Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline,Chunya
WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema dhamira ya serikali kuongeza thamani ya madini yanayochimbwa nchini, imeendelea kutekelezwa kwa vitendo baada ya uzinduzi wa kiwanda cha uchenjuaji madini ya shaba ambacho ni cha kwanza nchini.
Amesema kiwanda hicho cha Mineral Access Systems Tanzania Ltd (MAST) cha kuchenjua madini hayo kwa teknolojia ya Kisasa, kimeiweka Wilaya ya Chunya katika ramani ya dunia kama mzalishaji wa madini.

Akizindua kiwanda hicho wilayani Chunya mkoani Mbeya Juni 18,2025 Majaliwa amesema ujenzi wa kiwanda hicho ni uthibitisho wa vitendo na dhamira ya serikali ya kuongeza thamani madini hapa nchini.
“Uwekezaji huo mkubwa kutoka kwa kampuni ya MAST ni ushahidi wa kuimarika kwa mazingira ya biashara na uwekezaji nchini,” alieleza.
Aidha Majaliwa amesema kuwa kiwanda hicho kinaendana kikamilifu na matakwa ya Sera ya Madini, kwa kuleta mapinduzi katika kuhamasisha uongezaji thamani ndani ya nchi, kuhamasisha matumizi ya teknolojia ya kisasa, pamoja na kuhifadhi mazingira katika maeneo ya shughuli za madini.
“Hii ni hatua ya msingi katika kuifanya Tanzania isiwe tu nchi ya kuchimba madini bali pia kuwa nchi ya viwanda vya kuongeza thamani ya madini na kutengeneza bidhaa zenye thamani kubwa zinazotokana na madini,”amesisitiza Majaliwa.

Vilevile amesema msisitizo mkubwa umewekwa katika kuhakikisha kuwa madini yote yanayochimbwa nchini yanaongezewa thamani ndani ya nchi na kuwa hatua hiyo inalenga kuongeza ajira, mapato ya serikali kupitia kodi na tozo mbalimbali, na kuendeleza viwanda vya ndani vinavyotegemea malighafi ya madini, hivyo kulifanya taifa kuwa na uchumi shindani kimataifa.
Kutokana na hayo aliagiza shughuli zote za uchimbaji wa madini zitekelezwe kwa kuzingatia utunzaji wa mazingira kwa kujumuisha matumizi ya teknolojia rafiki, urejeshaji wa maeneo baada ya uchimbaji, na kuzuia uchafuzi wa mazingira ili kulinda maisha ya watu, vyanzo vya maji na viumbe hai.
Katika kulinda maslahi ya jamii zinazozunguka migodi, Majaliwa alisisitiza kuwa wawekezaji waajiri wakazi wa maeneo hayo kwa nafasi zisizohitaji ujuzi maalum. Hii itasaidia kupunguza ukosefu wa ajira na kuongeza kipato kwa wananchi wa maeneo ya miradi.

Pamoja na hayo Waziri Mkuu amesema kuwa wawekezaji wote wanapaswa kulipa tozo na ushuru wa serikali ikiwemo mrabaha. Utii wa masharti haya ni muhimu kwa Serikali kupata mapato ya kugharamia huduma za kijamii kama elimu, afya, na miundombinu.
Pia ameziagiza kuwa kampuni zote zitekeleze wajibu wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) kwa kuhakikisha jamii zinazozunguka maeneo ya miradi zinanufaika na huduma kama vile shule, barabara, zahanati au maji safi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa MAST, Godfrey Kente, alisema kuwa lengo la kuanzishwa kwa kiwanda hicho ni kuchenjua mashapo ya madini ya shaba yenye kiwango cha chini asilimia 0.5 hadi asilimia mbili kutoka eneo la Mbugani, Chunya na kuyapandisha thamani hadi kufikia kiwango cha asilimia 75 ya shaba kupitia teknolojia ya kisasa.

Ameeleza kuwa kwa sasa kiwanda hicho kina uwezo wa kuchakata tani 31,200 za mashapo ya shaba kwa mwezi, ambapo tani 27,200 zinatoka kwenye mgodi wa kampuni hiyo na tani 4,000 zitanunuliwa kutoka kwa wachimbaji wadogo nchini.
Kente ameeleza kuwa MAST inatarajia kujenga viwanda vingine vitatu vya kuchenjua madini ya shaba katika mikoa ya Manyara–Simanjiro, Ruvuma–Mbesa (Tunduru) na Dodoma, ambapo kila kiwanda kitapata wafanyakazi zaidi ya 500 na kuchangia kwa athari za kiuchumi zenye thamani ya zaidi ya USD milioni 40 kwa mwaka.
“Tayari kiwanda hiki kimetoa ajira kwa wafanyakazi 254, wakiwemo 209 waliopo moja kwa moja chini ya MAST na 45 kupitia wakandarasi. Kati yao, Watanzania 205 wamenufaika moja kwa moja, ambapo takribani asilimia 60 wanatoka Mkoa wa Mbeya, hususan Wilaya ya Chunya,”amesema Kente.

Aliongeza kuwa MAST ni kampuni ya Kitanzania iliyoanzishwa mwaka 2011, ikiwa na dhamira ya kuendeleza biashara ya madini kwa njia jumuishi na endelevu, na kwamba imekuwa ikishiriki katika biashara ya madini ya kimkakati kama shaba, nikeli na manganese ndani na nje ya nchi kwa kushirikiana na wachimbaji wadogo.
Awali, akimkaribisha Waziri Mkuu, Naibu Waziri wa Madini Dkt.Steven Kiruswa, alisema kuwa Ilani ya CCM ya 2020 – 2025 imeelekeza ujenzi wa viwanda vya kuongeza thamani ya madini nchini, kama mkakati wa kuifanya Tanzania isiwe mzalishaji tu wa malighafi bali pia mzalishaji wa bidhaa zenye thamani kubwa.
Dkt.Kiruswa ameeleza kuwa kiwanda cha MAST ni miongoni mwa viwanda tisa vinavyotarajiwa kujengwa nchini kwa ajili ya kuongeza thamani ya madini muhimu.
“Juhudi hizi ni sehemu ya mpango wa taifa wa kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha uchakataji wa madini barani Afrika, na kuongeza uwezo wa kuuza bidhaa zilizoongezwa thamani badala ya malighafi,”amebainisha.




More Stories
Mfanyabiashara,vibarua mbaroni wakituhumiwa kuchimba mahandakiÂ
Silinde azindua baraza la sita la Wafanyakazi Tume ya Taifa ya Umwagiliaji
NMB ilivyosaidia Serikali kukusanya zaidi ya Sh trilioni 9.8