December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Historia ya Malenga wa Kiirani Saadi Shirazi

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Musharraf al-Din Mosleh ibn Abdullah ibn Musharraf, ambaye baadaye alijulikana kama Saadi Shirazi, ni mmoja kati ya malenga na mshairi mkubwa na mashuhuri nchini Iran.

Wanahistoria wanaamini kwamba Saadi Shirazi alizaliwa kati ya mwaka 600 na 610 Hijiria (sawa na takriban mwaka 1210 Miladia). Walakini, hakuna tarehe kamili inayojulikana ya  kuzaliwa kwa malenga huyu,  ingawa wanahistoria  wanakadiria  mwaka huo wa kuzaliwa kulingana na athari za kazi zake.

Saadi alizaliwa katika familia ya wanazuoni, wasomi na watu wenye maadili mema. Baba yake alikuwa mfanyakazi wa Mahakama ya Atabak na Shah Saad bin Zangi. Wengine wanaamini kwamba mshairi huyu amechagua jina la ukoo la Saadi kama ni mtu mwenye utambuzi wa haki. Mbali na kuhudumu katika mahakama, baba yake pia alikuwa akijishughulisha na masuala ya kidini na alikuwa akimshajiisha mno mtoto wake kujifundisha elimu ya kisekula na kidini pia. Kwa msaada wa baba yake, Saadi alipata ujuzi wa kina katika nyanja za historia na fasihi.

Wakati wa kuzaliwa kwake, mtawala wa Shiraz alikuwa mfalme wa tatu wa serikali ya Atabakan. Nguvu ya Waseljuk ilipodhoofika siku baada ya siku katika kutawala nchi, uliibuka mlolongo wa utawala wa kieneo. Mbali na Shiraz, Atabak pia alikuwa na nguvu za kiutawala huko Damascus, Mosul, Aleppo (Halab), Mesopotamia ( Furati na Hidekeli), na Azerbaijan.

Baba yake Saadi alifariki dunia, wakati Saadi akiwa na umri wa miaka 12, na babu yake mzaa mama, Massoud ibn Mosleh, alichukua jukumu la kumlea na kumtunza mjukuu wake.

Katika wasifu wa Saadi, tunasoma kwamba baada ya mshairi huyu kujifunza misingi ya elimu ya kidini na fasihi huko Shiraz, alikwenda Baghdad akiwa  bado barobaro na kijana chini ya usimamizi wa Atabak na akajiunga katika  madrasa ya Nidhamiyyah. Shule hii  ilikuwa inatoa elimu maalumu kwa watu wanaotaka kujikita zaidi katika nyanja za fiqh ( sheria za Kiislamu)  na falsafa. Wanazuoni wakubwa kama vile Suhrawardi walimlea  kielimu Saadi katika madrasa hiyo.

Baada ya kumaliza mafunzo, Saadi akaazimia kufanya safari katika maeneo ya Hijaz, Sham na Syria kwa lengo la kupata elimu na uzoefu zaidi. Baada ya hapo akashika njia na kuelekea Makka. Wakati huo huo, alifanikiwa kufunga ndoa, na  kisha alifanikiwa kupata mtoto, lakini baada ya kumpoteza mtoto wake huyo, Saadi aliamua kusafiri tena ili kuvumilia mateso hayo, mateso ambayo yalimfanya awe mwenye kupenda zaidi mashairi.

Saadi alitembelea miji  mbalimbali duniani kote na huko alijishughulisha zaidi na kufundisha na kuhubiri katika miji hiyo.

Wataalamu wengine wa historia wamethibitisha kufanya  safari yake ya India na sehemu nyingine kadhaa za dunia, na wanaeleza kuwa, safari hizo zilidumu takriban miaka 30. Hata hivyo, muda wa safari na maeneo aliyotembelea  Saadi, ni mambo ambayo bado yanatiliwa shaka mno.  

