October 30, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Malolo wafurahia maboresho miundombinu ya elimu

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online,Tabora

WAKAZI wa Kata ya Malolo Halmashauri ya Manispaa Tabora wameeleza kufurahishwa na maboresho ya miundombinu ya Shule ya Msingi Mawiti iliyopo katika Kata hiyo ambayo yamesaidia watoto wengi zaidi kupenda shule.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwenye mkutano wa hadhara ulioandaliwa na Diwani wa Kata hiyo Naomi Kasanga wameeleza kuwa mazingira ya shule hiyo yalikuwa hayafurahishi hata kidogo.

Ofisa Mtendaji wa Kata hiyo Naima Mbwela ameishukuru Serikali ya kwa kuwapatia zaidi ya sh.mil 13 kwa ajili ya ujenzi wa matundu 6 ya vyoo vya wavulana.

“Shule yetu ilikuwa na uhaba wa matundu ya vyoo hali iliosababisha watoto kupata shida huku wengine wakilazimika kujisaidia vichakani.Lakini sasa hali imekuwa shwari, hakuna mtoto anayejisaidia vichakani tena,” amesema na kuongeza:

“Vyumba vya madarasa navyo vilikuwa vichache, lakini Serikali imetupatia zaidi ya sh.milioni 137 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba 3 vya madarasa, jengo la awali na matundu 12 vya vyoo, haya ni maboresho makubwa,”.

Kasanga ameeleza kufurahishwa na mafanikio makubwa waliyopata tangu achaguliwe mwaka 2025,ambapo amedai kata yao imepiga hatua kubwa kimaendeleo katika sekta zote ikiwemo elimu.

Amebainisha kuwa ushirikiano wa wananchi, wadau na Serikali umekuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo ya kata hiyo,na kusaidia miundombinu ya Shule ya Msingi Mawiti kuendelea kufanyiwa maboresho makubwa.

Ametaja mafanikio mengine kuwa ni kufukua mtaro mkubwa wa maji ili kuepusha mafuriko ya mvua za El-nino,kutoa mkopo nafuu wa zaidi ya sh.mil 55 kwa vikundi 4 vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu ili kuwainua kiuchumi na kujengwa Ofisi ya Mtendaji wa Kata kwa gharama ya sh.mil 20.

Mjumbe wa Kamati ya Siasa wa Kata hiyo Ramadhan Athuman, ameeleza kufurahishwa na juhudi zilizofanywa na zinazoendelea kufanywa na Serikali ili kuhakikisha shule yao inakuwa na mazingira bora ya kusomea watoto.