Na Mwandishi Wetu, Dodoma
MWENYEKITI wa CCM, Rais John Magufuli amekutana na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Dkt. Ali Mohamed Shein katika kikao cha ndani kilichofanyika Ikulu, Chamwino Mkoani Dodoma na kuzungumzia masuala mbalimbali kuhusu CCM.
Kikao hicho ambacho kilifanyika jana kilihudhuriwa na Makamu Mwenyekiti CCM Bara, Philip Mangula na Katibu Mkuu wa CCM, Bashiru Ally.
Baada ya kikao hicho, Rais Shein alikwenda kuweka udongo katika jiwe la msingi la ujenzi wa Ofisi za Ikulu na kukagua maendeleo ya kazi ya ujenzi wa ofisi hizo inayofanywa na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kupitia shirika lake la Suma JKT.
Rais Shein alimshukuru, Rais Magufuli kwa kumpa fursa ya kwenda kuweka udongo ikiwa ni kumbukumbu ya ujenzi wa ofisi hizo na amebainisha kuwa kujengwa kwa ofisi hiyo ni heshima kwa Taifa na tafsiri sahihi ya kujitawala.
“Huko ndio kujitawala, kutawaliwa sio kuzuri, mtawala anafanya anavyotaka yeye, anafanya kwa utashi wake pale anapotaka yeye kufanya, tunapochukua hatua ya kujitawala wenyewe tunafanya mambo makubwa kama haya kwa ajili ya wananchi, hii ofisi ni ya wananchi wa Tanzania,” amesema Rais Shein.
Rais Shein aliwasalimu vijana wa JKT wanaofanya kazi za ujenzi wa ofisi hizo, amewapongeza kwa kazi nzuri wanayoifanya na amewataka kujivunia fursa hiyo adhimu ya kujenga ofisi ya Ikulu za nchi yao, badala ya kazi hiyo kufanywa na kampuni za nje ya nchi kama ambavyo hufanyika katika maeneo mengi.
More Stories
Amos Lengael Nnko afariki kwa ajali ya gari
Gridi za Tanzania, Kenya kuimarisha upatikanaji wa umeme
Mama Zainab:Watoto yatima ni jukumu la jamii yote