December 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Madiwani Kaliua wasikitishwa kuchelewa miradi ya maji

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Kaliua

MADIWANI wa halmashauri ya Wilaya Kaliua Mkoani Tabora wamemtaka Meneja wa Wakala wa Maji safi na Usafi wa Mazingira Vijijini Wilayani humo kuhakikisha miradi yote iliyokwama inatafutiwa ufumbuzi ili ikamilike.

Wakiongea katika kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri hiyo jana wameeleza kusikitishwa na baadhi ya miradi ikiwemo ya uchimbaji mabwawa na visima katika vijiji mbalimbali kukwama kwa mda mrefu hali inayoibua maswali.

Akiongea kwa uchungu diwani wa Kata ya Kazaroho, Haruna Kasele amesema kuwa Meneja amekuwa akitoa maelezo mazuri ya kutekelezwa miradi hiyo lakini cha kusikitisha hakuna kinachoendelea na miradi haikamiliki.

‘Tunataka kusikia mikakati ya kumaliza kero ya maji katika maeneo yote yanayolalamikiwa ikiwemo kata ya Makingi, Ichemba na kwingineko, tumechoka hadithi za kwenye makaratasi, uchaguzi umekaribia tutasema nini’, ameema.

Diwani wa Kata ya Ichemba katika tarafa ya Ulyankulu, Juma Hamduni amesema kuwa mradi wa Bwawa la Ichemba ulishaletewa fedha zaidi ya miaka 3 iliyopita, lakini cha kusikitisha hakuna kinachoendelea, hali inayoleta sintofahamu.

‘Huu ni mwaka wa 5 sasa tangu mradi wa Ichemba uanze kutekelezwa lakini hatuoni maendeleo yoyote, na wananchi kila siku wanauliza, lakini hawapati majibu ya kueleweka, Meneja tunaomba ufuatilie ili ukamilike sasa’, ameeleza.

James Nundo, diwani wa kata ya Makingi amelalamikia mradi wa kisima katika kata hiyo ambao uligharimu mamilioni ya fedha ambapo licha ya wataalamu kufanya utafiti kabla ya kuanza uchimbaji na kujiridhisha kwamba kuna maji, walipofanya majaribio walipata maji kidogo sana na kuamua kuachana nacho.

Amebainisha kuwa visima zaidi ya 5 vimeshachimbwa katika vijiji mbalimbali baada ya kufanyika utafiti wa uwepo wa maji lakini cha kusikitisha hadi sasa havitoi maji na kuhoji kama wataalamu hao wana weledi wa kutosha au la.

Diwani wa Kata ya Silambo, Mashaka Mpuya ameeleza kuwa licha ya kutengwa fedha kwa ajili ya mradi wa kisima cha Kijiji cha Mpandamlowoka hakuna utekelezaji wowote hadi sasa, hili linaumiza wananchi.

Akifafanua malalamiko hayo Kaimu Meneja wa RUWASA Wilayani hapa Mhandisi Zacheo John amesema kuwa wilaya hiyo haina mito, maziwa wala bahari kama yalivyo maeneo mengine hivyo vyanzo pekee vya maji ni visima au bwawa.

Amesisitiza kuwa wataendelea kutumia wataalamu kutafiti maeneo mengine yenye maji ardhini ili kuchimba visima, huku akiwatoa hofu kuwa maeneo yote waliyochimba visima na kukosa maji wataalamu watachimba vingine.

Kuhusu miradi ya mabwawa ya maji ameeleza kuwa taratibu za manunuzi kwa baadhi ya miradi hiyo zilichelewa kidogo ila miradi yote iliyokwisha tengewa fedha itatekelezwa kama ilivyopangwa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Japhael Lufungija amemwaagiza Meneja huyo kufuatilia miradi yote inayolalamikiwa na waheshimiwa madiwani na kutoa majibu sahihi katika kikao kijacho cha baraza la madiwani.

Amesisitiza kuwa majibu ya malalamiko hayo ni muhimu sana ili kujua miradi hiyo imekwama wapi na hatua gani zichukuliwe kabla ya kuingia kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa, aliongeza kuwa miradi hiyo ni utekelezaji ilani ya chama.