Na Penina Malundo,timesmajira, Online
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa mapambano ya kupiga vita vya matumizi ya dawa za kulevya yanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya wananchi kuwafichua wale wote wanaohusika na usafirishaji, uingizaji, uuzaji na utumiaji wa dawa za kulevya nchini.
Waziri Majaliwa ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati wa kilele cha kupinga matumizi ya dawa za kulevya kitaifa yaliyoandaliwa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA).
Amesema wananchi wengi wanawafahamu watu wanaohusika na uuzaji na usambazaji wa dawa za kulevya lakini wamekuwa hawapo tayari kuwafichua jambo linalokwamisha mapambano ya kupiga vita matumizi ya dawa hizo.
“Serikali inahitaji wahusika hao watajwe na kubainika ili kutokomeza biashara hiyo kwa lengo la kuwalinda vijana ambao ndiyo nguvu kazi ya taifa,”amesema na kuongeza
“Tunaendelea na udhibiti katika maeneo yote nchini kupitia Tume ya udhibiti dawa za kulevya kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kutokomeza hizi dawa,”amesema
Amesema wamefanikiwa kukamata dawa nyingi za mkupuo kwa kipindi kifupi na kubainisha kuwa hiyo siyo dalili nzuri.
“Aprili mwaka huu walikamata heroin kilo 174 hii siyo dalili nzuri kabisa, ni muhimu Watanzania tuungane pamoja kupambana na hawa waingizaji wa dawa za kulevya nchini,” amesema.
Aidha amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wanaopambana na dawa za kulevya wakati wote watakapokuwa wanatekeleza majukumu yao.
Kwa upande wake Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) Gerald Kusaya amesema takribani waraibu 12,329 wanatumia dawa za usaidizi wa kuacha kutumia mihadarati ‘methadone’ katika vituo 15 vilivyopo nchini.
Amesema tangu kuanza kwa huduma hiyo miaka mitano iliyopita huduma hiyo imetanuka kutoka vituo vitatu vilivyokuwepo jijini Dar es Salaam vilivyohudumia wagonjwa 443 mpaka kufikia vituo 15 vilivyopo katika mikoa 11.
More Stories
Mama Zainab:Watoto yatima ni jukumu la jamii yote
DC Korogwe awataka viongozi wa vijiji kuwatumikia wananchi kwa uadilifu
Premier Bet yamtangaza mshindi mkubwa