May 17, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wakazi wa mjini wa Uvira wakipambana kuokoa maisha na vitu mbalimbali baada ya mto Mulongwe kujaa maji na kuingia katika makazi ya watu

Mafuriko yaathiri maelfu ya watu

GENEVA, Zaidi ya watu 80,000 wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wanatarajiwa kupatiwa misaada ya kibinadamu baada ya kuathiriwa na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa zinazoiendelea kunyesha.

Hayo yalibainishwa na Msemaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR), Andrej Mahecic wakati akizungumza na waaandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi.

Alisema, UNHCR inashirikiana na mamlaka pamoja na wadau nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kutoa msaada kwa watu 80,000 ambao wameathiriwa na mafuriko makubwa katika jimbo la Kivu Kusini.

Alieleza kuwa, mvua kubwa katika mji wa Uvira kwenye jimbo la Kivu Kusini pamoja na maeneo jirani na mji huo, ilinyesha kati ya Alhamisi na Jumamosi iliyopita na kusababisha mafuriko kuyakumba maeneo yaliyo na watu wengi katika mji na vijini vinavyozunguka eneo hilo ambavyo pia vinawahifadhi watu waliofurushwa makwao, wakiwemo wakimbizi.

Taarifa zinaonesha mafuriko yameharibu zaidi ya nyumba 15,000 huku tathimini ikiendelea ingawa tayari ni dhahiri hali hii imeongeza ugumu katika eneo ambalo tayari limeathiriwa na kukosekana kwa usalama na migogoro.

“Hali inayoendelea itaongeza hofu ya wakazi ambao tayari wanakabiliwa na adui mwingine, janga la virusi vya corona,”alisema.

Taarifa za awali zilieleza kuwa,zaidi ya watu 25 wamefariki dunia kutokana na mafuriko hayo na zaidi ya watu wengine 40 walijeruhiwa huku ikihofiwa kuwa wengine wengi huenda wamesombwa na mafuriko.

Kiliniki moja katika moja ya viunga vya Uvira kimesambaratishwa na maji na pia maeneo ya kujisafi katika mji ulio na watu wengi nayo yamesambaratishwa.

UNHCR inaharakisha kupeleka misaada kutoka katika ghala lake la Uvira yakiwemo mahema kwa ajili ya makazi, magodoro, ndoo na vyandarua.

ìTutakuwa tunatoa vifaa vya makazi zaidi katika siku zijazo kusaidia kupunguza mateso ya baadhi ya watu ambao nyumba zao zimesambaratishwa. Wakuu wa serikali za mitaa na mkoa wanaongoza majibu kwa msaada kutoka kwa MONUSCO,”alisema.