May 16, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Magonjwa ya mifugo changamoto kwa wafugaji kuku, ng’ombe

Na Esther Macha,Timesmajira, Online, Mbeya

Imeelezwa kuwa changamoto ya wafugaji wa kuku na ng’ombe kushindwa kudhibiti magonjwa ya mifugo kunachangia mifugo hiyo kuwa na uzalishaji hafifu wa maziwa na mayai.

Hayo yamebainishwa na Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania(TVLA) Dkt. Stella Bitanyi
wakati walipotembelewa na Waziri Mkuu mstaafu Mizengo Pinda,katika banda lao kwa ajili ya kujione shughuli zinazofanywa na wakala hao ambao wapo kwenye maonesho ya wakulima Nane Nane yanayofanyika kitaifa katika viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya.

Dkt Stella amesema kuwa changamoto kubwa ambayo imekuwa ikizungumziwa zaidi na wafugaji wanaotembelea banda lao ni ya magonjwa ya mifugo yao ya ng’ombe na kuku ambayo wanashindwa kudhibiti hivyo kuendelea kuwa na uzalishaji hafifu.

“Wafugaji wengi waliotufikia hapa kwenye banda letu ni wafugaji wa kuku na ng’ombe kwa hiyo wanakuwa na uzalishaji hafifu, tunawapa ushauri kwenye matumizi sahihi ya dawa,magonjwa na udhibiti wa magonjwa,”amesema Dkt.Stella

Pia amesema kwamba wamekuwa wakiifanya kazi mbalimbali ikiwemo kufanya uchunguzi magonjwa ya mifugo,kuzalisha chanjo za mifugo pamoja na tafiti zake,kufanya uthibiti na ubora wa vyakula vya mifugo pamoja na kufanya tafiti mbalimbali za magonjwa ya mifugo

Hata hivyo amesema kuwa wanawafikia wafugaji kwa kiwango kikubwa kwani wana vituo 13 nchi nzima ambavyo vinafanya kazi ya kuwafikia wakulima wote na wafugaji pamoja na kutoa mafunzo kwa makundi hayo.

“Watalaam wetu wamekuwa wakifika kwenye mashamba kutoa elimu na kuchukua sampuli na kupima magonjwa na kuonesha hali ya ugonjwa uliopo,”amesema.