July 3, 2022

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Maafisa habari wa serikali washiriki bonanza la michezo jijini Tanga

Na Hadija Bagasha, TimesMajira Online, Tanga

Maafisa habari wa serikali wameshiriki bonanza la michezo jijini Tanga ikiwemo mchezo wa mpira wa miguu kwa wanaume, kuvuta kamba kukimbia na magunia pamoja na mpira wa pete (Netball) kwa wanawake.

Maafisa habari hao wa Mikoa, Halmashauri na taasisi zote zilizopo chini ya serikali wameshiriki bonanza hilo la michezo wakiwa jijini Tanga kwenye kikao kazi cha 17 kinachofanyika kwa siku tano jijini Tanga.

Akizungumza katika bonanza hilo msemaji wa serikali Gerson Msigwa amewataka waandishi wa habari kufanya mazoezi kwajili ya kuimarisha afya zao ili wawexe kuwa imara wakati wa kutekeleza majukumu yao ya kihabari.

Msigwa amesema kuwa wamefurahi kushiriki michezo hiyo ambayo imewakutanisha pamoja jambo ambalo litawafanya waendelee kuwa imara katika majukumu yao ya kila, siku.

“Michezo hii itausaidia kupeleka ujumbe kwa watanzania kwamba michezo ni sehemu ya maisha yetu tukiiweka mbali michezo tutakuwa na afya zisizoridhisha na matokeo yake sisi maafisa habari tutashindwa kufanya kazi zetu vizuri ya kufikisha ujumbe kwa wananchi wetu, “alisisitiza Msigwa.

Akifungua bonanza hilo mkuu wa wilaya ya Tanga Hashimu Mgandilwa amewataka watumishi wote wa serikali kuwa na desturi ya kupenda kufanya mazoezi mara kuwa mara ili kuimarisha afya zao ikiwa pia ni njia moja wapo ya kuondokana na magonjwa mbalimbali yasiyoambukiza.

“Nataka niwaambieni kuwa mazoezi ni muhimu sana wengi wetu wafanyakazi tumekuwa ni wahanga wa kubwa sana lakini kupita mazoezi itatusaidia kuondokana na magonjwa mbalimbali amabayao tunaweza kujikinga kupitia mazoezi na hii isiwe kwa watumiashi tu bali Hata watu wa kawaida waone umuhimu wa kufanya mazoezi “Alisema Mgandilwa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Maafisa habari Nchini Pascal Shelutete amewapongeza maafisa habari hao kwa kushiriki michezo hiyo huku akiwataka kuendelea kutoa taarifa kwa wananchi juu ys miradi mbalimbali ya kimaendeleo inayofanywa na serikali pamoja na miradi ya kimakakati.

Katika mchezo wa mpira wa miguu uliowakutanisha mashabiki wa timu ya Yanga SC dhidi ya watani wao wa Jadi Simba SC ulimalizika kwa Yanga kuwagalagaza wenzao baada ya kuwashushia kipigo kizito cha mabao 4-1 michezo yote ikifanyika katika viwanja vya Popatlal jijini Tanga.

Kwa upande wa mchezo wa kuvuta kamba Chama cha maafisa Habari na mawasiliano wa Serikali, (Tagco) waliwashinda nguvu Mkwakwani Fitness kwa wanaume , huku upande wanawake Tagco wakiendeleza ubabe huo kwa Tanga kwanza wanawake.