Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Katavi
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amekagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa bandari ya Karema na kusema kwamba ameridhishwa na ubora na hatua iliyofikiwa
Ameyasema hayo jana baada ya kukagua mradi huo unaojengwa katika kata ya Karema wilaya ya Tanganyika Mkoani Katavi.
Waziri Mkuu amesema Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan amedhamiria kwa dhati kuhakikisha miradi yote inayoendelea na mingine inayo anza inakamilika kwa wakati.
Amesema mradi huo ambao utakuwa ni kiunganishi cha usafirishaji wa mizigo na abiria katika bandari hiyo na bandari ya Karemie iliyoko Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
“Nimefurahi kusikia mradi huu umefikia asilimia 50 na ifikapo Machi mwakani utakuwa umekamilika na tayari kwa matumizi, hivyo nawaomba wananchi mchangamkie fursa ya uwepo wa mradi huu.”
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) Erick Hamiss amesema ujenzi wa mradi wa bandari ya Karema umefikia asilimia 50 ya utekelezaji.
Amesema ujenzi wa mradi huo wenye thamani ya shilingi bilioni 47.97 ulianza Agosti, 2019 na unatarajiwa kukamilika Machi, 2022. Mradi huo umeajiri watu 300 kati yake raia wa kigeni ni tisa tu.
“Mradi huu ni kichocheo cha ukuaji wa uchumi nchini hususan katika maeneo ya ukanda wa Ziwa Tanganyika na nchi jirani za Zambia, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.”
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko amesema mkoa umejipanga kuzitumia vizuri fursa zitokanazo na ujenzi wa mradi huo kwa ajili ya kukuza uchumi.
More Stories
Walimu elimu ya lazima watatakiwa kuwa wabobezi kwenye masomo wanayofundisha
Wahakikishiwa usalama siku ya kupiga kura
CCM inabebwa na kazi nzuri za Rais Dkt. Samia-Makalla