
Na Joyce Kasiki, TimesMajiraonline
MKUU wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (LATRA), Salum Pazzy, ametoa onyo kali kwa watoa huduma za mifumo ya tiketi kwa njia ya mtandao, akisisitiza kuwa leo Juni 30, 2025 ni siku ya mwisho ya kukamilisha taratibu zote muhimu zinazohitajika kwa ajili ya kutoa huduma kwa mujibu wa masharti ya LATRA.
“Kuanzia kesho, Julai Mosi 2025, LATRA itatoa taarifa rasmi kwa umma kuhusu hatua zitakazochukuliwa kwa wale wote ambao hawajakamilisha taratibu hizi. Tangazo lilitolewa mapema, na hivyo hakuna sababu ya kutofikia viwango vilivyowekwa,” alisema Pazi kwa msisitizo.
Akizungumza Juni 30,2025 katika maonyesho ya kimataifa ya Biashara jijini Dar es Salaam kwenye banda la LATRA Pazzy amesema kuwa LATRA haitaruhusu utoaji wa huduma yoyote kwa mtoa huduma ambaye hajakidhi matakwa hayo, hatua ambayo inalenga kulinda abiria dhidi ya usumbufu na kuhakikisha usalama na uwajibikaji wa watoa huduma.
Katika kuimarisha huduma za usafirishaji, Pazzy pia almeeleza kuwa LATRA imewekeza katika mifumo ya kisasa kama mfumo wa tiketi mtandao ambao husaidia mamlaka kufahamu idadi ya abiria wanaosafiri kwenda maeneo mbalimbali, hivyo kurahisisha kupanga na kuongeza leseni kulingana na mahitaji halisi ya soko.
Mfumo huo pia unatoa taarifa ya majina ya abiria waliopo kwenye kila chombo, jambo linalosaidia katika masuala ya kiusalama na ufuatiliaji wa safari.
Aidha amesema , LATRA ina mfumo wa huduma kwa wateja unaomwezesha abiria kutoa malalamiko au taarifa za changamoto wanazokutana nazo safarini, ambapo taarifa hizo huandikwa rasmi kwa ajili ya ufuatiliaji na ushahidi dhidi ya mtoa huduma husika.
Kuhusu ukaguzi wa Leseni na Nauli Kupitia LATRA App ,Pazzy amebainisha kuwa mfumo huo umekuwa ekuwa nyenzo muhimu kwa abiria, ambapo kwa sasa mtu anaweza kukagua leseni ya gari analopanda ili kuhakikisha kuwa mtoa huduma anatoa huduma kwa mujibu wa sheria.
Amesema App hiyo pia inamwezesha abiria kujua nauli halisi, umbali wa vituo vya mabasi na madaraja ya huduma, hivyo kuondoa migogoro na kero zilizokuwa zikijitokeza awali.
Akizungumzia mifumo mingine ya kisasa, ametaja mfumo wa Taarifa kwa Abiria (PIS) kuwa moja ya nyenzo muhimu kwa abiria, wasindikizaji na hata familia zao, kufahamu mahali halisi lilipo basi, saa linatarajiwa kufika stendi fulani na maendeleo ya safari hiyo.
Amesema mfumo huu umetengenezwa kwa kutumia teknolojia ya akili mnemba (AI), ambayo huhesabu kwa usahihi mwendo wa basi, vituo vitakavyopita na muda wa kufika kwenye kila kituo, hivyo kusaidia kupanga safari kwa ufanisi zaidi.
Kwa kutumia mfumo huo, mtu anaweza kufungua ramani ya stendi aliyopo – mfano Nane Nane, Dodoma – na kuona mabasi yote yanayokuja katika kituo hicho na muda yanayotarajiwa kufika.
Huduma kwa Watoa Huduma: Usajili Mtandaoni na Uthibitishaji wa Leseni
Kwa upande wa watoa huduma,amesema LATRA inatoa huduma ya usajili wa wahudumu wa mabasi, usajili wa madereva wanaoelekea kufanya mitihani ya kuthibitishwa, pamoja na kuruhusu uwasilishaji wa maombi ya leseni kwa njia ya mtandao. Hii imeleta mageuzi makubwa kwa sekta ya usafirishaji kwa kupunguza urasimu na kuongeza uwazi.
Pazzy ametumia nafasi hiyo kuwaalika wananchi wote na wadau wa sekta ya usafiri ardhini kutembelea banda la LATRA , ili kujionea huduma zote wanazotoa kwa uwazi.

More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi