December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Makamu wa kwanza wa Rais Zanzibar ashiriki kongamano maalum la ngome ya vijana ACT-Wazalendo

Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline

MWENYEKITI wa Taifa wa ACT Wazalendo ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar,Othman Masoud Othman, leo Jumapili Aprili 21, 2024 amehudhuria, akiwa Mgeni Rasmi, katika Kongamano Maalum la Ngome ya Vijana  wa Chama hicho,katika Ukumbi wa Picca Dilly, Kombeni Mkoa wa Mjini-Magharibi, Unguja.

Kongamano hilo ambalo limebeba Maudhui ya Maadhimisho ya “Miaka Kumi (10) ya Wazalendo”, limejikita katika Mjadala juu ya Dhima na Wajibu wa Rika hilo Muhimu katika Kupigania kile kinachoitwa  “Zanzibar Mpya, Zanzibar Moja na Zanzibar yenye Mamlaka Kamili”, ambayo ni miongoni mwa Sera za sasa za ACT-Wazalendo,hafla ambayo pia imekuja  sambamba na Shamra-Shamra za Kutimia Miaka Sitini (60) ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Viongozi wa Ngazi mbali mbali wa Chama hicho, kutoka Zanzibar na Tanzania Bara wamehudhuria katika Kongamano hilo, wakiwemo Makamu Mwenyekiti wa ACT- Wazalendo Zanzibar,Ismail Jussa,Makamu Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana Taifa, Nassor Marhoun,Naibu Katibu Mkuu Mstaafu Zanzibar na Waziri wa Afya wa Zanzibar Nassor Ahmed Mazrui, Naibu Katibu Mkuu wa Vijana Taifa,Ruqayya Mahmoud Nassir, Wajumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu za Chama hicho,Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Wabunge na Mwanasheria Mkuu wa ACT-Wazalendo ambaye pia ni Waziri wa Biashara na Viwanda wa Zanzibar,Omar Said Shaaban.

Hafla hiyo ambayo imeshuhudia pia Uwasilishaji wa Mada kuhusu historia ya kuundwa kwa muungano wa Tanganyika na Zanzibar na mambo saba yanayodhoofisha Zanzibar katika muungano kutoka kwa Ismail Jussa, na  Othman mbele ya Vijana hapa Visiwani, imepambwa kwa Tumbuizo na Hamasa za Harakati tofauti, zikijumuisha Vikundi vya Burudani.

Katika Kongamano hilo, Mheshimiwa Othman ameambatana na Mke wake,Mama Zainab Kombo Shaib.