October 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mafuta yapanda baada ya miezi mitatu

Na Mwandishi Wetu    

SERIKALI imesema inaweka mkazo katika kuhakikisha bidhaa za mafuta zinaendelea kupatikana  hapa nchini kwa uhakika, na kwa bei himilivu, licha ya mabadiliko ya bei katika soko la dunia yanayoendelea kuathiri bei za ndani.

Serikali imechukua hatua hizo kutokana na mwenendo wa bei za mafuta hapa nchini kuendelea kuathiriwa na mgogoro wa kisiasa katika eneo la Mashariki ya Kati, ambako Tanzania ununua sehemu kubwa ya bidhaa zake za mafuta, ambao uliibuka upya na kuathiri uzalishaji, upatikanaji na usafirishaji wa mafuta duniani.

Hali hiyo ilisababisha kupanda kwa bei za bidhaa za mafuta yaliyosafishwa katika soko la dunia.Kutokana na mwenendo huo, bei za petroli, dizeli na mafuta ya taa  hapa nchini kwa mwezi Oktoba 2026 zimeongezeka ikilinganishwa na Septemba 2026,ambapo sasa bei hizo zimepanda  baada ya kushuka kwa miezi mitatu mfululizo.

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji(EWURA), kama ilivyo wajibu wake, imetangaza bei kikomo za bidhaa za mafuta ya petroli zitakazotumika  hapa nchini kuanzia leo Jumatano ya Oktoba 7, 2026, saa 6:01 usiku.

Mwezi Oktoba 2026, katika Mkoa wa Dar-es-Salaam, bei kikomo ya rejareja ni sh.4,057 kwa lita ya petroli, sh.4,086 kwa lita ya dizeli na sh. 4,067 kwa lita ya mafuta ya taa.

Kwa Mkoa wa  Tanga, bei kikomo ya rejareja ni sh.4,123 kwa lita ya petroli, sh.4,152 kwa lita ya dizeli na sh.4,133 kwa lita ya mafuta ya taa.

Na kwa Mkoa wa Mtwara, bei kikomo ya rejareja ni sh.4,170 kwa lita ya petroli, sh.4,199 kwa lita ya dizeli na sh. 4,180 kwa lita ya mafuta ya taa. 

Taarifa hiyo iliyotolewa  imewakumbusha wananchi kuchukua risiti baada ya kununua mafuta kwenye vituo ili kuwa na ushahidi wa ununuzi huo.