November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mamia ya wakazi Dar wajitokeza kupima macho bure

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online, Dar

SERIKALI imezipongeza Hospitali za CCBRT na Polisi Kilwa Road kwa kushirikiana kutoa huduma bure ya upimaji wa macho kwa wakazi wa Jiji la Dar es salaam katika kuadhimisha siku ya Macho Duniani.

Akizungumza kwenye maadhimisha siku hiyo muhimu, iliyofanyika kwenye eneo la Hospitali ya Polisi Kilwa Road katika Manispaa ya Temeke leo, Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Jokate Mwegelo katika hotuba yake iliyosomwa na Katibu Tarafa wa Chang’ombe, Sadath Mtware mbali ya kutambua mchango mkubwa CCBRT katika upimaji na utoaji ushauri juu ya magonjwa mbalimbali ya macho, amezitaka taasisi hizo mbili kuwa na ushirikiano endelevu kwa manufaa jamii nzima ya watanzania.

“Kabla sijaendelea na hotuba yangu napenda kuchukua fursa hii kuzipongeza hospitali hizi mbili kushirikiana kutoa huduma hii kwa Watanzania hasa wakazi wa wilaya ya Temeke, hili ni jambo la msingi sana na niseme mmetekeleza kwa vitendo, maelekezo yaliyotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan,”amesema Jokate katika hotuba yake.

Jokate amezitaka taasisi nyingine katika wilaya yake ya Temeke kuangalia uwezekano wa kuunganisha nguvu na wadau mbalimbali ili kupanua wigo wa utoaji wa huduma kwa wananchi wilayani na sehemu nyingine nchini, ambako uhitaji wa huduma hiyo ni mkubwa,

“Nimefurahishwa na kauli mbiu ya mwaka huu inayosema ‘Yapende macho yako, Nenda kapime sasa, kila mtu anahusika’ kwani inalenga kutuonesha sisi kama jamii kutambua umuhimu wa afya na ubora wa macho,” alisema na kuongeza kuwa kila mmoja na hasa watu wasiokuwa na tabia ya kupima afya ya macho yao kujenga tabia ya kupima.

Amesema CCBRT imetoa mchango mkubwa katika kutekeleza Mpango Mkakati wa Taifa wa afya ya macho 2018- 2022, ambao unalenga kuwa na jamii yenye afya bora ya macho ambayo pia itawezesha maendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

Daktari wa Macho, Dkt. Joseph Sunguro kutoka Hospitali ya CCBRT akimpima macho Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Temeke ambaye pia ni Katibu Tarafa wa Chang’ombe, Sadath Mtware aliyemwakilisha, Jokate Mwegelo akipimwa macho kwenye Hospitali ya Polisi Kilwa Road Jijini Dar es Salaam leo ikiwa ni siku ya kwanza kati ya siku tatu ya kuadhimisha Siku ya Macho Duniani itakayofanyika Alhamis wiki hii. Wanaoshuhudia kuanzia kushoto ni Inspekta wa Polisi, Stephen Kisanga, Afisa Mtendaji Mkuu wa CCBRT, Brenda Msangi na Mratibu wa Macho Wilaya ya Temeke, Daniel Ringo.

“Nafahamu vizuri kuwa CCBRT mbali ya kuwa hospitali bobezi ya macho wanatibu pia magonjwa mengi tofauti na macho,” alisema na kuhamasisha wana Temeke kujitokeza kwa wingi kupima afya ya macho.

Awali akimkaribisha, Jokate, Afisa Mtendaji Mkuu wa CCBRT, Brenda Msangi alisema taasisi yake na hospitali ya Polisi Kilwa Road zina ubia wa kufanya kazi pamoja katika kutoa huduma ya macho kwa Watanzania na kwamba katika kipindi cha mwaka mmoja pekee wagonjwa zaidi ya 300 wameshapata huduma ya afya ya macho.

“Kama mnavyofahamu CCBRT ni mdau mkubwa wa afya ya macho hapa nchini kwa mwaka Hospitali yetu huona wagonjwa wa macho takribani 64,000, hivyo napenda kutoa wito kwa Watanzania wenzangu hasa wakazi wa Temeke na maeneo ya jirani kuchangamkia fursa ya huduma za macho zinazotolewa kwa ushirikiano baina ya hospitali zetu hizi mbili ili kwa pamoja tuweze kuzuia au kupunguza upofu unaozuilika miongoni mwetu,” amesema.

Kwa mujibu wa Brenda, CCBRT na Menejimenti ya Kilwa Road walikubaliana kuanza maadhimisho haya mapema kwa kuendesha zoezi la siku tatu la utoaji wa huduma za macho kwa wananchi wa Wilaya ya Temeke na maeneo ya jirani kwani siku rasmi itaadhimishwa tarehe 14 Oktoba 2021.

Alisema mbali ya ushirika na hospitali ya Polisi Kilwa Road, CCBRT inafanya kazi na taasisi zingine mbalimbali hapa nchini ikiwemo serikali na mfano mzuri ni ubia kati ya serikali yetu na hospitali ya CCBRT kwenye mradi wa kuwajengea uwezo watumishi wa afya ya uzazi katika vituo na hospitali 23 za serikali mkoani Dar es Salaam.

“Mradi huo ulianza mwaka 2010 na umetekelezwa kwa mafaniko makubwa ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo kwa mamia ya watumishi, kuboresha miundo mbinu ya afya ya uzazi, kuimarisha mifumo ya rufaa pamoja na utunzaji wa takwimu na kumbukumbu mbalimbali za afya ya uzazi katika hospitali na vituo vya afya vya serikali mikoani,”alisema Brenda.

Mapema, Mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Hospitali ya Polisi Kilwa Road, Kaminshna Msaidizi wa Polisi (ACP), Mabula Kawala mbali ya kuishukuru CCBRT kwa ushirikiano wa kutoa huduma ya macho amesema kuna maeneo mengine ambayo wataomba ushirikiano na taasisi hiyo hasa eneo la kupunguza vifo vya mama na mtoto.

Afisa Mtendaji Mkuu wa CCBRT, Brenda Msangi (kushoto)akisitiza jambo wakati ya siku ya kwanza ya siku tatu ya kuadhimisha Siku ya Macho Duniani itakayofanyika Alhamis wiki hii. Katikat ni Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Temeke ambaye pia ni Katibu Tarafa wa Chang’ombe, Sadath Mtware aliyemwakilisha, Jokate Mwegelo. Kulia ni Mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Hospitali ya Polisi Kilwa Road,Kaminshna Msaidizi wa Polisi (ACP), Mabula Kawala.

“Ushirkiano wetu na CCBRT umekuwa na mafanikio makubwa sana kwani tumeweza kuwafikia wadau wengi kwenye suala la afya ya macho,” amesema ACP Kawala na kutoa wito kwa wakazi Dar es Salaam kuzitumia siku tatu ushirika kwenda kupima macho.

ACP Kawala amesema Jeshi la Polisi limeshapeka serikalini ombi la kuipandisha hadhi hospitali hiyo kuwa Hospitali ya Rufaa kutokana na umuhimu wake sambamba na kupanuka kwa huduma zake.

Siku ya Afya ya Macho Duniani huadhimishwa duniani kote Alhamisi ya pili ya mwezi Oktoba ya kila mwaka kwa lengo la kuhamasisha jitihada za kutokomeza upofu unaozuilika duniani.CCBRT imeweka kambi rasmi kuanzia jana mpaka Oktoba 14 (Alhamisi) kwaajili ya huduma ya macho.