May 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mambo matatu yanayovutia wawekezaji wa Ujerumani kwenye uongozi wa Samia



Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

UONGOZI wa Rais Samia Suluhu Hassan, umezidi kuimarisha uhusiano na mataifa mbalimbali ambao umesaidia kufungua fursa nyingi, hasa za uwekezaji katika nyanja mbalimbali.

Ndani ya uongozi wake tumeshuhudia viongozi wa mataifa mbalimbali wakifanya ziara hapa nchini ambazo zimeimarisha ushirikiano.

Lakini pia kupitia ziara za wakuu wa nchi hapa nchini, tumeshuhudia yakifanyika makongamano baina ya wafanyabiashara wa Tanzania na wa nje ambapo mikataba mbalimbali imesainiwa.

Wiki hii Watanzania wameshuhudia ziara nyingi ya kihistoria iliyofanywa na Rais wa Shirikisho la Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier.

Ziara ya Rais Steinmeier,hapa nchini haikuja kwa bahati mbaya na hiyo inadhihirishwa na kauli yake ambapo alipongeza utulivu uliopo nchini, akitaja mambo matatu kwenye masuala ya demokrasia, utawala wa sheria na utawala bora.

Utulivu huo anasema umepelekea wafanyabishara wa Ujerumani kuja Tanzania kuangalia fursa za uwekezaji. Utulivu huo ambapo anaueleza Rais Steinmeier ni matunda ya uongozi wa Rais Samia, kwani Watanzania wengi wanaelewa mazingira ambayo aliyakuta katika nyanja za kidemokrasia, utawala bora na utawala wa sheria mwaka 2021 alipopewa kijiti cha kuongoza Tanzania.

Rais huyo anaweka wazi kufurahishwa na moyo wa Rais Samia wa kuendelea kudumisha na kuendeleza uhusiano huo baina ya nchi hizo mbili kwa ajili ya kesho yetu.

Anasema ujio wake nchini Tanzania umepokelewa vizuri sana na watu wa Ujerumani pamoja na Dar es Salaam na wana shauku, kwani wameona namna Rais Samia alivyoweza kujenga uchumi na katika suala zima la utawala wa sheria na utawala bora.

“Tumeona kazi kubwa ambayo imeishafanyika hata katika suala zima la kidemokrasia. Tumeona namna ambavyo umeweza kufanyakazi nzuri, tunapenda kuwahakikishia sisi watu wa Shirikisho la Ujerumani tunakwenda kusimama na ninyi kwa karibu,” anasema Rais Steinmeier.

Anafafanua kwamba urafiki baina ya Tanzania na Ujerumani  utaendelea kuwepo kwa sababu ya uaminifu ambao nchi hizo mbili zinao.

Anaongeza kuwa ziara hiyo italeta matunda mazuri sana kwa upande wa mahusiano ya kiuchumi na katika sekta mbalimbali, hivyo ana uhakika wataweza kusimama na kutumia zaidi fursa zinazotokana na mahusiano baina ya nchi hizo mbili.

Rais Steinmeier, anasema katika mazungumzo yao na Rais Samia walijadili juu ya uhusiano wa nchi hizo mbili na namna uhusiano huo utakavyoendelea kuwa na nguvu zaidi na kuvuka hata mipaka ya kisiasa.

Rais Steinmeier, anasema ni muhimu kuwa na watu ambao ni wabobevu zaidi katika suala zima la uchumi wa kidigitali ili kuongeza ajira kwa kizazi kijacho.

Aidha, anasema waliongelea suala zima la watalii kutoka Ujerumani  ili kuendelea kudumisha ushirikiano baina ya nchi mbili na katika maeneo mengine, kielimu, kitamaduni.

Rais Steinmeier anasema nchi hizo mbili zina ushirikiano wa karibu kwa miaka mingi, wameona vyuo vingi vinatoa kozi mbalimbali ambazo zinawaleta karibu wanafunzi wa Tanzania na Ujerumani.

