October 30, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

NeST yafungua milango ya uchumi kwa vijana,wanawake

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira

UNUNUZI wa umma unaendelea kuwa moja ya milango muhimu ya ushiriki wa Watanzania katika uchumi, huku matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa zabuni yakipanua fursa za biashara kutoka kampuni kubwa hadi vikundi vya wananchi wanaotaka kujikwamua kiuchumi.

Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) imesema zabuni 430,643 zenye thamani ya Sh trilioni 42.6 zimetolewa kupitia Mfumo wa Ununuzi wa Umma Kielektroniki (NeST), unaowawezesha wazabuni kushiriki katika michakato ya zabuni bila kulazimika kufuata taratibu za kuwasilisha nyaraka kwa njia ya kawaida.

Ukubwa wa soko hilo unaonesha nafasi ya ununuzi wa umma katika kukuza biashara za ndani, kuongeza ushiriki wa wajasiriamali na kufungua fursa za kiuchumi kwa wananchi katika ngazi mbalimbali.

Akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari katika muendelezo wa mikutano inayoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina, jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mkuu wa PPRA, Dennis Simba, amesema mfumo huo umeleta mabadiliko katika usimamizi wa zabuni, ikiwamo kurahisisha ushiriki wa wazabuni na kuongeza uwazi katika michakato ya ununuzi wa umma.

Amesema mfumo huo unamuwezesha mzabuni kushiriki katika zabuni akiwa mahali alipo, huku akifuatilia mchakato wa maombi yake na malipo ya mikataba kupitia huduma za kielektroniki.

Hatua hiyo ina umuhimu kwa wajasiriamali wanaotaka kushindana katika soko la Serikali, kwa kuwa inapunguza ulazima wa kusafiri kuwasilisha nyaraka za zabuni na gharama zinazohusiana na utaratibu huo.

Katika kuimarisha ushiriki wa wananchi katika uchumi, mfumo wa NeST unatumika pia kuwezesha makundi maalumu kushiriki katika zabuni za Serikali.

Kwa mujibu wa Simba, makundi 33,659 ya vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu yamesajiliwa kwenye mfumo huo, huku yakiwa yamepata zabuni zenye thamani ya Sh bilioni 82.34.

Kati ya thamani hiyo, vikundi vya vijana vimepata zabuni za Sh bilioni 44.74, wanawake Sh bilioni 33.15, wazee Sh bilioni 3.78 na watu wenye ulemavu Sh milioni 680.21.

Sheria ya Ununuzi wa Umma inaelekeza taasisi za umma kutenga asilimia 30 ya bajeti zao za ununuzi kwa ajili ya makundi maalumu, hatua inayolenga kupanua ushiriki wa makundi hayo katika shughuli za kiuchumi.

PPRA inalenga kuongeza idadi ya makundi yaliyo tayari kushiriki zabuni hadi kufikia 300,000, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kujenga uchumi unaowapa wananchi nafasi ya kunufaika na fursa zilizopo.

Kwa mujibu wa hotuba hiyo, kikundi kinaweza kupata zabuni moja yenye thamani ya hadi Sh milioni 500, huku wananchi wakihimizwa kuungana katika vikundi, kujisajili katika halmashauri zao na kujiunga na mfumo wa NeST.

Matumizi ya teknolojia yamekuwa sehemu muhimu ya maboresho ya ununuzi wa umma, kwa kuwezesha michakato mingi kufanyika kwa njia ya kielektroniki.

PPRA imesema kiwango cha uzingatiaji wa sheria katika ununuzi wa umma kimeongezeka kutoka asilimia 65 katika mwaka wa fedha 2023/24 hadi asilimia 79 katika mwaka wa fedha 2025/26.

Aidha, matumizi ya NeST yamewezesha kuzuia uchapishaji wa zaidi ya kurasa milioni 288.57 za nyaraka za zabuni, hatua ambayo kwa mujibu wa mamlaka hiyo imeokoa takribani Sh bilioni 27.64.

Mfumo huo pia unawezesha maandalizi, uhakiki na usainishaji wa mikataba kufanyika kidijitali, huku ukiunganishwa na mifumo mingine ya Serikali na taasisi za fedha ili kuboresha uhakiki wa nyaraka na dhamana za zabuni.

Katika hatua nyingine, PPRA imeanzisha programu ya simu ya NeST Tenderer, inayopatikana kupitia Play Store na App Store. Programu hiyo inamwezesha mtumiaji kujisajili, kuomba zabuni na kufuatilia malipo ya mikataba.

Sheria ya Ununuzi wa Umma imeweka utaratibu wa upendeleo kwa wazabuni wa ndani, ikiwamo zabuni zenye thamani isiyozidi Sh bilioni 50 kutengwa kwa wazawa pekee, kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa na PPRA.

Pia, upendeleo wa hadi asilimia 10 umewekwa kwa wazabuni wa ndani katika zabuni zinazohusisha ushindani wa kimataifa, huku bidhaa zinazozalishwa nchini zikipata upendeleo wa hadi asilimia 15 dhidi ya bidhaa za nje.

Hatua hizo zinalenga kuongeza nafasi ya kampuni na wazalishaji wa ndani kushiriki katika soko la ununuzi wa umma na kuchangia ukuaji wa shughuli za kiuchumi nchini.

Kwa ujumla, upanuzi wa matumizi ya NeST unaweka teknolojia katika nafasi ya kuwawezesha wananchi kupata taarifa za zabuni, kushiriki katika michakato ya ununuzi na kufuatilia hatua za mikataba.

Changamoto na fursa zilizopo sasa ni kuhakikisha wajasiriamali wengi zaidi wanauelewa mfumo huo na wanajenga uwezo wa kuandaa maombi yenye ushindani, kutekeleza mikataba kwa viwango vinavyotakiwa na kutumia fursa hizo kukuza biashara zao.

Hivyo, ununuzi wa umma si mchakato wa Serikali kupata bidhaa na huduma pekee, bali pia ni njia inayoweza kuwaunganisha wajasiriamali na soko, kuchochea uzalishaji wa ndani na kupanua ushiriki wa wananchi katika uchumi wa Taifa.