Ni katika kumpata mgombea urais na kumnadi. Mafisadi wazidi kunyoshewa kidole. Mbinu za ushindi Pemba zaanikwa
Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Dar es Salaam
MFANYABIASHARA maarufu wa Zanzibar na aliyekuwa Mwakilishi wa Jimbo la Uzini Zanzibar kwa tiketi ya CCM, Mohammed Raza, ametaja mambo ambayo yataivusha salama Zanzibar kwenye kinyang’anyiro cha urais.
Mambo hayo ni kuanzia kwenye mchakato wa kumpata mgombea urais atakayepeperusha bendera ya CCM upande wa Zanzibar, nini cha kufanyika baada ya mgombea huyo kupatikana na namna ya kupata kura za ushindi visiwani Pemba.
Raza ambaye ni mwanasiasa mkongwe alitaja mambo hayo wakati wa mahojiano maalum na mtandao wa TimesMajira Online yaliyofanyika jijini Dar es Salaam leo.
Raza amemhakikishia Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais John Magufuli kwamba hadi sasa Zanzibar ni shwari na hakuna mpasuko wowote, licha ya kujitokeza wagombea 32 wanaowania nafasi hiyo.
Amesema kati ya wagombea hao 32 atakayepitishwa kuwania nafasi hiyo ni mmoja na kwamba huyo ndiye atakuwa mgombea wa CCM.
“Yule atakayesema haiwezekani maana yake huyo atakuwa anashindana naMungu, kama hawezi kukubali basi aondoke CCM asituletee fujo, CCMhakuna umaarufu wa mtu, bali chama ndicho maarufu, kama hakuridhika aende akatafute nafasi hiyo vyama vingine,” amesema Raza.
Amesema kazi iliyofanywa na Serikali ya Rais Magufuli na Dkt. Ali Mohamed Shein ni kubwa, hivyo mgombea yeyote atakayebahatika kuteuliwa na CCM, ndiye huyo atakuwa wa wao wote.
Alishauri baada ya kupatikana mgombea huyo iundwe kamati ndogo ya ushindi wa Zanzibar. “Hiyo ndiyo itakuwa Kamati itakayomvusha mgombea Rais wa Zanzibar na wakereketwa wa CCM,” amesema Raza.
Namna ya kupata kura Pemba
Akizungumza sababu ambazo zimekuwa zikichangia CCM kutopata kura nyingi Pemba, Raza amesema ni pamoja wana-CCM Pemba kutoaminiwa.
“Nataka nimwambie Rais Magufuli, Zanzibar ni lazima tuwaamini Wapemba ambao ni wana CCM, tatizo letu Rais akishateuliwa wanatoka watu Unguja wanaoonekana kama mafisadi na kwenda kuwanadi wagombea Pemba, wakati viongozi wa CCM Pemba wapo, lakini wanaonekana kama hawafai matokeo yake tunawavunja moyo,” amesema Raza na kuongeza;
“Suala la mgombea urais tuwaachie viongozi wa CCM wa Pemba, vifaa vyote vya kufanyia kazi wapewe wao. Haiwezekani mtu anakaa Unguja hajui siasa, lakini baada ya miaka 10 anavaa kofia yake anasema yeye ni mkereketwa wa CCM wakati hata kura moja Pemba hana.”
Kwa mujibu wa Raza, bila kufanya hivyo kwa Pemba endapo majimbo yote yakichukuliwa viongozi wa CCM Pemba watasema; “Ninyi ndiyo mlipeleka watu huko.
Watahoji mbona hao watu hawajawahi kuwaona kwa kipindi chote cha miaka 10 au mitano? Tuwaachie viongozi wa Pemba, sio unatoka Ugunja unaenda Pemba wakati hata kura moja hauna. Kwa kweli hii inawavunja moyo watu wa Pemba.
Alimshauri Rais Magufuli kuhakikisha Kamati ndogo anayopendekeza kuundwa iwe na mvuto na watu wenye busara na hekima . Amesema ni vizuri kuhakikisha kwenye Kamati hiyo mafisadi hawaingii na kutohusika kwa namna yoyote kwenye misafara ya mgombea urais wa CCM Zanzibar.
Alifafanua kwamba wengine wanapenda kujipenyeza kwenye ndege ya mgombea, kwa hiyo ni muhimu kuhakikisha mgombea wa CCM kila anapoenda, apelekwe na vyombo vya ulinzi.
Baada ya Rais kupatikana
Pia Raza, alishauri baada ya Rais wa CCM kupatikana, Rais Magufuli aitazame Zanzibar kwa macho matatu, isije ikawa wanachaguliwa kwenye Serikali watu kwa misingi ya mtu fulani nilisoma naye au kucheza naye.
“Isije ikawa huyo nilisoma naye, huyu ni ndugu yangu, hiyo haiwezi kukubalika,” amesema na kuongeza; “Nchi hii inatakiwa kuwa na viongozi wenye busara.’