Aidha,  anasema walijadiliana namna ya kujenga mahusiano karibu katika maeneo mengine ya ushirikiano na maeneo mengine ya ushirikiano.

Anasema kongamano la wafanyabiashara wa Ujerumani na Tanzania litawafungua na kuweza kuona ni namna gani wanaweza kufanyakazi kwa karibu .

Anasema amefurahi kuwepo tena Tanzania, kwani hiyo sio mara ya kwanza. “Nimeshafika hapa mara mbili, lakini sasa hivi ndiyo nakuja mara ya kwanza kama Rais wa Shirikisho la Jamhuri ya Watu wa Ujerumani.”

Kupitia ziara hiyo, Rais huyo wa Ujerumani imeiomba radhi Tanzania kwa makosa ya ukatili na mauaji yaliyofanywa ya wanajeshi wa nchi hiyo wakati wa vita ya Maji Maji.

Aidha, ametaka kukubali kufanyika mazungumzo baina ya Serikali hiyo ili kutumia suala hilo kuimarisha mahusiano kwa faida ya nchi zote mbili.

Rais Steinmeier alitoa kauli hiyo alipotembelea Makumbusho ya Kumbukumbu ya Vita vya Maji Maji Songea mkoani Ruvuma.

Katika ziara hiyo alitembelea makumbusho na kufanya mazungumzo na baadhi ya ndugu wa marehemu mashujaa wa vita hiyo na hatimaye kutoa heshima kwa mashujaa wa vita hivyo katika makabuli yaliyopo katika makumbusho hayo.

“Nimeguswa sana, ninaona aibu kwa majeshi ya wajerumani waliyowatendea, lakini licha ya historia hii ninaomba msamaha kwa mambo waliyoyatenda.” Anasitiza Rais Steinmeier.

Aidha, anasema Serikali yake ipo tayari kushirikiana na Serikali ya Tanzania kuyapatia majawabu maswali yote yanayohusiana na suala hili kwa faida ya pande zote mbili.

Kwa upande wake Rais Samia, anasema ziara ya Rais wa Shirikisho la Watu wa Ujerumani, Steinmeier, hapa nchini ni ishara njema kuhusu umuhimu wa uhusiano kati ya nchi hizo mbili na inathibitisha dhamira yake ya kuendeleza uhusiano huo wa kihistoria.

Rais Samia anasema yeye na Rais Steinmeier, walipata fursa ya kuzungumza kuhusu masuala muhimu yanayohusu uhusiano na ushirikiano kati ya Tanzania na Ujeruman.

Kwanza, Rais Samia anasema wamezungumzia kuhusu ushirikiano wa kijamii na kiuchumi, ambapo uhusiano baina ya nchi hizo mbili umefikisha miaka 60.

Kwa mujibu wa Rais Samia katika kipindi chote hicho, nchi hizo zimekuwa zikishirikiana vyema.

“Serikali ya Ujerumani imekuwa ni rafiki, mbia mzuri ambaye tulishikana vizuri mkono katika mambo mengi, “anasema Rais Samia.

Anataja sekta ambazo Tanzania ilifanyakazi na Serikali ya Ujerumani kuwa ni pamoja na masuala ya afya.

“Kama mnavyojua suala la Bima ya Afya tulitaka usaidizi kutoka kwao, lakini pia Serikali ya Ujerumani inajenga hospitali nzuri na kubwa sana ya Jeshi, pale Dodoma, lakini pia imetusaidia kujenga hospitali kubwa na ya kisasa ya maradhi ya kuambukiza Lugalo,” anasema Rais Samia.

Aidha, anasema Ujerumani imekuwa ikiisadia Tanzania katika masuala ya usambazaji maji safi na salama, masuala ya kilimo, elimu, elimu ufundi, utalii na utamaduni na michezo.

