NAGASAKI, Zaidi ya mabaharia 34 waliokuwa kwenye meli ya safari za kitalii iliyotia nanga katika mji wa Nagasaki nchini Japan wamegundulika kuwa na virusi vya Corona (COVID-19).
Kwa mujibu wa Msemaji Mkuu wa Serikali ya Japan, Yoshihide Suga, meli ya Costa Atlantica (PICHANI JUU) iliwasili kwa mara ya kwanza Nagasaki mwezi Januari, mwaka huu kwa ajili ya kufanyiwa ukarabati ikiwa imewabeba mabaharia 600.
Alisema, mwishoni mwa wiki iliyopita wasimamizi wa meli hiyo waliwasiliana na mamlaka kutaka msaada wa kufanyiwa uchunguzi wa kiafya watu kadhaa waliokuwa wakishukiwa kuwa na virusi hivyo.
Aidha, baada ya hatua hiyo alisema, mabaharia wote wako ndani ya meli ikiwemo waliokutwa na virusi.
Wakati huo huo, imeripotiwa kuwa, watoto wachanga wanane katika kituo kimoja cha malezi nchini Japan wamekutwa na maambukizi ya virusi vya Corona baada ya mhudumu mmoja wa kituo hicho kupata maambukizi.
Hospitali Kuu ya Saiseikai mjini Tokyo ambayo inakisimamia kituo hicho ilieleza kuwa, watoto hao walioambukizwa wamelazwa hospitali wakati wengine 21 wamegundulika hawana virusi na wanaendelea kufuatiliwa.
Kituo hicho ni cha watoto yatima wakiwemo watoto waliotenganishwa na wazazi wao kutokana na sababu za uwezekano wa kunyanyaswa au kutelekezwa.
Aidha, bila kutoa maelezo mengi hospitali hiyo imetoa taarifa ikisema mhudumu wa kituo hicho alikutwa na maambukizi Aprili 16, mwaka huu na kusababisha kufanyika maamuzi ya kuwapima watoto wote.
WASHINGTON
Katika hatua nyingine, afisa mmoja wa kijeshi nchini Marekani amesema kuwa meli 26 za kivita za nchi hiyo zimekumbwa na virusi vya Corona.
Afisa huyo wa kijeshi aliyasema hayo katika mahojiano na mtandao wa habari wa Hill wa nchini Marekani na kuongeza kuwa, meli hizo za Marekani zilikuwa zimetia nanga bandarini na kwamba kila moja, imekumbwa na tatizo la virusi vya Corona.
Inadaiwa kuwa, theluthi moja ya askari wa majini wa Marekani wameathirika na virusi hivyo hatari vya Corona baada ya kusajiliwa kesi 1,298 katika jeshi hilo.
Pia inadaiwa,karibu nusu ya kesi hizo zinawahusu askari wa meli ya kivita ya Theodore Roosevelt.
More Stories
Dk. Mpango amwakilisha Samia sherehe za Uhuru wa Lesotho
Samia atangaza Tanzania kumuunga mkono Odinga
Tanzania yaongoza kikao maalum cha nishati safi