December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mafunzo wasaidizi wa Kisheria sasa kuanzia ngazi ya Cheti

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

TAASISI ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania inatarajia kuanza kutoa mafunzo ya wasaidizi wa kisheria ngazi ya cheti kwa lengo la kuwajengea uwezo zaidi katika masuala ya kisheria .

Aidha,  taasisi hiyo ipo kwenye mchakato wa kuandaa mtaala wa diploma ambapo mwanafunzi atakapomaliza mafunzo ngazi ya cheti ataweza kuendelea mbele kwa ngazi ya diploma.

Hayo yamesemwa jijini hapa na Afisa Habari,Elimu na Mawasiliano wa Taasisi hiyo Scholastica Njozi wakati Akizungumza na waandishi habari kwenye maonyesho ya wiki ya sheria ambayo kilele chake kinatarajiwa kuwa Februar Mosi mwaka huu mkoani humo.

Njozi amesema mafunzo yatakayotolewa na Taasisi hiyo yatakuwa na ubora ambao utamuwezesha mwanafunzi kufanya kazi kama msaidizi kisheria au kuendelea mbele kimasomo ngazi ya diploma au shahada iwapo atapenda kufanya hivyo ambapo cheti hicho kitakuwa kinatolewa na kutambuliwa na NACTE.

Amesema mafunzo ya wasaidizi wa kisheria ngazi ya cheti yatatolewa kwa muda wa mwaka mmoja na yatatolewa kwa nadharia na vitendo.

Afisa Habari wa Taasisi hiyo amesema, mafunzo hayo yataanza kutolewa Septemba mwaka huu huku akisema kwa Sasa wanasubiria kupata ithibati na usajili kutoka Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi( NACTE).

Kuhusu sifa za kujiunga na mafunzo hayo amesema ni mtu yeyote aliyehitimu elimu ya kidato cha nne na kuendelea na mwenye ufaulu wa alama D kwenye masomo manne ya kidato cha nne likiwemo somo la Kiingereza.

Sheria ya Msaada wa Kisheria ya mwaka 2017 pamoja na mambo mengine inaelekeza kuwa mafunzo ya wasaidizi wa kisheria yatatolewa katika ngazi mbalimbali na kwa kufuata utaratibu ulioainishwa ndani ya sheria ambapo ngazi za mafunzo zitakuwa ni mafunzo ya muda mfupi miezi mitatu mpaka sita, mafunzo ya ngazi ya cheti na mafunzo ngazi ya diploma.

Njozi ametumia nafasi hiyo kuwaasa watanzania  wenye  sifa  kujiunga pindi watakapofungua dirisha la udahili .

“Mafunzo yatatolewa kwa mwaka mmoja ….., miezi mitano wanafunzi watajifunza wakiwa darasani na miezi mitano  mingine, watajifunza wakiwa sehemu za kazi kwenye taasisi zinazotoa msaada wa kisheria.”alisema na kuongeza kuwa 

” Taasisi inajivunia kuwa ndio taasisi ya kwanza kutoa mafunzo haya kwa ngazi ya cheti…,hivyo wananchi hii ni fursa kwenu mjitokeze ili kupata mafunzo haya.”