March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Maktaba ya taifa kujengwa Dodoma

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online- Dodoma

MGOMBEA Mwenza wa kiti cha urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Emmanuel Nchimbi, amesema miongoni mwa mipango ya chama hicho kwa miaka mitano ijayo kikirudi tena madarakani ni kujenga maktaba ya taifa mkoani Dodoma.

Dkt. Nchimbi ameyasema hayo Oktoba 17, 2025, katika mkutano wake wa hadhara wa kampeni za CCM uliofanyika Dodoma Mjini,akiomba kura kwa ajili ya waogombe wa nafasi mbalimbali wa chama hicho ikiwemo Urais, Wabunge na Madiwani,katika uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 29,2025, ambapo zimesalia takribani siku 11.

“Maktaba hiyo itahifadhi kumbukumbu, nyaraka na maandiko mbalimbali ya kitaifa, na itatumiwa na watafiti, wanafunzi na wananchi kwa ujumla kwa maslahi ya taifa,”amesema Dkt.Nchimbi.

Dkt.Nchimbi ameeleza kuwa Serikali ya CCM pia imedhamiria kujenga shule mpya za msingi 21 na sekondari 16, madarasa 150, maabara 15 za sayansi na mabweni 17 ili kuboresha mazingira ya elimu na kupunguza msongamano darasani.

Hata hivyo baada ya kufanya mkutano wa kampeni Dodoma Mjini, ikiwa ni mkutano wa mwisho mkoani humo huku leo Oktoba 18,2025,Dkt.Nchimbi ataanza mikutano ya kampeni mkoani Morogoro.

Tangu kuanza kwa kampeni Dkt.Nchimbi amefanya mikutano ya kuomba kura za wagombea wa chama hicho katika mikoa 24.