Na Mwandishi Wetu,Timesmajira Online, Dar
SERIKALI ya Awamu ya Sita inaelekea kutimiza miaka mitatu chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, tangu aliporithi mikoba ya Hayati Rais John Magufuli, Machi 19, 2021.
Kwa muda huo wote wa uongozi wa Rais Samia, tumeshuhudia utendaji, sera na falsafa yake ya R4 inavyozidi kushamirisha demokrasia nchini.
Kwenye uwanja wa siasa ameendelea kuachia nafasi nzuri wanasiasa kujadiliana na kuamua hatima ya maisha yao kisiasa, sanjari na kuruhusu pia waandamane, kuandamana jambo ambalo ni tofauti na ilivyokuwa huko nyuma.
Mfano, leo hii tayari tumeshuhudia chama kikuu cha upinzani CHADEMA kikifanya maandamano katika mikoa mitatu mikubwa nchini ya Dar es Salaam, Mwanza na Mbeya ambayo yalifanyika juzi.
Kinachoonekana leo kinanikumbusha kauli ya Rais Samia aliyoitoa siku za mwanzo aliposhika nafasi hiyo, akisema;
“Nilisema mwanamke ni kujiamini nami kama Mwenyekiti wa CCM najiamini, najiamini kufungua uwanja wa siasa nikijua kwamba wana CCM tutakwenda pamoja na tutajadiliana na wenzetu na kuifanya nchi yetu twende vizuri.”
Hicho alichokisema Rais Samia ndicho kinaonekana sasa, kwani kwenye maandamano yanayofanywa na CHADEMA, tumeshuhudia viongozi wa CHADEMA hicho kwamba kwenye maandamano yao hakuna hata sisimizi aliyeumizwa.
Maandamano hayo wanayojifunia hata sisimizi kutoumizwa yameruhusiwa na Rais Samia tangu Serikali ya awamu ya tano ilipoyazuia pamoja na mikutano ya hadhara mwaka 2016.
Tofauti ya sasa na wakati ule wa zama za hayati Magufuli ni kwamba utawala ule haukujali kuufungamanisha uhalali wa serikali yake katika mageuzi ya kidemokrasia. Kitu ambacho Serikali ya Samia inajali hilo.
Kinachoonekana sasa ni kuendelea kueleweka kwa dhana ya R4 za Rais Samia Suluhu Hassan kwa wadau wa demokrasia nchini baada ya msafara wa Naibu Waziri Mkuu, Dkt. Doto Biteko kukutana na maandanano ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), huku kila upande ukiendelea safari zake bila kubughudhi mwenzake.
Hayo yalijiri jana juzi Mbeya wakati wa msafara ya Dkt. Biteko ulipokutana na waandamanaji wa CHADEMA, lakini kila upande ulionekana kutekeleza kwa ueledi R4 za Rais Samia.
R4 hizo za Rais Samia ni maridhiano, ustahamilivu, mageuzi na kujenga upya sasa.
Kilichokidhihirisha jana kwenye maandamano hayo ni ustahamilivu, kwani waandamaji walisika wakifikisha ujumbe wao kwa Naibu Waziri Mkuu, Dkt. Biteko kwamba wanataka Katiba Mpya.
“Mwimbie Naibu Waziri Mkuu kwa sauti kwamba tunataka katiba mpya…, Ndugu Waziri Mkuu kundi linalopita linataka Katiba Mpya, muimbie,” alisema mmoja wa washereheshaji wa maandamano hayo, huku waandamanaji wakiendelea kuiomba wanataka katiba mpya.
Mshereheshaji hiyo, aliwaambia kwamba upatikanaji wa Katiba mpya utasaidia kupugua kwa misafara mikubwa ya viongozi, kwani ni matumizi ya mabaya ya mali ya umma.
Kitendo cha kukutana kwa msafara ya Dkt. Biteko la maandamano ya CHADEMA, kinazidi kuipatia umaarufu Rais Samia, kwani miaka yote iliyopita, mikutano ya vyama vya siasa au maandamano yalizuiwa kufanyika pale ambapo kwenye mkoa fulani kama kulikuwa na ziara au shughuli za viongozi wa kitaifa au vyama vingine vya siasa.
