Na Stephano Mango,TimesMajira Online,Songea
MADIWANI Wateule nane wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Mkoa wa Ruvuma, wamejitokeza kuchukua fomu za kuwania kuteuliwa na vikao vya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kugombea nafasi ya Umeya wa manispaa hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Kaimu Katibu wa CCM wa Wilaya ya Songea Mjini, Rehema Hussein alisema chama hicho kimefungua milango wazi kwa Madiwani Wateule kuchukua fomu za kuwania nafasi ya Umeya na nafasi ya Unaibu Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea.
Rehema ambaye pia ni Katibu wa Jumuiya ya Wanawake (UWT) wa Wilaya ya Songea Mjini aliwataja Madiwani hao na kata zao kwenye mabano kuwa ni Mathew Ngalimanayo (Mjini), Maiko Mbano(Msamala), Issa Mkwawa (Matogoro) na Yobo Mapunda (Lilambo).
Amewataja wengine kuwa ni Festo Mlelwa (Seedfarm), Mussa Mwakaje (Mateka), Hajira Kalinga (Mfaranyaki) na John Ngonyani wa Kata ya Subira, pia kwa nafasi ya Unaibu Meya akiyechukua fomu ni Judith Mbogoro, Diwani Kata ya Matarawe.
Katibu huyo amesema katika Baraza la Madiwani la Halimashauri ya Manispaa lililopita nafasi ya Umeya, ilikuwa inashikiliwa na Alhaji Abdul Mshaweji ambaye alikuwa Diwani wa Kata ya Subira ambapo kwenye kinyang’anyiro cha kura za maoni ndani ya CCM, aliangukia pua na badala yake wanachama walimchagua John Ngonyani, kupeperusha bendera ya chama.
Wakati huo huo, Katibu wa CCM wa Wilaya ya Songea Vijijini, Mohamed Lawa amesema katika Halmashauri ya Songea aliyekuwa Makamu Mwenyekiti kwenye Baraza la Madiwani lililopita, Menas Komba ambaye ni Diwani Mteule wa Kata ya Matimira amechukua fomu ya kuomba kuwania nafasi ya Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo.
Lawa aliongeza kuwa kwa nafasi ya Makamu Mwenyekiti aliyechukua fomu ya kuomba kuwania nafasi hiyo ni Simon Kapinga, ambaye ni Diwani wa Kata ya Lilai Muhukuru.
Amesema pia katika Halmashauri ya Wilaya ya Madaba aliyechukua fomu ya kuomba kuwania nafasi ya Mwenyekiti ni Vistus Mfikwa, ambaye ni Diwani wa Kata ya Mkongotema anayetetea nafasi hiyo kwani katika baraza lililopita, alikuwa Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo na Teofanes Mlelwa ambaye ni Diwani wa Kata ya Wino.
More Stories
CCM hakuna kulala, Nchimbi atua Tabora kwa ziara ya siku mbili
Kongamano la Uwekezaji na Biashara lafunguliwa Pwani
Rais Samia afurahia usimamizi mzuri wa miradi