Na George Mwigulu, Katavi.
WAKALA wa Nishati Vijijini (REA) inatarajia kusambaza jumla ya majiko 9,765 ya gesi (LPG) ya kilo sita katika Mkoa wa Katavi yanayotolewa kwa bei ya ruzuku ya asilimia 50 ikiwa ni utekelezaji wa mpango mkakati wa taifa wa nishati safi ya kupikia.
Mkakati wa taifa wa nishati safi ya kupikia 2024-2034 umekuja baada ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kuongoza mkakati wa nchi za Afrika kuwawezesha wanawake kuanza kutumia nishati safi ya kupikia, ambapo hapa nchini aliuzindua ili kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati hiyo.
Mtaalam wa Jinsia na Nishati wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Dkt.Joseph Sambali akizungumza Desemba 19, 2024 ameweka wazi kuwa kwa umuhimu wa mapambano ya matumizi ya nishati chafu itokanayo na kuni na mkaa. Serikali imelipia kila jiko nusu ya gharama ambapo badala ya kuuzwa Tsh 39,000/= na sasa yatauzwa Tsh 19,500/=
Akiwa katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Amefafanua kuwa majiko ya gesi 3,255 yatagawiwa kwa kila wilaya huku akitoa wito kwa wananchi kuchangamkia fursa hiyo ambayo ni agenda muhimu inayolenga kutokomeza matumizi ya nishati chafu ambayo wataalamu wanaonya kuwa sehemu ya ongezeko la matatizo ya kiafya na uharibufu wa mazingira.
Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko akitoa mkazo kuhusu makakati huo amesema kupitia majukwaa mbalimbali tayari wamegawa mitungi 450 kwa wananchi ikiwa ni hatua za awali za kutekeleza maelekezo ya Rais.
Katika mkakati wa kugawa mitungi kwa bei ya ruzuku kwa muda wa miezi nane hadi tisa, Ametoa wito kwa wananchi wa halmashauri zote za mkoa huo kuwa majiko hayo ya ruzuku yatakapofika wanunue na kuyatumia.
Mrindoko amebainisha kuwa lengo ni kupunguza matumizi ya kuni na mkaa kwa maana ya utunzaji mazingira ambapo kama jinsi mkoa ulivyo kinara wa biashara ya hewa ukaa unaotokana na utunzaji wa misitu basi wananchi wanawajibu wa kuendelea kutuza misitu kupitia matumizi ya nishati safi.
Kiongozi huyo wa mkoa vilevile amezitaka taasisi ambazo zinahudumia wananchi zaidi ya mia moja kwamba maagizo ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan yameshatolewa na kusisitizwa na Waziri Mkuu Kasim Majaliwa ifikapo Decemba 31, 2024 zimefunge mifumo ya nishati safi ya gase ya kupikia.
“Natoa msisitizo kwa taasisi hizi kwa tarehe hiyo iliyotolewa hakikisheni mifumo hiyo mnafunga na baada ya hapo nitapita kufanya ukaguzi kama mmetekeleza kikamilifu” Amesema.
Zainab Rashidi, Mkazi wa kijiji cha Mtapenda halmashauri ya wilaya ya Nsimbo ameishukuru serikali kwa kazi nzuri ya kutoa ruzuku ya majiko hayo, ambapo anadai kuwa suluhu ya matatizo ya wanawake ya kutafuta kuni na mkaa imepatikana.
“Bei ya jiko moja ya Tsh 19,500/- kwetu ni sawa na bure. Sikuamini hadi nimekuja hapa kujipatia jiko hili” Amesema Zainab huku akisisitiza kuwa ni mwazo wa njia nzuri ya kuweza kuondokana na matendo ya kikatili waliyokuwa wakipitia wakati wa kutafuta kuni vichakani hususani ya ubakaji.
Rais Dk Samia Suluhu Hassan akiwa katika mkutano wa 28 wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya tabianchi (COP 28) Dubai aliongoza mkakati huo ambao ni wa miaka 10 huku akitaka kuwepo nguvu ya pamoja kuanzia wahisani wa kimaendeleo, taasisi za umma na sekta binafsi ili kuongeza juhudi kufikia malengo yake.
More Stories
NIDA yawakumbusha wananchi kuchukua vitambulisho vyao
Dkt.Kafumu:Uteuzi wa Rais Samia umezingatia katiba
Kliniki ya sheria bila malipo yazinduliwa Kilimanjaro