December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mabadiliko ya tabianchi yatajwa kichocheo ongezeko la Malaria

Na Agnes Alcardo, Timemajira Online. Dar

WAGONJWA wa malaria wameripotiwa kuongezeka, huku chanzo kikielezwa kuwa ni Mabadiliko ya tabianchi, yanayosababisha kuongezeka kwa mvua zinazosababisha mazalia ya mbu.

Akizungumza mwishoni mwa wiki, Jijini Dar es Salaam, wakati akifungua Kongamano la Malaria la mwaka 2024, lililoandaliwa na Taasisi ya Afya Ifakara ( ihi), lililowakutanisha, watafiti, Serikali, watunga sera na jamii kwa ujumla, ili kuweza kujadili namna ya kutokomeza ugonjwa wa Malaria na kufikia zero mwaka 2030.

Mganga Kuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu amesema, pamoja na kuwepo kwa ongezeko la wagonjwa, pia vifo vitokanavyo na ugonjwa wa malaria vimeongezeka.

Amesema, wagonjwa wa Malaria wametajwa kuongezeka katika kipindi cha mwaka 2023, huku jamii ikisisitizwa kuchukua tahadhari ili kujikinga na ugonjwa huo, ikiwa pamoja na kutumia vyandarua vyenye dawa.

Ameongeza kuwa, kwa upande wa Zanzibar, 2022 waliripotiwa kuwepo kwa wagonjwa 4000 wa malaria, tofauti na huku mwaka 2023 kuwa na ongezeko la wagonjwa 19,000, huku akitaja takwimu zaTanzania Bara za mwaka 2022 kuwa kulikuwa na wagonjwa 3,478,875, ambapo mwaka 2023 kulikuwa na wagonjwa 3,534,523 ikiwa sawa na ongezeko la asilimia 1.6, huku vifo vikiongezeka kutoka 1,430 hadi kufikia 1,954 kwa mwaka 2023.

“Mwaka huu kama tulivyoona wote mvua zimeongezeka na mabadiliko ya tabianchi husababisha husababisha ongezeko la ugonjwa wa Malaria, hivyo tunaishukuru sana Taasisi ya Afya Ifakara kwa kuendelea kuwakutanisha wadau mbalimbali katika masuala ya afya na kujadili jinsi ya kupambana na ugonjwa wa Malaria”, amesema Dkt. Tumaini.

Aidha amewaagiza wanasayansi kuangalia njia ya kutumia Teknolojia ili kudhibiti malaria, akitolea mfano wa mabadiliko ya tabianchi jinsi gani wanaweza kufikia jamii kwa kutumia teknolojia ili kufikisha ujumbe kwa jamii namna ya kujikinga na ugonjwa huo.

Nae Mkurugenzi Mkutendaji wa Taasisi ya Afya Ifakara (ihi), Dkt. honorati Masanja, amesema, lengo la taasisi hiyo ni kuhakikisha inatokomeza ugonjwa wa Malaria kabisa na kudai kuwa tayari jitihada zimeshaanza kufanywa ambapo hadi kufikia 2030 ugonjwa huo kutokuwepo kabisa.