June 18, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Maelekezo ya Samia yavunja rekodi TRA

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online,Dar

MAELEKEZO ya Rais Samia Suluhu Hassan na miongozo ya Serikali juu ya namna bora ya kukusanya mapato bila matumizi ya nguvu ni miongoni mwasababu zilizoiwezesha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kukusanya sh. trilioni 12.4 katika nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha 2022/2023.

Aidha makusanyo ya Desemba, 2022 yamevunja rekodi tangu kuanzishwa kwa mamlaka hiyo mwaka 1996.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TRA na kusainiwa na Kamishna Mkuu, Alphayo Kidata, jana makusanyo hayo ni sawa na ongezeko la sh. trilioni 1.35 ikilinganishwa na sh. trilioni 11.11 iliyokusanywa kipindi kama hicho Mwaka wa Fedha 2021/22.

Baadhi ya wafanyabiashara waliozungumzia na gazeti hili mara baada ya TRA kutoa taarifa inaoonesha kuvuka lengo la ukusanyaji mapato, wamesema matokeo hayo ni matunda ya maelekezo ya Rais Samia kwa TRA.

Mfanyabiashara Abdul Shamban, alisema uamuzi wa Rais kupiga marufuku TRA kuwadai kodi za miaka ya nyuma wafanyabiashara na kuwataka kuwa makini na namna wanavyosimamia ukusanyaji wa kodi ni moja na sababu ya makusanyo hayo.

Akizungumza na wananchi wa Mkoa wa Kagera katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Kaitaba, Rais Samia alisema wafanyabiashara wasisumbuliwe kwa madeni ya miaka ya nyuma, bali waachwe wafanye biashara.

“Naweza kuwaelewa kama mtadai kodi ya mwaka mmoja nyuma, lakini sio miaka ya nyuma ambayo inawezekana uzembe ulikuwa kwenu nyie ambao mlishindwa kuweka vizuri mahesabu yenu,” alisema Rais Samia.

Hata hivyo amewataka wafanyabiashara kulipa kodi kwa mujibu wa sheria na kuitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania kusimamia vema ukusanyaji wa mapato.

TRA imekusanya sh. trilioni 12.4 katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha 2022/23 yaani Julai hadi Desemba 2022.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya TRA, Makusanyo hayo ni sawa na asilimia 99 ya lengo la makusanyo ya sh. trilioni 12.48.

“Ongezeko hili ni sawa na ukuaji wa makusanyo wa asilimia 12.2,” ilieleza taarifa hiyo. Hata hivyo, katika kipindi cha Desemba 2022, TRA imefanikiwa kukusanya sh. trilioni 2.77 kati ya lengo la kukusanya sh. trilioni 2.60.

Makusanyo hayo ya Desemba 2022 yanatajwa kuwa na ufanisi wa asilimia 106.5, sawa na ukuaji wa asilimia 10.3 ukilinganisha na makusanyo ya Desemba 2021

“Pamoja na makusanyo haya kuvuka lengo la Desemba 2022, ndicho kiwango cha juu zaidi kukusanywa kwa mwezi tangu kuanzishwa kwa mamlaka mwaka 1996.

“Tunaendelea kuwashukuru walipakodi nia wadau wetu mbalimbali kwa kujitoa kwenu katika kipindi cha nusu mwaka ambapo mwenendo wa ulipaji kodi kwa hiari na uhusiano baina ya mamlaka na walipakodi umeendelea kuimarika kwa kiwango cha kuridhisha.

Pamoja na mafanikio hayo, TRA imesema inaendelea kufanyia kazi malekezo na miongozo ya Serikali juu ya namna bora ya kukusanya mapato bila matumizi ya nguvu na hivyo kuendelea kujenga mazingira wezeshi ya uwekezaji ya ufanyaji biashara nchini.

“Pia Serikali imeendelea kuisaidia Mamlaka katika ujenzi na matumizi ya mifumo inayochangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa ufanisi katika utendaji kazi wetu.

Vilevile, TRA inaeleza kwamba itaendelea kuboresha huduma kwa Walipakodi kwa kuzingatia dhana ya uadilifu, weledi na uwajibikaji ili kujenga taswira yenye kuaminika katika jamii

“Pamoja na mafanikio tuliyoyapata, bado upo umuhimu wa kuongeza kiwango cha makusanyo kwa kuinua kiwango cha ulipaji kodi kwa hiari kwa walipakodi ili kuiwezesha Serikali kuongeza wigo wa utoaji huduma kwa wananchi wote kama vile ulinzi, miundombinu ya barabara, huduma za kijamii zikiwemo elimu, afya, maji, umeme,” amesema Kidata katika taarifa yake.

