May 13, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Magufuli atoa ya moyoni kuhusu Kigogo wa zamani wa Chadema

Na Penina Malundo,TimesMajira ,Online

MGOMBEA Urais kupitia Chama cha Mapinduzi CCM,John Magufuli amefichua siri jinsi alivyomfahamu aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA na Mbunge wa Jimbo la Karatu  Balozi Dkt.Willibroad  Slaa kwa jinsi alivyokuwa tofauti na wapinzani wengine.

Balozi Dkt.Slaa alihama Chadema wakati  vuguvugu la uchaguzi mkuu wa mwaka 2015,baada ya kutoridhishwa na uamuzi wa Chama hicho kikiungana  na vyama vilivyokuwa vikiunda UKAWA kumpitisha Waziri Mkuu Mstaafu Edward Lowassa kuwa Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano .

Mbali na Chadema vyama vingine vilikuwa ni Chama cha Wananchi CUF,NCCR Mageuzi na NLD.

Akizungumza hayo leo, jimboni  karatu mkoani Arusha kwaajili ya kuomba kura kwa wananchi,Magufuli amesema Balozi Dkt.Slaa alikuwa ni tofauti na wapinzani wengi  kwa jinsi  alivyokuwa mtu makini,mwenye kujenga hoja na alikuwa mwakilishi mzuri wa wananchi wa jimboni kwake.

Magufuli amesema kwake yeye  kama kuna mtu mmoja kwenye vyama vya upinzani ambaye anaweza akasema huyu ni kweli alikuwa Mpinzani kwaajili ya watu ,Mzalendo wa kweli na  Muadilifu ni Balozi,Dkt Slaa.

Balozi Dkt.Slaa alikuwa na uwezo mkubwa wa kujenga hoja ,kuchagua maneno ya kuzungumza,muadilifu na mzalendo wa kweli .

Amesema kwa kutambua uwezo na kuamini kuwa  kuna mpinzani mmoja kati ya wapinzani wote waliopo Tanzania wa kweli aliamua kumteua Balozi Dkt.Slaa kuwa balozi wa nchi Tisa.

 “Wakati alipotaka kuja kuomba ubunge huku (karatu)aliomba nafasi hiyo kupitia Chama cha Mapinduzi kwasababu yeye alikuwa mwanaccm,Chama cha mapinduzi hapa karatu wakamfanyizia figisu hawakulirudisha jina lake ndipo akaamua kwenda mageuzi,”amesema na kuongeza

“Balozi Dkt.Slaa baada ya kukaa upinzani na kuona ubabaishaji kwenye Chama hicho aliamua kujitoa katika Chama hicho,”amesema

Amesema hata alipokuwa bungeni alivyochaguliwa alikuwa mtu makini,mwenye kujenga hoja,anawakilisha mawazo ya wananchi waliokuwa chini,hali hiyo iliwafanya hata watu waliokuwa CCM kumpenda katika kipindi chake.

 “Inawezekana namna alivyo ilitokana na kazi yake aliyofanya ya Upadri na kuwa Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Tanzania…kwangu Mimi kama kuna mtu mmoja kwenye vyama vya upinzani ambaye anaweza akasema huyu ni kweli alikuwa kwaajili ya watu basi ni Balozi Dkt.Slaa,”amesema na kuongeza

 “Dkt.Slaa alikuwa mstaarabu tofauti na wapinzani tunaowaona leo ambao  wakiingia bungeni hawajengi hoja,Mkitangaza bajeti kwaajili ya wananchi wa karatu na maeneo mengine wao hawawasapoti,mkijadili bajeti kwaajili ya maendeleo ya wananchi wao wanatoka nje siku nyingine wanaweka plasta midomoni,”amesema

Amesema katika maisha yake yote alivyokuwa Mbunge hakuwahi kumuona Balozi Dkt.Slaa akiweka plasta katika mdomo akiwa bungeni.

“…Ndio maana nasema kwa ukweli kutokana na uwezo mkubwa wa mwanamapinduzi wa Dkt.Slaa na kutokana na upendo alionao kwa wananchi bila kubagua vyama niliamua kumteua kuwa balozi kuwakilisha Tanzania katika nchi tisa.

 ***Akizungumzia Jimbo la Karatu

Magufuli amesema katika  sekta ya afya  zimejengwa hospitali mbili, kituo cha afya Karatu kimepanuliwa na kujengwa wodi ya wanawake na wanaume, Bajeti ya dawa imeongezwa kutoka milioni 131 hadi milioni 450 utolewa kila mwaka.

Pia, amesema sh. bilioni 7.4 zimetumika kugharamia elimu ya msingi mpaka sekondari, ujenzi wa madarasa 208, ununuzi wa madawati 4886 huku nyumba za walimu 84 zikijengwa.

Magufuli amesema suala la  umeme takribani vijiji 47 vimewekwa umeme na  kubaki  vijiji 10 ambapo atakapochaguliwa ndani ya miaka miwili watamaliza vijiji hivyo vilivyobaki..

Aidha amewahidi wana Karatu kuwatatulia changamoto mbalimbali zilizopo eneo hilo ikiwemo ya gharama kubwa za maji ambapo wananchi wanatozwa uniti moja kwa sh. 3000 badala ya 700 na upanuzi wa kituo cha afya Karatu mjini.