November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Makampuni Zaidi ya 11 ya Nchini Pakistani Kushiriki Maonesho ya 46 ya DITF(SabaSaba)

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Nchi ya Pakistani imethibitisha Ushiriki wa Makampuni yake zaidi ya 11 kwenye Maonesho ya 46 ya DITF(SabaSaba) kutoka Sekta mbalimbali ikiwemo Ujenzi, Vifaa Tiba, Nishati, Vifungashio, Matunda na Mbogamboga.

Hayo yamesemwa na Balozi wa Pakistani Nchini Tanzania Mhe.Mohammad Saleem tarehe 26 Mai, 2022 alipotembelea TanTrade na kuonana na Mkurugenzi Mkuu Bi.Latifa Khamis ambapo, Mhe.Balozi ameeleza kuwa Makampuni hayo yatakuja na bidhaa na teknolojia ambazo zitawasaidia Wajasiliamali na Wakulima nchini katika kuongeza ubora wa bidhaa katika kila hatua ya mnyororo wa ongezeko la thamani.

Pia amesema Makampuni hayo yatashiriki pia katika Programu mbalimbali kwenye Maonesho hayo ikiwa ni pamoja na Mikutano ya B2B na Makongamano ya Biashara.
Aliongeza kuwa hadi hivi sasa Makampuni 11 ndio yamethibisha kushiriki na Ubalozi wa Pakistani unaendelea kufuatilia Makampuni mengine kutoka Nchini humo ambayo yameonesha nia ya kushiriki kwenye Maonesho hayo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade Bi.Latifa Khamis ameishukuru Pakistani kwa kuendelea kuimarisha Diplomasia ya Uchumi kati yake na Tanzania ambapo imekuwa ikishiriki kwenye Maonesho ya DITF kwa kuleta Makampuni yenye fursa mbalimbali kwa Wajasiliamali, Wafanyabiashara na Wakulima wa Tanzania.

Pia aliipongeza Nchi ya Pakistani kwa jinsi ilivyoshirikiana na Tanzania kwenye Siku ya Tanzania kwenye Maonesho ya Expo 2020 Dubai kwa kuwaalika Wafanyabiashara wa Nchi hiyo kwenye Kongamano la Biashara na Uwekezaji liloambatana na Siku ya Tanzania.