Na Esther Macha,Timesmajira,Online,Chunya
IMELEEZWA kuwa wazazi na walezi Wilayani Chunya Mkoani Mbeya wamekuwa wakichangia ongozeko la vitendo vya ukatili dhidi ya watoto zaidi kutokana na kuruhusu watoto wao kuitwa majina yasiyostahili katika jamii.
Hayo yamesemwa jana na Ofisa Elimu Kata ya Bwawani katika Mamlaka ya Mji Mdogo wa Makongolosi Wilaya ya Chunya Mkoani Mbeya ,Donard Sawanga wakati wa mahafali ya tatu ya darasa la awali katika shule ya mchepuo wa Kiingereza ya Hollyland Pre and Primary School inayomilikiwa na Lawena Nsonda(Baba Mzazi).
Sawanga amesema kuwa majina yasiyostahili kwa watoto yamekuwa chanzo cha vitendo vya ubakaji na ulawiti katika jamii hivyo wazazi na walezi wana wajibu wa kuwa walinzi wa watoto wao ili kuweza kuepukana na vitendo hivyo .
“Nyie ndugu zangu wazazi msipende kukubali watoto wetu waitwe wachumba,baby na majina mengine mabaya pia kupokea zawadi kwa watu wasiowafahamu kwani watu hao hujenga mazoea na baadae kuwabaka watoto”amesema Sawanga.
Katika kukabiliana na changamoto hiyo mgeni rasmi amechangia mifuko 25 ya saruji yenye thamani ya shilingi laki tano akiungwa mkono na wazazi ambapo jumla ya shilingi 1,164,000/- zimechangwa papo hapo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shule ya Hollyland Lawena Nsonda(Baba mzazi) amesema maslahi bora kwa walimu na wafanyakazi wote ndiyo mafanikio ya shule hiyo na kiu yake ni kuanzisha pia sekondari ili watoto waendelee papo hapo na kuwafanya wawe na matokeo mazuri.
“Mikakati yangu ni kuhakikisha walimu na wafanyakazi wanakuwa iuzuri kimaslahi ili waweze kufundisha vizuri watoto hawa unajua moja ya njia ya kufanya shule ifaulishe izuri ni pamoja na kuboresha maslahi ya walimu na ndicho ninachofanya mimi ,lakini tuna mpango wa kuanzisha sekondari pia ili watoto watakaomaliza hapa waendelee kusoma hapa hapa”amesema Mkurugenzi huyo.
Awali Mwalimu Mkuu wa hiyo, Kenya Mahada amesema shule inafanya vizuri kitaaluma ambapo mtihani wa Mock darasa la nne 2021 Wilaya ya Chunya shule hiyo imeongoza kati ya shule 63 za Wilaya ya Chunya.
Aidha amebainisha baadhi ya changamoto ikiwemo uzio,madarasa na maktaba kwa mwaka ujao.
Shule ya Hollyland imezidi kukua siku hadi siku kwa kuwasogezea huduma ya elimu wakazi wa Chunya na mikoa jirani ambao walikuwa wakilazimika kuwapeleka watoto wao nje ya Wilaya ya Chunya.
More Stories
Serikali yaja na mwarobaini wa changamoto ya Kivuko Magogoni – Kigamboni
Kisarawe kukata keki ya Birthday ya Rais Samia
Wataalam wa afya wakutana kujadili ugonjwa wa Marburg