watembeleaji kutoka ndani na nje ya nchi, watapata fursa ya kuetembelea maonesho kupitia mtandao (live streaming and virtual exhibition). Kutakuwa pia na banda maalumu litakalotangaza bidhaa za kilimo yakiwemo mazao ya kimkakati,”imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Aidha, Serikali imetoa wito kwa wadau wa viwanda nchini, wakulima, taasisi za umma, halmashauri za wilaya, taasisi binafsi kushiriki katika maonesho hayo ili kuongeza wigo wa masoko ya bidhaa za kilimo, viwanda, uvuvi na madini zinazozalishwa nchini.