“Ulinzi tunashirikiana vizuri, maliasili na udhibiti wa fedha.” Alisema katika mazungumzo yao wamesisitiza umuhimu wa kukuza ushirikiano wa nchi hizo na watu wake.

“Na katika hili, tumezielekeza timu za watalaam wa Tanzania na Ujerumani kuendelea na mazungumzo pamoja na mashauriano ya mara kwa mara yanayolenga kuboresha maeneo yaliyopo ya ushirikiano na kuibua maeneo mengine mapya yenye umuhimu wa kuinua uchumi wa nchi hizo mbili,”anasema Rais Samia.

Anasema katika hilo, amemhakikishia Rais Steinmeier kwamba Serikali ya Tanzania ipo tayari kuwa mwenyeji wa mazungumzo ya yajayo ya ushirikiano wa maendeleo yatakayofanyika mwakani 2024.

Kwa upande wa biashara na mahusiano ya uwekezaji, Rais Samia alisema walizungumza na kusisitiza mchango wa biashara na uwekezaji katika kuchochea mchango mzima wa kijamii na kiuchumi, ambapo Ujerumani ina miradi 180 katika ngazi mbalimbali ambayo imewekezwa hapa nchini.

“Lakini pia tumekuwa tukifanya biashara na Ujerumani, ingawa bado kuna uwezekano mkubwa wa kukuza biashara na hilo watalielekeza kwenye mazungumzo yajayo,” anasema Rais Samia.

Anasema kwenye kongamano la wafanyabiashara baina ya Tanzania na Ujerumani, huko, ndiko fursa zote za uwekezaji na biashara zitaelezwa na pengine watakaokubaliana wataingia mikataba.

Rais Samia alipongeza kazi nzuri iliyofanywa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar, Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Kijerumani katika kuandaa kongamano hilo ili kuwezesha biashara na kukuza uwekezaji kati ya nchi hizo mbili.

Kwa upande wa utalii, Rais Samia anasema wamekuwa wakifanyakazi vizuri, wamekuwa wakipata watalii kutoka Ujerumani, lakini bado kuna uwezekano wa kupata idadi kubwa zaidi ya watalii kutoka Ujerumani pale watakapojitangaza vizuri kwao.

“Lakini tumekuwa tukishirikiana katika uhifadhi na mashirika mengine ya Ujerumani yamekuwa yakitusaidia katika uhifadhi wa mbuga zetu hasa Selou na Serengeti,”anasema Rais Samia.

Anataja mambo mengi waliozungumza kuwa ni ya kihistoria, ambapo Tanganyika na Zanzibar kwa kipindi kidogo zilikuwa chini ya utawala wa Mjerumanina.

Anasema katika utawala huo, mambo mengi yamepita na walizungumza kwa urefu wakati wa mazungumzo yao.

Anasema wapo tayari kufungua majadiliano ya kuona jinsi ya kukubaliana wa yale yaliyopita nini wafanye. “Na nina jua kuna familia ambazo bado zinasubiri mabaki ya wapendwa wao, ambao wako Ujerumani katika makumbusho mbalimbali za Ujerumani, yote hayo tunaenda kuyazungumza na kuona vipi tuende nayo vizuri,” alisema.

Anaongeza kuwa Tanzania wanaangalia usawa wa jinsia na uwezeshaji wa wanawake kiuchumi.

Rais Samia anaongeza kwamba; “Kwenye masuala ya demokrasia, haki za binadamu, utawala wa sheria na utawala bora wamezungumza na Rais wa Ujerumani, Steinmeier amepongeza Tanzania kwamba Tanzania tunaonekana tumetulia kwenye utawala wa sheria, utawala bora, ndiyo maana wamevutika,”alisema.

Anasema ziara hiyo inathibitisha dhamira ya Serikali zote mbili za kuimarisha na kukuza ushirikiano wa urafiki wa nchi hizo kwa lengo la kunufaisha watu wetu.