Hatimaye, baada ya kupita miaka mingi na kupata uzoefu wa kutosha, malenga huyu aliamua kurudi katika  nchi yake na mji wake wa asili wa Shiraz. Wakati wa kurejea kwake Shiraz, Abu Bakr ibn Sa’d, mfalme wa Atabaki, alikuwa akitawala huko Shiraz wakati huo. Na kulingana na baadhi ya maelezo ya watu, mshairi huyo  alichukua jina la ukoo wa Saadi kutoka kwa jina la mfalme (Saad).

Baada ya Saadi  kurejea Shiraz, mshairi huyu alianza kuandika na kukusanya kazi zake. Kazi yake ya kwanza aliyoiandika ilikuwa kuandika kitabu cha mashairi alichokipa jina la Bustan, mnamo mwaka 655 Hijria, na kukabidhi mkusanyiko wa mashairi hayo kwa mfalme aliyekuwa akitawala kipindi hicho aitwaye Abubakar ibn Sa’d Zangi.

Kitabu cha mashairi cha Golestan kilichoandikwa na malenga huyu mkubwa kilitungwa mwaka wa 656 Hijiria, mwaka mmoja baada ya kuandikwa kwa kitabu cha Bustan. Saadi alikamilisha uandishi wa mashairi ya kitabu hicho kwa muda mfupi.

Kuandikwa kwa vitabu viwili katika muda mfupi kunaonyesha kwamba,  kwa kiasi kikubwa mashairi hayo  yalikuwa yameshatayarishwa mapema, bali alichokifanya ni kukusanya na kufanya masahihisho katika hatua za mwisho kabla ya kuchapishwa.

Mengi yamesemwa kuhusu  Saadi juu ya ustadi  na umahiri wake, na hasa kuhusiana na uzuri wa mashairi na uzoefu wake, lugha na maneno anayotumia, ni miongoni mwa mambo yaliyoleta chachu kwa baadhi ya waandishi na washairi  wengine kuiga mfumo wa tungo za mashairi ya malenga huyo.

Kitabu cha Bustan, kinachoitwa “Saadi Nameh”, kiliandikwa wakati Saadi alipokuwa akisafiri sehemu mbalimbali za dunia. Kazi hii, ambayo imefanyika katika mfumo wa Masnavi, maudhui yake yamelenga  zaidi katika nyanja ya maadili, malezi, siasa na masuala ya kijamii.

Moja ya sifa kuu za kazi na athari za Saadi, ambazo zimesababisha kuenea athari hizo kwa watu mbalimbali duniani, ni usahili wa kazi zake. Kitabu cha Bustan, pamoja na lugha yake kuwa ni nyepesi, kina mafuhumu na maudhui ya kina ya kimaadili.

Kitabu cha Bustan kina faslu (sura) kumi, na kila moja ina maudhui maalumu kwa mfano; unyenyekevu, uadilifu na usawa, tadaburi, kushukuru na kadhalika.

Kitabu cha Bustan kina karibu beti 4,000 na nakala zake nyingi zimechapishwa na kusambazwa sehemu kadhaa duniani. Tunaweza kusema kuwa, Bustan ni kitabu cha maadili na mafundisho ambapo Saadi ameelezea uwepo wa sifa za mji wake.

Golestan ni kitabu cha nathari  kinachoonekana na watu wengi kuwa ni chenye taathira kubwa katika fasihi ya lugha ya Kifarsi, na kilichapishwa mwaka mmoja tu baada ya kuchapishwa kitabu cha Bustan.

Sanaa iliyotumiwa na mshairi Saadi katika kitabu cha Golestan  ina mvuto wa kipekee kwa matabaka yote na yeyote atakayekisoma kitabu hicho atakuwa ni mwenye kuathirika na maneno yake. Kwa hakika, Golestan ni aina ya kioo kwa jamii katika zama zake, kwani ndani ya kitabu hicho kumeonyeshwa hali ya kiutamaduni na kijamii ya watu waliokuwa wanapenda ushairi  maalumu wa malenga Saadi.  

Kipande mashuhuri cha shairi Bani-Adam katika sura ya kwanza ya Golestan kinaeleza kuwa (sio kwa muundo wa kishairi):

     “Wanadamu ni washiriki wa jumla,

      Katika uumbaji  ni chanzo na nafsi moja.

