November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Makinda aipongeza HKMU kwa kutoa wahitimu bora

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online, Dar

SPIKA Mstaafu, Anne Makinda amepongeza upanuzi unaofanywa na Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Hubert Kairuki (HKMU) maeneo ya Boko jijini Dar es Salaam, kwani utasaida kutoa wahudumu wengi wa sekta ya afya nchini.

Makinda ambaye kwa sasa ni Mkuu wa chuo hicho aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na wafanyakazi, walimu na wanafunzi wa chuo hicho ikiwa ni mara yake ya kwanza tangu ateuliwe kushika nafasi hiyo..

Amesema anakifahamu chuo hicho tangu kuanzishwa kwake, kwani kimekuwa kikifanya vizuri kwa kutoa wahitimu ambao wamekuwa wakifanya vizuri kwenye sekta ya afya katika maeneo mbalimbali nchini.

“Nampongeza Makamu Mkuu wa chuo kwa kutoa wahitimu bora na ambao wananidhamu sana kwa kweli huwa nakutana nao maeneo mengi wanayofanyakazi unaona kabisa huyu daktari au muuguzi amefundishwa na akafundishika. Endeleeeni kutoa huduma bora watu watawakimbilia,” amesema

Aidha, amesema amesikia changamoto ya mikopo kutoka kwa wanafunzi wa chuo hicho ambayo amesema ataifikisha kwa wahusika ili ifanyiwe kazi ili waweze kuhudumiwa kama wengine.

“Mwenyekiti wa bodi aliwahi kuyasema haya mbele yangu kwamba wanafunzi hawa wakitoka hapa wanakwenda kufanyakazi kwenye hospitali za Serikali sasa kwanini wakose mikopo, mimi nimelielewa na nitalifikisha kwa wahusika,” amesema Makinda

Mtaalamu wa maabara wa Chuo Kikuu cha Hubert Kairuki (HKMU), Walter Msangi akimweleza Mkuu wa Chuo hicho, Anne Makinda kuhusu shughuli zinazofanywa na maabara hiyo katika kufundisha wanafunzi wa chuo hicho wakati wa ziara yake chuoni hapo jana. Anayefuata ni Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Charles Mgone, Makamu Mkuu wa chuo hicho anayeshughulikia taaaluma Profesa Moshi Ntabaye na Mwenyekiti wa Baraza la chuo hicho, John Ulanga

Mwenyekiti wa Bodi ya Mtandao wa Elimu na Afya Kairuki (KHE), Kokushubira Kairuki ameiomba Serikali isiwatoze pesa wanafunzi wa chuo hicho wanapokwenda kufanya mazoezi kwa vitendo kwani mwisho wa siku wanakwenda kulitumikia taifa la Tanzania.

“Tunapata shida wanafunzi wetu wanapokwenda kufanya mazoezi kwa vitendo kwani fedha wanazotaka ni kubwa nasisi hatuwezi kuwaongezea ada wanafunzi kufidia fedha hizo tunazotozwa hivyo tunaomba wasitutoze,” amesema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la chuo hicho, John Ulanga amesema chuo kimeendelea kuongeza uwezo wa kufanya tafiti mbalimbali na kuongeza walimu wenye weledi wa hali ya juu hivyo kukifanya chuo kuendelea kuwa bora.

Amempongeza Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Charles Mgone kwa kuimarisha ubora wa ufundishaji hali inayokifanya chuo cha HKMU kuendelea kuwa miongoni mwa vhyuo vikuu bora duniani na kwamba ndiyo sababu kinapata wanafunzi wengi kutoka nje ya nchi.

“Mfano kwenye mradi wa uyoga chuo chetu kimefanya utafiti sana kwenye eneo hili kuliko mtu yeyote yule na kwenye upande wa ushauri wa kitaalamu tunafanya vizuri sana na tunaahidi kuendelea kufanya vizuri zaidi,” amesema Ulanga.