May 16, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kasi ya Rais Samia kufungua uchumi iwaamshe wasaidizi


Na Markus Mpangala, TimesMajira Online

UTAFITI Oxford Economics mwaka 2016 unaonesha kuwa asilimia sabini na nane(78%) ya biashara ya bidhaa na huduma imefungamanishwa na rasilimali za asili za nchi za kusini kwa njia ya moja kwa moja au kwa njia ya mahusiano kati ya biashara moja na nyingine, nchi moja na nyingine au kampuni moja na nyingine.

Nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara zinachangia asilimia arobaini na saba (47%) ya hiyo asilimia sitini kwa njia ya moja kwa moja au njia ya mahusiano ya kibiashara. Pamoja na kujifungamanisha na biashara hii ya Dunia kiasi hicho, bado mchango wa Afrika, kusini mwa Sahara kwenye biashara ya dunia, ni chini ya asilimia nne nukta tano (4.5) kwa mujibu wa tafiti za hivi karibuni za Chuo Kikuu cha Sussex cha nchini.

Kwa msingi bado safari ya kufungua uchumi ingalipo na serikali inafanya juhudi kuhakikisha kila mkoa wa Tanzania unatumia fursa zake kuinuka kiuchumi.

Uthibitisho wa safari ya Rais Samia kufungua uchumi wa mikoa ya kusini na namna anavyoiunganisha na sehemu nyingine.

Inafahamika kuwa ujenzi wa barabara za kiwango cha lami katika wilaya ya Tunduru kuunganisha na wakazi wan chi ya Msumbiji ni lango mojawapo la kuifungua nchi yetu kiuchumi.

Vilevile wananchi wa mkoa wa Ruvuma wanayo matumaini makubwa baada ya serikali kuendelea kumpa nafasi mkandarasi kukamilisha ujenzi wa barabara ya Kitai hadi Ruanda ambako eneo hilo limekuwa likitawaliwa na wawekezaji wakubwa wanaochimba Makaa ya Mawe.

Vitalu vya uchimbaji wa Makaa ya Mawe kuanzia kijiji cha Amanimakoro hadi Ruanda vinatarajiwa kufungua uchumi wa wananchi wa mikoa ya kusini na kujiunganisha na majirani zao wa Msumbiji, Malawi na hata Zambia.

Meli za abiria kutoka Msumbiji zinatarajiwa kufanya safari upande wa bandari za Tanzania jambo ambalo limekuza uhusiano mkubwa unaoendelea kwa sasa kutokana na juhudi za serikali ya awamu ya sita.

Tangazo la kufanya Mji wa Mbamba kuwa makao makuu ya bandari kwa mkoa wa Ruvuma limekuja hivi karibuni huku maelfu ya wananchi wa mkoa huo wakiwa na matumaini ya ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami kuanzia kijiji cha Ruanda hadi Bandari ya Ndumbi inayotarajiwa kuhudumia wafanyabiashara wa ndani nan je.

Juhudi za serikali ya Samia kuwaunganisha wananchi pamoja na kuwafungulia nchi kiuchumi inaonesha bayana namna watendaji wanavyoshiriki kukamilisha maono yake.

Nguvu ya diplomasia ya uchumi
Rais kama nembo ya maendeleo ya nchi amekuwa kinara wa kutengeneza diplomasia ya uchuimi.

Miongoni mwa njia hiyo ni kuhakikisha anajenga mahusiano mazuri kati ya serikali yake nan chi jirani.

Hivi sasa mazungumzo ya viongozi wa Mataifa ya Malawi na Msumbiji na Tanzania yanajikita katika kufungua uchumi wa wananchi wao.

Kila kiongozi wa Msumbiji na Malawi anaelewa kuwa jitihada kubwa za Tanzania ni kuhakikisha kila mwananchi ananufaishwa na matunda ya kufunguliwa kiuchumi. Wananchi jirani wa Msumbiji wanategemea kupata huduma na ununuzi wa bidhaa pamoja na kufanya utalii kwenye nchi yetu.

Diplomasia ya uchumi imejikita pia katika utalii.

Vivutio vya kila kona ukanda wa mikoa ya kusini ni miongoni mwa mambo yanayoifanya serikali ya awamu sita kuwa ya aina yake.

Kuelewa Dunia ya sasa.

Rais Samia kama kiongozi mkuu wan chi anaelewa kuwa diplomasia ya uchumi ndiyo nyenzo muhimu ya kuifungua nchi.

Mathalani katika takwimu zilizotolewa hivi karibuni kuhusu watanzania wanaoishi nje ya nchi wanavyochangia pato la taifa kwa Trilioni tatu, ni dhahiri hizi si fedha nyingi wala si ndogo.

Lakini kadiri Rais Samia anavyozunguka huku na huko na kuifanya nchi yetu ikaribishe wawekezaji na wanunuzi wa bidhaa za kitanzania ndivyo anavyoifungua nchi yetu zaidi.

Mathalani katika mikoa ya kusini imekuwa kivutio cha mataifa ya Msumbiji, Malawi, Zimbabwe, Zambia, Uingereza, Ujerumani na kadhalika.

Watu wengi kutoka mataifa hayo wamekuwa wakitembelea vivutio vya utalii.

Hata hivyo kutokana na serikali ya awamu ya nne kukamilisha ujenzi wa miundombinu unafungua mianya ya kuwavutia wawekezaji wakubwa kwenye maeneo hayo.

Mfano wawekezaji kwenye machimbo ya makaa yam awe wanaweza kujenga hoteli, kufungua sehemu za starehe,kufungua shule za sekondari binafsi na msingi kwa ajili watu wanaoshughulikia machimbo hayo.


Kwa maana hiyo hata wageni kutoka mataifa jirani nao watakuwa wanavutiwa na shughuli zinazoendelea na hivyo kuweza kuwaleta watoto wao kusoma kutokana na fursa wanazopewa na serikali ya Tanzania.

Uamuzi wa rais Samia kusimama kidete kuhusu kufungua diplomasia ya uchimi ndiyo kiini cha ubora wa maisha ya watanzania.

Kila mwananchi atakuwa ananufaika na fursa hizi.

Hakuna mwananchi ambaye anaweza kubeza namna juhudi hizi zinavyofanya kazi na kuwafikia wengi.

Fursa za diplomasia ya uchumi haziendi kwa wawekezaji pekee, badala yake huwafikia hata wananchi wa kawaida. Kuanzia mama lishe, maafisa usafirishaji,kampuni binafsi, watumishi wa umma na kadhalika.

Jitihada za serikali za kuijikita katika diplomasia ya uchumi inatokana na ukweli kwamba, ili kuongeza kiwango cha maisha ya wananchi wa kawaida lazima fursa zifunguliwe. Fursa hizo zinapaswa kutumiwa na watu wa kada zote bila kujali rika na jinsia.

Ni hapo ndipo utaona Rais Samia yuko katika mbio za nyika ambazo watendaji wake wanapaswa kuelewa sio zile za kulala usingizi.

Ni mbio za kuhakikisha mtandao mkubwa wa uchumi unawafikia wananchi wote bila ubaguzi, kuanzia huduma za afya,miundombinu, elimu na kadhalika.

Hakika utafiti wa Oxford ambao umebainisha namna nchi za kusini mwa Jangwa Sahara zinavyochochea ukuaji wa biashara na bidhaa ni dhahiri kuwa nchi hizo zinahitajiana.

Kwa kutambua hilo Rais Samia amewaweka karibu Malawi na Msumbiji, huku akiendelea na kuweka mazingira mazuri kwa watumiaji wajao wa Reli ya kisasa kwa maslahi ya taifa.