January 13, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Makonda atoa maagizo kwa Mkurugenzi wa Hanang

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

MKuu wa Mkoa wa Manyara Queen Sendiga amemuagiza Mkurugenzi wa Hanang  Francis Namauombo kwa kumpa siku 5 kulipa deni la Tsh Milioni 27.5 kwa Vijana waliofanya kazi ya kutengeneza madirisha ya shule.

Hatua hiyo imekuja mara baada ya Katibu wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi Taifa, Itikadi, Uenezi na Mafunzo Ndugu. Paul Makonda kutoa maelekezo ya CCM kwa Mkuu wa Mkoa kuhakikisha kikundi cha Vijana wanaodai fedha zao kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Hanang. Francis E. Namaumbo zinalipwa.

“Vijana wana haki kwa namna nilivyosikiliza vema malalamiko na majibu ya Mkurugenzi wetu hivyo naomba nikuhakikishie Ndugu Mwenezi Makonda kama serikali ilifanya ubovu wa kusainj hati mbovu na ubovu huohuo wautumie kuwalipa pesa zao Vijana hawa na namuagiza hapa Mkurugenzi huyo wa Hanang kuhakikisha ndani ya siku 5 hadi kufikia Januari 30 pesa hizo zote Milioni 27.5 ziwe zimelipwa kw Vijana hao ” Alisema RC Sendiga

Mmoja kati ya Wananchi wa Hanang aliyasema malalamiko hayo kwa Mwenezi Makonda aliposimama kuwasalimia Wananchi wa Mji mdogo wa Katesh akiwa njiani kuelekea Mkoani Singida jana tarehe 25 Januari, 2024.

Mwananchi huyo alieleza kuwa walifanya kazi ya kutengeneza madirisha ya shule yenye thamani ya Tsh Milioni 27.5 na angali tayari mhandisi wa Wilaya alishawapatia hati ya kuonesha kumalizika kwa kazi tangu mwezi Septemba, 2023 na bado hawakilipwa na baada ya kusikikia kwa ujio wake ndio akaitwa na kupelekwa site kisha akaambiwa hakuna ubora wa kazi aliyoifanya na kudai wamlipe Tsh Milioni 13.5 hali iliyopelekea kutokukubaliana na hilo.

Mara baada ya kusikiliza pande zote mbili, Mwenezi Makonda alibaini makosa ndani ya Ofisi ya Mkurugenzi na Kumtaka Mkuu wa Mkoa wa Manyara kwa mamlaka aliyonayo kutoa neno na ndipo akaagiza ndani ya siku 5 kulipwa kwa fedha hizo Tsh Milioni 27.5 kwa Vijana hao.

“Tunawezaje kuwajengea Uchumi Vijana wa Nchi yetu kama iwapo hata kazi wanazofanaya kwenye Serikali yetu na bado hamuwalipi? Rais Samia anawapenda Vijana na kuwaamini kufanya hivi ni kumkosea na kuwanyima haki Vijana wetu” Alisema Mwenezi Makonda.

Makonda alisema wameamua wao kwenye Chama kuipeleka serikali maabara, waipime kidogo ili waone wapi kuna shida

“Chama hiki hakipaswi kushindwa na hakuna sababu ya kushindwa kwasababu serikali Ina Bajeti na watendaji mpaka serikali za mitaa, tunataka Chama chetu kiwe Cha ukweli kushughulikie kero za wananchi kwasababu heshima ya Chama Cha Mapinduzi ni kutatua changamoto za wananchi”

“Sisi hatupendwi kwasababu ya nguo zetu za kijani, hatuheshimiki kwasababu ya nguo zetu za njano, tunaheshimika kwasababu nyinyi wananchi mmetupa kura tukajenga serikali na serikali inawafanyia kazi nyinyi”

Kadhalika, Makonda aliposimama kusalimiana na Wananchi wa eneo la Katesh, alibainisha mwananchi mmoja kupokonywa bango na polisi alilondika kero yake Pamoja na kuvunjiwa nyumba yake kutokana na kuonekana kutoa taarifa ya baadhi ya Askari kukamata wanywa gongo na kuomba kupewa hongo ya Tsh 700,000/=.

Mara baada ya kusikiliza malalamiko hayo, Mwenezi Makonda alibaini kuwa kutokana na Mwanachi huyo kutoa taarifa ya askari kutaka rushwa ndio imepelekea Askari hao kwa kushirikiana na watu wa Ardhi Halmashauri ya Hanang kwenda kuvunja nyumba ya Mwananchi na angali Mwananchi huyo ameeleza kuwa kesi ya mgogoro wa mipaka baina yake na eneo la polisi ilishafutwa mahakamani kutokana na kukosekana kwa ushahidi ya kuwa ni eneo la polisi mahali alipojenga nyumba yake na nyaraka za mahakama anazo.

Baada ya hayo, ndipo Mwenezi Makonda akatoa maagizo ya CCM ya kumtaka Mkuu wa Wilaya kukaa na OCD na Mwananchi huyo kwa kushirikisha anapewa haki zake.

Vilevile alimtaka DC Hanang kuhakikisha yaliyosemwa na mzee huyo kuhusiana na askari kutaka rushwa kama yakithibitika basi hatua za kisheria na kinidhamu zichukuliwa kwa Askari hao.

Mbali na hayo, Makonda alimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na wananchi wote kwa ujumla ikiwemo Viongozi wa Dini, Kimila na Taasisi mbalimbali kufika Hanang kuungana na wananchi wa eneo hilo kuwapa misaada mbalimbali kutokana na maafa waliyoyapata siku za hivi karibuni.

“Tunamshukuru sana Rais wetu kuonyesha uongozi hodari na Mahiri kwa kuacha kilakitu kuja kuungana nasi kwa vitendo, tunamshukuru kwa jitihada alizozichukua kuhakikisha nduguzetu 139 ambao walikuwa hawana makazi kabisa, kuendelea kuwahudumia ambapo mpaka leo wako chini ya Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan”

“Tunawashukuru watanzania wote walioshikama, tuliwaona viongozi wa Dini, kimila, Taasisi mbalimbali wamefika na wakawashika mkono na ndiyo maana Taifa letu limepata heshima kubwa ya kupambana na majanga, kuyatatua na kurekebisha miundombinu” Alisema Makonda