May 18, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Muhimbili yavuna kipande cha ubavu na kukiweka kama kiungo cha fuvu ili kumtengenezea magonjwa taya jipya

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Katika mwendelezo wa utoaji huduma za kibingwa na ubingwa bobezi unaotokana na kujenga uwezo wa watalaam wazawa chini ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Hospitali ya Taifa Muhimbili, leo kwa mara ya kwanza imefanya upasuaji wa kutoa mfupa kwenye ubavu na kutengeneza kiungio (joint) cha taya la chini na fuvu ili kumtengenezea mgonjwa taya jipya la kulia lililoathiriwa na uvimbe.

Akizingumza baada ya upasuaji huo, Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Uso na Taya Dkt Arnold Augustino amesema, mgonjwa huyo amefanyiwa upasuaji wa kuondoa taya lote la kulia lililoathiriwa na uvimbe na hivyo kumtengenezea taya jipya kwa kuchukua mfupa kutoka kwenye ubavu ambapo mfupa huo umepandikizwa kwenye kiungio cha taya.

Ameongeza kuwa mifupa mingine imechukuliwa kutoka kwenye nyonga pande zote mbili ili kuunganishwa na mfupa uliotolewa kwenye ubavu kuwezesha kutengenezwa kwa taya sawasawa na taya lake la awali na kisha kuunganishwa na kipandikizi cha chuma maalum kutengeneza sehemu ya taya iliyoharibika na ugonjwa.

Amesema, mara baada ya upasuaji huu mgonjwa huyo anategemea kuendelea kula na kutafuna kama kawaida kwani atawekewa meno bandia kwenye mfupa wa taya aliotengenezewa.

Ameongeza kuwa mgonjwa huyo amefanyiwa upasuaji aina tatu tofauti kwa wakati mmoja, wa kutoa kipande cha mfupa kwenye ubavu, wa pili ni kutoa mifupa kwenye nyonga zote mbili na wa tatu ni kuondoa uvimbe ambapo umechukua saa saba umeshirikisha timu watalaam wa MNH madaktari bingwa wa taya na uso (5) wataalamu usingizi na ganzi (2) manesi wa upasuaji (3) na wataalamu wengine waliokuwepo ni pamoja madaktari wanaosomea ubingwa wa kupasua mataya na uso (3)