***Wachumi: Rekodi itazidi kuvunjwa

Kufuatia rekodi hiyo iliyovunjwa na TRA katika ukusanyaji mapato, wataalam wa masuala ya uchumi wamesema rekodi hiyo itazidi kuvunjwa kutokana na dhamira ya Serikali ya Rais Samia kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji.

Mfano, wanasema dhamira nzuri ya Rais Samia imezidi kufikiwa kwa kiwango cha kuvunja rekodi ambapo kati ya Julai na Novemba, mwaka jana (2022) Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimesajili miradi ya uwekezaji 132 yenye kiwango cha thamani ya USD bilioni 3.16.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, John Mnali alisema wiki iliyopita, kuwa miradi hiyo imeongezeka kwa asilimia 259 ikilinganishwa na thamani ya miradi (USD milioni 881) iliyosajiliwa katika kipindi cha Julai – Novemba 2021.

Mnali alisema sababu za ongezeko kubwa la miradi iliyosajiliwa na TIC linatokana na jitihada za Serikali za kutangaza fursa mbalimbali za Uwekezaji zilizoko hapa nchini kupitia ziara mbalimbali za viongozi wa kitaifa nje ya nchi pamoja na juhudi za Serikali katika kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini.

Mtaalamu wa masuala ya uchumi, Anna Paul, akizungumzia mafanikio hayo yaliyopatina, alisema mwaka huu, 2022 Rais Samia amefanikiwa kwa kiwango cha juu kuifungua nchi na kuonekana ni sehemu salama kwa uwekezaji na kuvutia watalii.

Alisema kilichowaletea utulivu wafanyabiasha na wawekezaji wengi kujitokeza kuwekeza nchini ni pamoja na hotuba ya Rais Samia aliyoitoa mwaka 2021 mara baada ya kuwaapisha makatibu wakuu wa wizara mbalimbali na manaibu wao.

Katika hotuba yake hiyo, Rais Samia alisema licha ya Tanzania kutangazwa kuingia kwenye uchumi wa kati, hali ya kiuchumi bado ni ngumu kutokana na wawekezaji wengi kuamua kuhamisha biashara zao katika mataifa mengine kufuatia kile alichokitaja kuwa ni urasimu na unyanyasaji wa baadhi ya watendaji Serikalini.

Rais Samia alisisitiza kuwa Tanzania inawahitaji zaidi wawekezaji kuliko wao wanavyohitaji kuwekaza katika nchi hii.

Rais Samia aliitaka ofisi ya waziri mkuu, kuhakikisha wanaondoa urasimu katika mchakato wa kutolewa kwa vibali vya kazi kwa wawekezaji na kuwataka kuacha mara moja kuwalazimisha wawekezaji kuajiri wafanyakazi wa kitanzania kwani wanao uhuru wa kuchagua wa kufanya nao kazi.

Paul alisema mwaka 2022 Serikali ya awamu ya sita imefanikiwa kuifungua nchi hasa kwa kukaribisha wawekezaji, jambo ambalo linakaribisha mitaji.

“Nimewasikia TIC wakisema wamesajili miradi ya uwekezaji ya dola bilioni 3.16, hili sio jambo dogo ndani ya miezi mitano, sasa hivi badala ya wawekezaji kutukimbia, wanamiminika nchini,” alisema Paul na kuongeza kwamba uwekezaji huu unakuja kuwezesha TRA kupata mapato mengi zaidi, Rais Samia anastahili pongezi kwa hilo.

“Ukiifungua nchi, umefungua mitaji na wawekezaji katika eneo fulani, mfano Royal Tour. Ukikuza utalii unakuza ulaji wa vyakula mbalimbali vya ndani pamoja na kuongeza fedha za kigeni,” alisema

Alisema mwaka 2020 Tanzania ilipokea uwekezaji kutoka nje wa Dola za Marekani bilioni moja, lakini kwa Julai na Novemba 2022 imesajiliwa miradi ya uwekezaji yenye thamani ya Dola la Kimarekani bilioni 3.16 na kwamba hayo ni mafanikio makubwa kwa nchi, kwani nchi itapata kodi ambayo itasaidia kuwaletea maendeleo wananchi.

“Hili limefanikiwa kutokana na juhudi za makusudi zinazochukuliwa na Serikali katika kuimarisha mazingira ya uwekezaji,” alisema Paul.