Raza amesema ni muhimu wana CCM wakaelewa kuwa usalama wa Zanzibar ni wao wenyewe na anamhakikishia Rais Magufuli kwamba watahakikisha wanamnadi mgombea wa Urais wa CCM kwa mshikamano mkubwa.
“Niombe tu viongozi tushikamane na viongozi wa Zanzibar tuhakikishe tunafungua ukurasa mpya na alama hiyo itawekwa na Rais Magufuli,” amesema Raza.
Amesema Zanzibar wana mbio za vijiti vya pokezani, hivyo ni lazima wawe wavumilivu na wasije wakarejeshewa wagombea ubunge au uwakilishi ambao watasababisha kupungua kura za Rais.
Amesema umuhimu mkubwa kwa sasa Zanzibar upo kwenye kura za Rais na kwamba katika mihula yote miliwi ya Karume (Rais Mstaafu Amani Abeid Karume) na Shein (Ali Mohamed Shein) walikuwa wanapishana kwa sentimita na vyama vya upinzani na kwamba awamu ya pili aliyoshinda Rais Dkt. Shein kwani wale wengine (CUF) hawakuingia kwenye uchaguzi.
Amesisitiza kwamba uchaguzi wa Zanzibar washindi wanapishana kwa pointi.
Ni nini kifanyike Dodoma
Raza ametoa wito kwa CCM kuhakikisha inakuwa makini wakati wa kupitisha mgombea urais wa Zanzibar. “Kwa hiyo nataka nikiambie chama changu, huko Dodoma tuwe waangalifu na Rais Magufuli, Bashiru (Ally) na Mangula (Philip) kuzingatia mambo yote ya muhimu, kwani Dunia nzima itakuwa Zanzibar,” amesema
Amesema Rais Magufuli ameshapita, kwani wote akina Tundu Lissu, Mbowe (Freeman) Zitto Kabwe waliyokuwa wakilalamikia bungeni ilikuwa ni ufisadi ambao Rais Magufuli ameishaushughulikia.
“Kwa hiyo huku Bara hakuna tabu kwa sababu vyama vya upinzani kelele zao bungeni zilikuwa ni hoja ya ufisadi na tayari tumeuondosha,” amesema Raza. Bara tayari Magufuli ameweka heshima.”
Hata hivyo Raza amesema hawezi kudharau wapinzani, japo kilio chao kimeishafanyiwa kazi na CCM. Aliwataka Wazanzibar na Watanzania wasiwe na hofu na Serikali ya Rais Magufuli kwani kazi kubwa imefanyika chini ya uongozi wake
Wabunge/ wawakilishi waliokimbia
Akizungumzia wabunge na wawakilishi waliokimbia, Raza amesema; “Tunataka wabunge na wawakilishi katika kipindi hiki wanaoweza kukisaidia Chama, wale waliokimbia majimbo yao wasipewe nafasi tena, kwani kilichooza leo, kesho kitanuka.
Ametoa wito kwa Mwenyekiti wa CCM, Rais Magufuli kuhakikishawanachagua wabunge na wawakilishi wenye uwezo na uchungu na chama, kwani hatua hiyo italeta faida kubwa kwa Chama.
Alijitolea mfano yeye mwenyewe akisema kwamba Naibu Katibu Mkuu CCM Zanzibar amesoma naye darasa moja, kwa hiyo hawezi kusema ampitishe Raza kwa sababu amesoma naye.
“Tukianza kupitisha wagombea kwa kusema huyo nimesoma naye…huyo baba yake nimecheza naye tutakiumiza Chama, hasa kwa Zanzibar,” amesema Raza na kuongeza; “Tunapoenda kushinda ni lazima tutafute viongozi wanaokubalika.”
Ruzuku ya majimbo
Jambo jingine ambalo alizungumzia Raza kuhusu wabunge wa Bara ni kutaka waongezewe fedha za jimbo mara mbili.
Amesema mbunge wa Zanzibar na mwakilishi wa Zanzibar wanapewa fedha sawa na wabunge wa Bara.
“Sasa ukitazama majimbo ya Bara na Zanzibar ni tofauti, mbunge mmoja wa Bara jimbo lake ni sawasawa na majimbo matano ya Ugunja,” amesema Raza na kumuomba Rais Magufuli baada ya uchaguzi wabunge wa Bara waweze kuongezewa fedha za jimbo.
Amesema wao Zanzibar jimbo moja wana mwakilishi na mbunge, siku moja wanaweza kutembelea jimbo hilo na kulimaliza, lakini ndugu zao wa Bara wanaweza kutumia siku tano.
Aliiomba CCM kuweka sera maalum kupitia mfuko wake kuweza kuwasaidia wabunge wa Bara. Amesema hata kama kuna mfuko wa jimbo, wapewe fedha za ziada kutoka mfuko wa CCM, kwani Zanzibar jimbo moja anapata mbunge na anapata mwakilishi, lakini upande wa bara anaona mzigo ni mkubwa kwa wabunge.
More Stories
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake
HGWT yawataka wazazi na walezi kulinda watoto dhidi vitendo vya ukatili
ACT-Wazalendo,waitaka Polisi kutobeba chama kimoja