Na Jackline Martin,TimesmajiraOnline,Dar
HALMASHAURI Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) iliyokutana jijini Dar es Salaam imemteua aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Amos Makalla, kuwa Katibu NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo Maalum wa CCM.
Makalla anachukua nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na Paul Makonda kwa takribani miezi mitano. Makonda aliteuliwa hivi karibuni kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, akichukua nafasi ya John Mongella.
Taarifa iliyotolewa jana na Chama Cha Mapinduzi, ilieleza kwamba uamuzi huo ulifikiwa jana kwenye kikao Maalum cha Halmashauri Kuu ya CCM chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.
“”Pamoja na masuala mengine, Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, imefanya mabadiliko madogo ya Sekreterieti ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kwa kuwachagua wajumbe kama ifuatavyo,” ilieleza taarifa hiyo.
Kikao hicho kilimteua John Mongella kuwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, akichukua nafasi ya Anamringi Macha ambaye ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga.
AIdha,kikao hicho kimemteua Ally Hapi kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Wazazi Tanzania, akichukua nafasi ya Gilbert Kalima ambaye ameteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mkinga.
Kwa upande Jokate Mwegelo ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM, akichukua nafasi ya Fakii Lulandala ambaye ameteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro.
Aidha katika kikao hicho, Halmashauri Kuu ya CCM Taifa imezipongeza Serikali zake zote mbili, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, chini ya Rais Dkt. Hussen Ali Mwinyi, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, kwa kazi kubwa na nzuri ya kuendelea kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2020 — 2025.
More Stories
Madaktari bingwa wa Samia watua Rukwa
Utashi wa Rais Samia na matokeo ya kujivunia vita dawa za kulevya nchini
Uwekezaji wa Rais Samia sekta ya afya waendelea kuwa lulu Afrika