      Ikiwa kiungo kimoja kinaumwa na maumivu,

      Viungo vingine vitabaki na  wasiwasi.

      Ikiwa huna huruma kwa maumivu ya binadamu,

      Jina la mwanadamu huwezi kulihifadhi!

Kipande hicho cha beti ya shairi la Saadi kinaweza kuonekana hadi leo kikining’inia kwenye mlango wa Umoja wa Mataifa huko New York.

Lengo la mashairi yake mengi ni mapenzi na upendo. Saadi anachukuliwa kuwa mmoja wa washairi wachache ambao beti zake za upendo na mapenzi zimesalia, zinaenziwa na kuelezewa tangu  kipindi hicho hadi sasa.

Mikutano Mitano, Mkataba wa Hekima na Upendo, na Ushauri wa Wafalme ni vitabu vingine vya Saadi, ambavyo ufasaha wake na haiba yake ni sawa na vile vitabu viwili mashuhuri vya mshairi huyu, yaani  Bustan na Golestan.

Uandishi wa vitabu viwili, Bustan na Golestan, ulimfanya malenga  huyo kuwa maarufu mno. Baada ya kuandika vitabu hivi viwili, Saadi aliishi Shiraz na akatumia  muda wake wote kutunga mashairi na kutafakari, na kupelekea uaarufu wake kuenea nchi kadhaa duniani.

Sifa mojawapo mashuhuri ya kazi za mshairi huyu ambayo imempa umaarufu duniani ni wepesi mashairi yake. Mashairi ya Saadi yanaonekana kuwa ni rahisi na yenye ufasaha  na maneno magumu na yasiyoeleweka hayaonekani ndani yake.

Kupunguza misemo isiyo na maana katika ushairi sio tu haipunguzi uzuri wa maneno, lakini pia inafanya kuwa mazuri zaidi na yanayoeleweka kwa msomaji. Hakuna maneno ya ziada yanayoweza kupatikana katika beti za mashairi ya Saadi.

Muziki na mnyambuliko wa mashairi ya Saadi na mbwembwe zake, humrahisishia  msomaji  katika kusoma mashairi ya mshairi huyu. Kawaida hutumia uzito wa arudhi katika mashairi yake. Safu za kifasihi zinazofanya mashairi kuwa na sauti pia zinaweza kupatikana kwa wingi katika kazi za Saadi, kama vile: fonolojia, tamathali za semi, mizani ya upatanifu, urudiaji wa maneno, na kadhalika.

Mshairi huyu fasaha, kwa kutumia vipengele hivi kwa werevu, hutia uhai katika mashairi yake na kuyafanya yawe changamfu zaidi.

Saadi, mmoja wa washairi wakubwa wa Iran, amekuwa akifundisha na kuendeleza sayansi na fasihi ya wale wanaomzunguka katika  maisha yake yote. Wasifu wa Saadi umejaa matukio mazuri na yenye kuvutia. . Wengi hawamchukulii kuwa mshairi mwanafalsafa, lakini Saadi ni mshairi anayetoa mafundisho ya maadili. Maadili na fasihi, mafundisho ya kijamii na kisiasa ni miongoni mwa mambo ambayo mshairi huyu alisisitiza mno kwenye kazi kaze kila mara.

Katika kazi zake za ushairi, Saadi anajaribu kueleza makosa ya wale walio karibu naye kwa kutumia  lugha ya ucheshi na laini, mbali na ukosoaji mkali,  hufundisha maadili  bora na mema  kwa wale walio karibu naye.

Hata hivyo, wasifu wa mshairi Saadi hauonyeshi  tarehe au mwaka kamili wa kifo chake. Tarehe ya kifo cha mshairi huyu mashuhuri wa Kiirani imetajwa katika vyanzo mbalimbali vya kuanzia mwaka 690 hadi 695 Hijiria. Baadhi ya wanahistoria wanaamini kwamba mshairi huyu wa thamani alikufa mwaka 690 Hijiria katika nyumba ya watawa alimokuwa akiishi.  Kaburi la  malenga Saadi  liko katika mji wa Shiraz ulioko katika mkoa wa Fars nchini Iran.