May 21, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Machifu, Wazee wa kimila waombwa kupinga matumizi dawa za kulevya

KAIMU Kamishna Msaidizi wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Kanda ya Kati Dodoma, Christian Mbwasi amewaomba wazee wa kimila na Machifu nchini, kwa nafasi zao kupinga matumizi ya dawa za kulevya, ili kuiokoa jamii.

Pia, amewataka kutekeleza majukumu yao ya kuirejesha jamii katika misingi na tamaduni za mtanzania na kuukumbusha umma juu ya athari za kujihusisha na matumizi kilimo cha bangi, mirungi hali inayohatarisha ustawi wa taifa.

Hayo ameyasema leo kwa viongozi hao kutoka kanda ya Kati Dodoma na kanda ya pwani kwa mkoa wa morogoro pamoja na zanzibar, aliposhiriki kwenye sherehe za kimila zilizofanyika viwanja vya machifu eneo la bwibwi, Jedengwa Mkoani Dodoma alipokuwa akitoa salamu za Mamlaka.

Amesema, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, inaamini kupitia sauti za wazee wa kimila, kwa umoja wao wataweza kuiokoa jamii kuondokana na matumizi ya dawa hizo.

“Ninyi ni viongozi wa jamii, tunaamini kwa kupitia sauti zenu ujumbe wetu utafika kwa haraka kuhusiana na kuitaka jamii kuondokana na matumizi ya dawa za kulevya, hivyo tunaomba ushirikiano wenu katika hili, ili jamii iwe salama,” amesema Mbwasi.

Kwa upande wake, Afisa Utamaduni Jiji la Dodoma, Dezdel Ruzenza, ameiomba Mamlaka hiyo kuendesha majukwaa ya kutoa elimu kuhusiana na dawa za kulevya kufanyika mara kwa mara.

Nae Mkurugenzi kutoka Taasisi ya Pick Foundation, Shiganga George, amesema, taasisi hiyo inaunga mkono jitihada zinazoendelea kufanywa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, kupitia Kamishna Jenerali Aretas Lyimo, ambaye ameendelea kupiga na kuwachukulia hatua wale wote wanaobainika kutumia na kuuza dawa hizo.

Ameipongeza Mamlaka hiyo, kutumia nafasi ya kukutana na wazee wa kimila, kuwataka kutumia nafasi zao katika jamii kukemea vitendo vya matumizi ya dawa za kulevya ili kuokoa vijana kutojiingiza katika matumizi hayo.

Kwa upande wake, Mjukuu wa Chifu Chioma, Jailos Chioma, amesema kupitia elimu waliyopata kuhusiana na matumizi ya dawa za kulevya, kwa umoja wao watatumia vikao vyao kuelimisha vijana kuepukana na matumizi ya sawa hizo.