“Kilichoonekana Mbeya leo (jana) ni kielelezo kwamba Rais Samia amefanikiwa kuijenga Tanzania yenye haki, demokrasia na usawa, ndiyo maana tulichokiona hakiwezi kuonekana nchi nyingi na hata hapa hakijawahi kutokea,” alisema John Mwambukile aliyekuwa kwenye maandamano hayo.
Amesema kitendo cha Rais Samia kuruhusu demokrasia itamalaki kwenye nchi yetu, kimewapunguzia hasira Watanzania na sasa hivi wanafikisha ujumbe wao kwa kwa watawala kwa misingi ya kuvumiliana.
Alisema mabadiliko yaliyofanywa na Rais Samia katika uwanja wa siasa na namna wadau walivyoelewa falsafa zake za 4R ni jambo la Pongeza.
“Sasa hivi nao wameanza kuelewa R4 maana hata Polisi wale waliokuwa kwenye msafara wa Dkt. Biteko hakuna aliyeshuka kwenye gari, lakini pia waandamanaji wa CHADEMA, waliachia upande mmoja msafara ukaendelea na safari, hii ni fundisho kwa nchi nyingine za Afrika,” Amesema Mbone Mwaikina.
Amesema miaka sita iliyopita kulikuwa na tofauti za kisiasa zilizosabbisha kutokuwa na majadiliano baina ya chama tawala na vya upinzani, lakini tangu Rais Samia aingie madarakani mazungumzo yanafanyika na leo (jana) wameona matokeo yake.
Anasema Rais Samia amefungua ukurasa mpya wa siasa. Maandamano ya CHADEMA yaliyoongozwa na viongozi wa CHADEMA yalihitimishwa kwenye Viwanja vya Luanda Nzovwe.
Miongoni mwa waandamanaji waliokuwa na mabango yaliyokuwa na ujumbe mbalimbali. Maandano hayo yaliongozwa na Mwenyekiti Freemano Mbowe, na viongozi wengine wa juu yakimhusisha aliyekuwa Katibu Kuu wa CHADEMA, Dkt. Wilbroad Slaa .
Makala haya yanaangazia mabadiliko yaliyofanywa na Rais Samia katika uwanja wa kisiasa na namna wadau walivyoelewa falsafa yake ya 4R.
Itakumbukwa miaka sita iliyopita kulikuwa na tofauti za kisiasa zilizosababisha kutokuwa na majadiliano baina ya chama tawala na vya upinzani lakini tangu Rais Samia aingie madarakani mazungumzo yanafanyika.
Rais Samia amefungua ukurasa mpya wa siasa na demokrasia lakini kubwa ni fursa ya maridhiano ambayo yanaendelea mpaka sasa.
Dhamira yake ya kukutana na vyama vya siasa, mtu mmoja mmoja inatafsiriwa na wadau mbalimbali wa demokrasia kuwa inaleta faraja kwa wengi.
Rais Samia pia alitangaza kuruhusu kufanyika kwa mikutano ya kisiasa ya hadhara ambayo ilipigwa marufuku tangu mwaka 2016.
Aidha katika kuendelea kushughulikia masuala yanayohusu demokrasia ya vyama vingi vya siasa, Rais Samia alielekeza kuundwa kwa kikosi kazi ambacho kilipokea maoni na mapendekezo kisha kupendekeza mabadiliko yanayoweza kufanywa kuelekea mwaka 2025.
Kikosi kazi hicho kilichokuwa kikiongozwa na Profesa Rwekaza Mukandala, kilijumuisha viongozi wa serikali, asasi za kiraia, wasomi na viongozi wa vyama vya kisiasa.
Kilifanyia kazi maeneo tisa, mikutano ya hadhara na mikutano ya ndani ya vyama vya siasa, masuala yanayohusu uchaguzi, mfumo wa maridhiano ili kudumisha haki, amani, utulivu na umoja wa kitaifa.
Maeneo mengine ni ushiriki wa wanawake na makundi maalumu katika siasa na demokrasia ya vyama vingi vya siasa, elimu ya uraia, rushwa na maadili katika siasa na uchaguzi, ruzuku ya Serikali kwa vyama vya siasa, uhusiano wa siasa na mawasiliano kwa umma na suala la katiba mpya.
Mpendekezo kadhaa ya kikosi kazi hicho yanaendelea kufanyiwa kazi.
Pia chini ya utawala wake Rais Samia alielekeza kupitiwa mienendo ya baadhi ya kesi nchini pamoja sheria zilizoonekana kuwa na ukakasi na kuzifanyia marekebisho.
