Na Mwandishi Wetu,Tabora
KATIKA kuadhimisha Wiki ya Huduma kwa Wateja, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Kanda ya Magharibi, leo, tarehe 6/10/2026, imekutana na wanachama wa Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) kwa mkoa wa Tabora, na kuwaelimisha kuhusu haki na wajibu wao katika huduma za nishati na maji.
Wanachama hao pia wamepata elimu kuhusu utaratibu wa kuwasilisha malalamiko na namna yanavyoshughulikiwa, kanuni za ubora wa huduma ya maji, matumizi sahihi na salama ya gesi ya kupikia na umuhimu mikataba ya huduma kwa wateja huku wakisisitizwa kutumia mafundi umeme wenye leseni zilizotolewa na EWURA.
Meneja wa EWURA Kanda ya Magharibi, Mha. Karim Ally, akifungua warsha hiyo iliyofanyika katika Ofisi za EWURA Kanda ya Magharibi, mjini Tabora, ameeleza kuwa ni utaratibu wa Mamlaka kukutana na wadau mbalimbali ikiwemo watu wenye ulemavu ili kuwaelimisha kuhusu udhibiti sanjari na kupokea mrejesho kuhusu huduma zinazodhibitiwa.
Aidha, washiriki wameiomba EWURA kuendeleza elimu hiyo kwa kuwafikia wanachama wa SHIVYAWATA katika maeneo mbalimbali nchini na pia kwa makundi mengine ya aina hiyo ili kuimarisha uelewa wao katika masuala ya kiudhibiti.

More Stories
Zungu achaguliwa kuwa Rais wa Mkutano wa 153 wa IPU
Dkt.Homera azindua mkataba mpya wa huduma TANESCO
Dkt.Homera aitaka TANESCO kuboresha kasi ya huduma