Na Hadija Bagasha,TimesMajira Online, Tanga
Naibu waziri wa katiba na sheria Geofrey Mizengo Pinda amesema mpaka kufikia mwaka 2025 kila wilaya itakuwa na mahakama za wilaya nchini ili kuweza kurahisisha utoaji wa huduma za kimahakama kwa wananchi.
Naibu waziri huyo ametoa kauli hiyo wakati wa ziara ya kamati ya kudumu ya bunge ya katiba na sheria iliyotembelea mahakama kuu kanda ya Tanga.
Kamati hiyo ilitembelea mradi wa jengo la uhifadhi wa nyaraka za kumbukumbu za kimahakama ikiwa ni muendelezo wa kutembelea na kukagua miradi yote iliyotengewa fedha kwa mwaka 2021/22.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Tanga Naibu waziri amesema kati ya kata 3800 ni kata 960 ambazo zimeshapelekewa huduma ya mahakama na wanaendelea na maboresho hayo ili ifikapo 2025 ngazi ya wilaya iwe imepata mahakama ya wilaya.
Kwa upande wa ngazi ya Kata Naibu waziri Pinda amesema kipaumbele kimetolewa kwenye makao makuu ya tarafa wakati serikali ikiangalia uwezekano wa kujenga mahakama hizo kwenye ngazi ya kata.
“Ndani ya tarafa moja unaweza ukaenda kilomita zaidi ya 100 maeneo hayo yatapewa kipaumbele cha kufikiwa na hiyo huduma, “alisema Naibu waziri Pinda.
Alisema kwa upande wa Mkoa wa Tanga ni wilaya moja ya Mkinga ambayo bado haijawa na mahakama ya wilaya na kwamba tayari fedha zimeshatolewa na mahakama inaendelea na ujenzi wa mradi na hadi ifikapo mwishoni mwa mwezi wa 4 jengo hilo litakuwa limekabidhiwa na kuanza kutoa huduma kwa wananchi.
Kwa upande wake Makamu mwenyekiti wa kamati hiyo Emmanuel Mwakasaka amesema lengo la ziara yao ni kukagua miradi ambayo imepatiwa fedha za serikali kwa kipindi cha mwaka 2021/22 kuikagua na kwamba mbali ya yote amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuujali mhimili mkubwa wa mahakama.
Awali akizungumzia mradi wa jengo la uhifadhi wa nyaraka za kimahakama Makamu Mwenyekiti huyo amesema wameridhishwa na mradi huo huku wakisifu maboresho ya mfumo wa Tehama kwenye mahakama nchini.
“Mimi kwa niaba ya kamati ya bunge ya kudumu ya katiba na sheria tunawapongeza kwa namna ya maboresho mliyofika na kwamba kukamilika kwa ujenzi wa jengo la mahakama Wilayani Mkinga utasaidia kurahisisha huduma karibu na jamii, “alisistiza Kaimu Mwenyekiti huyo.
Profesa Elisante Ole Gabriel ni Mtendaji mkuu wa mahakama amesema mahakama inaanzisha nadharia mpya ya kujenga mahakama ya mwanzo, mahakama ya wilaya, mahakama ya hakimu mkazi, na mahakama kuu kwenye jengo moja lengo likiwa ni kupunguza usumbufu wa wananchi wa kutoka mahakama moja hasi nyingine.
“Kwa mfano mtu akitoka pale mahakama ya Temeke inashughulika zaidi na masuala ya kifamilia na mirathi akiwa mahakama ya mwanzo ni sakafu ya chini na, kama hajaridhika anataka kukata rufaa haendi tena kurasini au Gombolamboto anapanda tu gorofa inayofuata hajaridhika anaenda inayofuata mpaka mahakama ya rufaa inaweza kuwa pale, “alibainisha Elisante
Hata hivyo alisema lengo la serikali ni kuwezesha mahakama kwamba katika kanda zote 18 kuwa na hivyo vituo jumuishi, akitoa takwimu kwamba kwa sasa hivi vipo 6 viwili kwa Daresalaam, Morogoro, Arusha na Mwanza.
Ikiwa katika Mkoa wa Tanga kamati hiyo imetembelea mradi wa uhifadhi wa kumbukumbu za kimahakama pamoja na chuo cha sheria na mahakama cha IJA kilichopo Wilayani Lushoto.
More Stories
Serikali kupeleka mawasiliano maeneo ya mipakaniÂ
Sekondari ya Butata mbioni kufunguliwa Musoma Vijijini
TIC yapongeza mradi wa Kampuni ya Big Best