Kutokana na hatua hiyo watu zaidi ya 400 waliokuwa mahabusu kwa kesi zisizo na ushahidi waliachiwa huru, wakiwamo viongozi wa Uamsho waliokaa mahabusu kwa miaka minane wakituhumiwa kwa ugaidi.
Rais Samia alitangaza nia yake ya kuhakikisha Tanzania inachangamana na jumuiya ya kimataifa na kuihakikishia dunia kuwa Tanzania haitajifungia, itayapa kipaumbele mashirikiano ya kiuchumi na kimaendeleo.
Ameendelea kutembelea nchi mbalimbali na kuhudhuria vikao vya wakuu wa nchi mbalimbali ukiwamo mkutano wa 76 wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa.
Hatua ya kurejesha uhusiano wa kimataifa baina ya Tanzania na mataifa mengine duniani imewezesha kupata mafanikio mbalimbali ikiwemo mkopo wa sh. trilioni 1.3 wa masharti nafuu uliotolewa na IMF kwa ajili ya mapambano dhidi ya Uviko-19.
Fedha hizo zimetumika katika miradi mbalimbali ikiwamo ya ujenzi wa madarasa ya shule za msingi na sekondari, ununuzi wa vifaa tiba na miradi ya ujenzi wa miundombinu ya maji safi na salama.
Wadau mbalimbali wa demokrasia wameonesha namna 4R zilivyoleta mabadiliko nchini.
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema – Zanzibar, Salum Mwalimu, anasema 4R zinajenga misingi ya kuvumiliana kwa hoja ili kufika kwenye ujenzi wa Tanzania mpya.
“Rais alichukua nchi katikati ya mawimbi makubwa, tulitoka katika uchaguzi uliozaa taharuki kubwa ndani na nje. Rais aliona tunahitaji kurejea kwenye mstari, aliona haja ya kuzungumza kama taifa na kutuunganisha Watanzania,” anasema Mwalimu.
Katibu Mkuu wa Chama cha ACT – Wazalendo, Ado Shaibu, anasema 4R zitazamwe kwa muktadha zaidi kwani zikitekelezwa kwa ukamilifu taifa litakwenda sambamba na malengo ya dunia.
“Rais hakuwa na presha yoyote ya kisiasa lakini alitukuta tuko hoi, lakini kwa uungwana na hekima zake aliona bado taifa linahitaji 4R, kwa hilo tunampongeza sana…4R itapimwa kwa vitendo hivyo wadau wote tunayo kazi kubwa ya kufanya,” anasema Ado.
Mwanasiasa Mkongwe, Dkt. Getrude Mongela, anasema Rais Samia ameleta misingi ambayo itasaidia hasa wakati huu wa kutengeneza dira ya taifa na kushauri elimu iendelee kutolewa ili umma uzielewe 4R.
“4R zisiwe za mama Samia peke yake, ziwe za Watanzania wote, elimu itolewe huku tukizingatia pia matumizi ya lugha kwa sababu kuna watu wasomi na wasiosoma bado hawajajua 4R,” anasema Dk. Mongela.
Mwanasiasa Stephen Wassira, anasema; “Nimemuelewa zaidi Rais Samia na falsafa yake ya 4R, tunaendelea kuwa na mfumo wa vyama vingi, tofauti zetu hazivunji umoja wa kitaifa hivyo, kuaminiana kunahitajika zaidi.
Katibu Mkuu wa Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC), Doyo Hassan, anasema watendaji wa Serikali wanapaswa kuzielewa 4R za Rais Samia na kushauri yatengenezwe mazingira ya kuhakikisha falsafa hizo zinatekelezwa kwa vitendo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Jenister Mhagama, anasema Rais Samia ameanzisha utaratibu shirikishi wa watu kusikilizana ambao umeleta mabadiliko makubwa.
“Vyama viendelee kuzingatia falsafa ya 4R ili kuleta mageuzi ya mfumo wa demokrasia nchini,” anasema Waziri Mhagama.
More Stories
Siri ya Rais Samia kutembea kifua mbelea kijivunia Mapinduzi Matukufu ya Z,bar
Rais Samia anavyotimiza ahadi yake ya kumtua ndoo ya maji mwanamke
Rais Samia anavyozidi kusogeza karibu watoto wa kike na kasi ukuaji teknolojia